Maajabu ya Pete - Dar es
Salaam
16/10/2008

OMARI HAMISI, 28, ni
kijana aliyekumbwa na balaa la pete kung'ang'ania vidoleni. Kisa chake kinaendelea kuleta msisimko
mkubwa baada ya yeye mwenyewe kueleza bayana kwamba tangu avae pete hizo,
hana amani kabisa.
Akiongea na waandishi wa habari, Omari
amesema, usiku anapokuwa usingizini hupatwa na hali isiyo ya kawaida.
Anasema hali hiyo ya ajabu haikuwahi kumpata kabla ya kuokota pete hizo
na kuziweka vidoleni mwake. Amesema hali hiyo imekuwa ikimtokea kwa
miaka mitatu sasa tangu alipovaa pete hizo.
Omari amesema, "Tangu nizivae miaka mitatu
iliyopita, sikuwahi kuzivua, usiku huwa napatwa na hali nisiyoielewa
ambayo kabla ya kuzipata pete hizo sikuwa na hali hiyo".
Wakati Omar mwenyewe anaeleza hayo, Mtabiri
maarufu katika nchi za Afika Mashariki,
Sheikh Yahya Hussein amejitokeza na kutoa maelezo
aliyodai kuwa yataokoa maisha ya kijana huyo ambaye hadi sasa amelazwa
katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na madaktari wanahaha kutafuta namna ya
kumsaidia.
Sheikh
Yahya amesema, kama kitendo cha pete hizo kung'ang'ania vidoleni
kinahusiana na mambo ya kishirikina, basi kinachotakiwa kufanywa ni
kumenya vitunguu thumu, kuviponda ponda na kisha kufukiza huku moshi
wake ukielekea kwenye vidole hivyo. Amesema iwapo pete hizo ni za majini
basi yatatimuka na madaktari wataweza kufanikiwa kuzitoa kwa kuzikata
bila matatizo.
Sheikh Yahya amesema, "Kuna majini huwa
yanatupa pete na mtu anapookota basi anaweza kupata matatizo kama hayo".
Ameongeza kuwa iwapo zoezi hilo la kitunguu
thumu halitafanikiwa, basi ni budi zitafutwe njia nyingine za kumsaidia
kijana huyo.
"...siku ya kwanza tulianza kazi ya kuondoa
pete zile kwa kutumia sabuni na mafuta, lakini ilishindikana baada ya
kuonekana kuwa ngumu kiasi cha kutisha", alisema mmoja wa wauguzi ambaye
hakutaka jina lake litajwe.
Hata hivyo, madaktari hawakuishia hapo
kwani waliamuru apelekwe katika chumba maalum chenye vifaa vya kuondolea
vyuma mwilini, huko ndipo maajabu ya pete hizo yalipoanza kuonekana.
Inasemekana kila walipozigusa kwa mashine
hiyo kwa nia ya kuzikata, pete hizo zilitoa cheche za moto ambao ulikuwa
ukimuunguza mgonjwa huyo. Hata hivyo, alipoulizwa Afisa Uhusiano wa MOI,
juu ya sakata hilo alisema, mgonjwa huyo bado anaendelea kulazwa
hospitalini hapo wakati madaktari wanaendelea kufikiria njia ya kuondoa
pete hizo ambazo zimesababisha vidole vyake kuanza kuvimba.
|