TID (Khalid Mohammed)
ahukumiwa kifungo cha mwaka
24/07/2008

MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya (Bongofleva),
Khalid Mohamed maarufu kama T.I.D (pichani) amehukumiwa kutumikia
kifungo cha mwaka mmoja jela kufuatia kupatikana na hatia ya kushambulia
na kujeruhi.
T.I.D mwenye umri wa miaka 26 alisomewa adhabu yake hiyo na Hakimu
Hamisa Kalombola wa Mahakama ya wilaya ya Kinondoni baada ya Hakimu huyo
kuridhika na ushahidi ulitolewa na mashahidi wanne walioletwa mahakamani
na upande wa mashtaka.
Baada ya kusikiliza ushahidi huo, ndipo Hakimu Kalombola alisema
ushahidi uliotolewa na mashahidi hao wanne ulithibitisha mtuhumiwa
kufanya kosa hilo na hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kosa hilo.
Mara baada ya kusema hivyo Hakimu alitoa nafasi kwa Mwendesha Mashtaka,
Inspekta wa Polisi, Benedict Nyagabona ambaye alimwomba Hakimu kutoa
adhabu kali kutokana na tabia iliyokithiri ya watu kujichukulia sheria
mkononi kama alivyofanya mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye
tabia kama hiyo.
Baada ya maelezo hayo ya Mwendesha Mashtaka ndipo Hakimu alitoa nafasi
kwa mshtakiwa TID kutoa utetezi wake, ambaye aliiomba mahakama imhurumie
kwani alitenda kosa hilo sababu ya ulevi na kuwa familia yake
inamtegemea hasa mama yake.
Hata hivyo Hakimu Kalombola alitoa hukumu hiyo kwa kumwambia mshtakiwa
“kwa vile huwezi kujimudu ukilewa na huwezi kujizuia kunywa sasa na
kuhukumu uende jela mwaka mmoja ujifunze ili usiwe unakunywa hizo pombe”.
Baada ya hukumu hiyo ambayo ilipokelewa kwa mshtuko mkubwa na msanii
huyo aliyeng’ara sana katika fani hiyo ya muziki wa Bongofleva akiwa na
bendi yake ya Top Band, ndugu na jamaa zake waliangua kilio mahakamani
hapo wakati TID akipelekwa kwenye karandinga tayari kwenda kutumikia
kifungo hicho katika gereza la Segerea.
Wakati akipelekewa kwenye karandinga hilo, TID aliishiwa nguvu na
kuanguka mahakamani hapo na kubebwa na wenzake ambao baadhi yao walikuwa
wamekwisha hukumiwa na wengine bado wakiwa watuhumiwa na kumwingiza
kwenye gari hilo.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, Inspekta Nyagabona, T.I.D alimjeruhi
Ben Mashiba kichwani na mkononi kwa kutumia chombo cha kuwekea majivu ya
sigara ‘Ash Tray’ na alisomewa mashtaka hayo mara ya kwanza Julai 10
mbele ya Hakimu Kalombola.
Mwendesha Mashtaka huyo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa
hilo Julai 2 mwaka jana saa sita na nusu usiku katika hoteli ya Slipway
iliyopo maeneo ya Msasani jijini Dar es Salaam.
|