![]() |
|
![]() |
||||||
|
|
|
|||||||
|
|
||||||||
|
|
||||||||
|
|
||||||||
|
NEWS |
||||||||
|
|
||||||||
Watuhumiwa wa EPA hawakuhepa kizimbani06/11/2008
Kachero Koba Kimanga 'Assossa' (kushoto) akimuelekeza Jeetu Patel pa kwenda wakati watuhumiwa wa EPA walipofika mahakama ya Kisutu kujibu tuhuma za EPA.
Watuhumiwa wakiwasili mmoja baada ya mwingine katika mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam.
Baadhi ya watuhumiwa wakiwa wamechuchumaa kusubiri kuingizwa mahakamani Kisutu.
Jeetu Patel (pichani katikati) anayetajwa kuwa kinara katika wizi wa Sh bilioni 133 kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na wenzake tisa, walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuiibia benki hiyo. Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ni Devendra Vinodbhai Patel na Amit Nandy, Ketan Chohan, Johnson Lukaza, Bahati Mahenge, Davies Kamungu, Godfrey Mosha na Manase Mwakale anayeshitakiwa na mkewe, Eddah Mwakale, ambaye ndiye mwanamke pekee katika kesi hiyo ya EPA.
Jeetu, ambaye jina lake halisi ni Jayantkumar Chandubhai Patel, katika moja ya kesi anazokabiliwa nazo, anashitakiwa kwa pamoja na Devendra Vinodbhai Patel na Amit Nandy.
Washitakiwa hao pia wanatakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani, wanatakiwa wasisafiri nje ya mkoa hadi kwa ruhusa ya mahakama. Sharti jingine ni kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi wataripoti kwa mwendesha mashitaka na pale wanapokuwa na matatizo, wadhamini wao watalazimika kwenda kutoa taarifa mahakamani. Kwenye shitaka hilo, washitakiwa wanatuhumiwa kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuiba na kujipatia Sh bilioni 2.6 kwa kutumia kampuni yao ya Bencon ya Dar es Salaam. Wanadaiwa waliiba fedha hizo baada ya kudanganya kuwa Kampuni ya Matsushita Electric Trading Company iliwapa jukumu la kulipwa fedha hizo kupitia kampuni yao ya Bencon International Ltd. Washitakiwa hao pia kwa pamoja wanashitakiwa kula njama, kughushi, kuiba na kujipatia tena Sh bilioni 7.9 kwa kutumia kampuni hiyo ya Bencon International Ltd. Katika wizi huo, washitakiwa hao wanadaiwa kudanganya kuwa walipewa jukumu la kulipwa fedha hizo na Kampuni ya Maruben Corporation ya Japan wakati wanajua kuwa si kweli. Hakimu Euphamia Mingi alisema dhamana kwa washitakiwa ziko wazi, ila kila mshitakiwa anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha anazodaiwa kuiba, wadhamini wawili na mmoja kati yao awe ndugu wa karibu na wote watasaini hati ya dhamana. Jeetu pia anashitakiwa katika kesi nyingine na Ketan Chohan na Amit Nandy ambao wanadaiwa kuiba Sh bilioni 3.3 kwa kutumia Kampuni ya Navy Cut Tobacco Tanzania Limited. Walidanganya kuwa wameruhusiwa na Kampuni ya Matsushita Electric Trading Company ya Japan walipwe fedha hizo. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Neema Chusi na uamuzi wa dhamana yao utatolewa leo. Kinara huyo, pia anashitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 3.9 ambazo aliiba kwa kutumia kampuni ya Bina Rosorts Ltd kwa kudanganya kuwa walipewa mamlaka ya kulipwa fedha hizo na Kampuni ya C. Itoh & Company Ltd ya Japan. Katika shitaka hilo anashitakiwa kwa pamoja na wenzake Devenra Vinodbhai Patel na Nandy na kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Richard Kabate. Katika shitaka jingine, Jeetu anashitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 4.9 kwa kushirikiana na Devenra na Nandy. Wote wanatuhumiwa kufanya wizi huo kwa kutumia Kampuni ya Maltan Mining Company Ltd wakidanganya kuwa wameruhusiwa na Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan walipwe fedha hizo na BoT. Mtuhumiwa mwingine aliyefikishwa mahakamani jana ni Johnson Lukaza ambaye naye anatuhumiwa kula njama, kughushi, kuwasilisha hati ya uongo, kuiba na kujipatia Sh bilioni 6.3. Mtuhumiwa huyo na mwenzake aliyetajwa kwa jina la Mwesiga Lukaza ambaye hakuwapo mahakamani, wanadaiwa kufanya wizi huo Desemba 2005. Dhamana kwa kila mshitakiwa iko wazi ila mshitakiwa anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha anazodaiwa kuiba na wadhamini wawili na mmoja kati yao awe ndugu wa karibu, wote watasaini hati ya dhamana. Mshitakiwa pia anatakiwa kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani, anatakiwa asisafiri nje ya mkoa hadi kwa ruhusa ya mahakama. Sharti jingine ni kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi ataripoti kwa mwendesha mashitaka na pale anapokuwa na matatizo wadhamini wao atalazimika kwenda kutoa taarifa mahakamani. Wengine waliopanda kizimbani ni Bahati Mahenge, Davies Kamungu, Godfrey Mosha na Manase Mwakale anayeshitakiwa na mkewe, Eddah ambaye ni mwanamke pekee katika kesi hiyo. Washitakiwa wanatuhumiwa kuiba Sh milioni 855.4 ambazo waliiba kwa kutumia Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex Ltd baada ya kuwasilisha nyaraka za kughushi BoT wakionyesha kuwa kampuni hiyo, mkurugenzi wake Samson Mapunda ndiye aliyetoa idhini ya kulipwa fedha hizo. Watu hao pia walishitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 1.2, mali ya BoT baada ya kutumia kampuni ya Changanyikeni Residential Complex Ltd wakidai wamepewa mamlaka ya kulipwa fedha hizo na kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan. Uamuzi wa dhamana yao utatolewa kesho na Hakimu Victoria Nongwa. Akihutubia Taifa Ijumaa iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alisema Sh bilioni 69.3 ambazo ni sawa na asilimia 76.7 ya Sh bilioni 90.3 zilizochotwa kutoka EPA, zilikuwa zimerejeshwa kufikia Oktoba 31. Hata hivyo, aliagiza kuwa wote ambao kufikia siku hiyo (Oktoba 31, 2008), watakuwa hawajatekeleza agizo la kurejesha fedha hizo, hatua za kisheria zichukuliwe. Alitoa maelekezo kamili kwa ambao hawakutimiza malipo, majalada yao yakabidhiwe kwa Mkurugenzi wa Mashitaka mara moja, kwa hatua zipasazo za kisheria. Kampuni 23 zinadaiwa kuchota fedha, Sh bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya BoT, na iligundulika baada ya ukaguzi wa hesabu uliofanywa na Kampuni ya kigeni ya Ernst & Young katika mwaka 2005/2006 ambayo ilipewa kazi iliyoachwa na Deloitte & Touche ya Afrika Kusini. Chanzo na maelezo zaidi juu ya mchaka-mchaka huo rejea habari ya Zenjydar ya tarehe 09/01/2008 au bonyeza hapa. |
||||||||
|
Custom Search
|
||||||||
|
|
|
|||||||
|
©
www.zenjydar.co.uk - Since 2007 |
|
||||||||