Ripoti ya Rais wa Tanzania
juu ya CCM na CUF
Taarifa ya Rais wa Tanzania
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambayo aliitoa siku ya tarehe
14/08/2007, Ikulu, Dar es Salaam juu ya maelewano ya vyama viwili hivyo
(CCM na CUF). JK alisisitiza kuwa yeye ni
mwenye shauku kubwa ya kuleta mapatano na maendeleo ya kuafikiana baina ya vyama hivi
na alikisisitiza chama cha (CUF) na uongozi wa chama hicho akiwemo Profesa
Ibrahim Lipumba kuwa kujitoa katika maongezi hayo hakutoleta maendeleo
ya maelewano. JK alieleza kuwa ataendelea kuleta maendeleo ya
maelewano kati ya vyama hivyo na alikumbusha chimbuko la mazungumzo hayo
ni ya ahadi aliyoitoa kwa Watanzania katika bunge tarehe 30 Disemba
2005. Alisema katika taarifa yake, anaamini kwa dhati ya moyo wake
kuwa hakuna tofauti zozote za kisiasa na kijamii katika nchi yetu zisizomalizwa kwa mazungumzo na
anaamini mpasuko huo wa kisiasa unaweza ukawafikiana ikiwa
vyama hivyo vitakaa pamoja na kuzungumzia tofauti zao. JK alisema katika
taarifa hiyo, mpaka sasa wameshakaa vikao vingi vya maelewano na
wameshaelewana katika sehemu tofauti za mazungumzo yao na anaamini kuna sehemu
chache tu zilizobakia ambazo pia zinaweza kumalizwa kimazungumzo.
Rais Kikwete alisema, mpasuko
huo wa kisiasa unaweza ukatatuliwa kimazungumzo ya maelewano ya pande
zote mbili; na kama mpasuko huo ukiendelea bila ya mazungumzo, tutarudi kule
tulikokuwa, yaani kwenye uhasama, shutuma zisizoisha, kubaguana,
kutozikana na hata kutosalimiana. Itakuwa tutaendelea na utamaduni mbaya wa
kuzifanya tofauti zetu za kisiasa kuwa ni chanzo cha uadui, chuki na
hivyo kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa taifa letu na watu wake.
Taarifa kutoka Ikulu, Dar es
Salaam, tarehe 14/08/2007 |