Kikwete afanikiwa
kuwapatanisha Kabila na Museveni
11/05/2008

JK akiwa katika
mazungumzo na marais Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila wa
jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, ikulu, Dar leo hii ambapo JK aliweza
kuwapatanisha viongozi hao ambao nchi zao zilikuwa zimewekeana bifu kwa
muda mrefu. Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamezungumzia ufunguzi
wa ofisi za kibalozi katika nchi zao.
RAIS Jakaya Kikwete amefanikiwa
kuwapatanisha marais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) na Yoweri Museveni wa Uganda ambao sasa wanaangalia uwezekano wa
kufungua ofisi za ubalozi katika nchi zao.
Marais hao wawili waliwasili nchini jana asubuhi kwa ziara ya siku moja
ya kikazi kufuatia mwaliko wa Rais Kikwete na wakatumia fursa hiyo
kujadili hali tete ya uhusiano baina yao na masuala ya usalama na uchumi.
Rais Kikwete ndiye aliyeanzisha mchakato wa mazungumzo hayo ya amani kwa
kuwakutanisha marais hao kwa mara ya kwanza huko Ngurdoto, Arusha, mwaka
jana, wakati huo uhusiano kati ya Uganda na DRC ulikuwa usababishe nchi
hizo mbili zipigane vita.
Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho kilichofanyika Ikulu na
kusomwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe ilisema katika suala la usalama Kabila na Museveni walikubaliana
kuondoa uhasama wa kijeshi katika mpaka baina yao.
Ilisema viongozi hao ambao waliondoka kurudi kwao baadaye jioni,
walimsisitiza kiongozi wa uasi wa kikundi kinachopingana na Serikali ya
Uganda cha Lord’s Resistance Army (LRA) Joseph Kony, kufuata makubaliano
ya Juba yanayomtaka kuacha kuendeleza vita.
Kuhusu ushirikiano katika sekta ya uchumi wakuu hao walieleza
kuridhishwa na ushirikiano uliopo ikiwamo haja ya kusainiwa mikataba ya
maendeleo baina ya mawaziri wa madini, nishati na umeme.
Pia walikubaliana kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni
pamoja na kuomba misaada ya fedha kutoka Jumuiya ya Ulaya na mashirika
mengine kufadhili mradi wa umeme kati ya Uganda Magharibi na kaskazini
mashariki mwa DRC.
Baada ya mazungumzo hayo ya jana, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais wa
Uganda anayeshughulikia Mambo ya Nje, Isaac Msumba na mwenzake wa DRC
Mbusa Nyamisi walisaini mikataba ya makubaliano.
Akizungumza baadaye, Waziri wa Ulinzi wa DRC Chikez Diemu alisema kuwa
jeshi la nchi hiyo litalazimika kutumia nguvu kuwaondoa raia wa Uganda
ambao watakaidi kurudi nchini kwao kutoka Kongo kwa hiyari.
Diemu alisema kuwa nchi hizo mbili zinatakiwa kuacha mapambano na kuanza
upya kujenga nchi zao katika uchumi kuweza kuleta maendeleo.
Mkutano huo ulichukua takribani saa nne huku ambako kila upande
ulionyesha kuridhishwa na makubaliano hayo.

Makamu wa Rais Dk Ali
Mohamed Shein akimshindikiza Rais wa Jamhuri ya watu wa Kongo Mh. Joseph
Kabila baada ya mkutano wake na rais JK na rais Yoweri Museveni.
|