Uraia wa nchi mbili
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard
Membe, amesema serikali itahakikisha sheria ya uraia wa nchi mbili
inapitishwa kwa manufaa ya Watanzania na taifa na si vinginevyo.
Akizungumza na baadhi ya Watanzania waliokutana naye mjini New York
wiki iliyopita katika hoteli ya Grand Hyatt, Waziri Membe alisema
lengo la serikali ni kuwasaidia Watanzania na si kugawa uraia wa
Tanzania kwa wageni wenye uraia wa nchi zao.
Alisema haingii akilini ni kwa nini Mtanzania wa kuzaliwa
anyang’anywe uraia wa Tanzania kwa kuwa amechukua uraia wa nchi
nyingine kutafuta faida za kielimu, ajira au hata matibabu.
“Ni kwa nini tumuadhibu huyu Mtanzania wa kuzaliwa kwa kuwa tu
amechukua uraia wa nchi nyingine ili apate elimu ama ajira na
kusaidia ndugu zake waliobaki Tanzania?” alihoji Waziri Membe.
Waziri alisisitiza kuwa sheria hiyo itakapopitishwa haitatoa mwanya
kwa kila mtu kuuvamia uraia wa Tanzania bali itawalinda Watanzania
wanaotaka kuchukua uraia wa nchi za nje kwa manufaa yao na taifa kwa
ujumla.
Akitoa mfano mmojawapo bila kutaja majina ya wahusika, Waziri Membe
alisema anaifahamu familia moja ya Watanzania ambayo ililazimika
kuchukua uraia wa Kanada kwa sababu za matibabu, na kwamba
kuwanyang’anya uraia watu hawa ni kuwaadhibu bila kujali uhai wao.
Alieleza kuwa familia hiyo ina watoto wawili ambao matibabu yao
hugharimu dola 2,000 kwa kila mmoja kwa mwezi, na kwamba kwa
kuchukua uraia wa Kanada, matibabu hayo yanakuwa bure. Alihoji je,
ni haki kuwanyang’anya uraia wao wa Tanzania?
Akitoa mfano wa manufaa yanayopatikana Ghana, Waziri Membe
aliwaambia Watanzania hao kwamba ni muhimu kwa Tanzania kutumia raia
wake walioko nje kwa manufaa ya taifa na siyo kuwabagua.
“Mwaka jana pekee wananchi wa Ghana walioko nje waliingiza dola
bilioni 2.5 kwa njia mbalimbali halali,” na akaongeza: “Taifa dogo
kama Komoro, mwaka jana lilipata dola milioni 89 kutoka kwa wananchi
wake walioko Ufaransa pekee.
Akifafanua zaidi, Waziri Membe alisema wakati akiwa Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani kwa kipindi kisichofikia miaka miwili, Tanzania
ilitoa uraia kwa wageni 101 na kushangaa ni kwa nini Watanzania wa
kuzaliwa wapoteze uraia wao.
Waziri Membe aliwataka Watanzania kujenga umoja thabiti na
kuwahakikishia kwamba serikali itakuwa pamoja nao ili kuleta
maendeleo kwa taifa, na kwamba mawazo kuwa usalama wa taifa utakuwa
hatarini si la jambo kuhofia iwapo sheria itatungwa vizuri.
Tanzania ina raia wake waliosambaa nchi mbalimbali duniani huku
idadi kubwa ikiwa katika nchi za Kiarabu za Ghuba ambako wakati
serikali ikiongeza ofisi moja ya Ubalozi nchini Oman miaka michache
iliyopita ilikadiria kuwa kuna Watanzania laki tano.
Nchi nyingine ambazo Watanzania wanakadiriwa kuwa wengi ni za
Marekani Kaskazini na Ulaya Magharibi ambako wako kwa maelfu, ambao
wengi wao hukabiliwa pia na utata wa uraia wa watoto wao wanaozaliwa
ugenini.
Mjadala wa suala la uraia wa nchi mbili umekuwa ukiendelea nchini
katika siku za karibuni ambako kumeibuka kambi za wanaopinga kwa
madai ya kulinda maslahi ya nchi na wanaounga mkono kwa madai hayo
hayo ya kulinda maslahi ya nchi.
Habari na
Mobhare Matinyi, New York.
|