Wakimbizi wa Burundi
kuomba uraia Tanzania
24/10/2008

Habari na Muandishi Maalum, Urambo,
Tabora
FAMILIA
8,307 za wakimbizi wa Burundi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya
Ulyankulu, wilayani Urambo, Mkoani Tabora, wameomba uraia wa Tanzania,
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameambiwa leo, Ijumaa, Oktoba 24, 2008.
Akiwasilishiwa taarifa ya utendaji wa Serikali katika Wilaya ya Urambo
katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nane katika Mkoa wa Tabora
mjini Urambo, Rais Kikwete ameambiwa kuwa familia hizo zina jumla ya
wakimbizi 40,886.
Taarifa
hiyo imesema kuwa baada ya baadhi ya wakimbizi kukubali kurejea nyumbani
kwao Burundi, kiasi kubwa cha wakimbizi wameomba uraia wa Tanzania baada
ya kuwa wamekaa nchini kwa miaka mingi kama wakimbizi.
Baada ya
kuwa amejulishwa habari hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni vyema kuachia
mchakato wa kuomba uraia kuendelea kwa kushughulikiwa na taasisi husika,
na kuwa baada ya kuwa umekamilika Serikali itachukua uamuzi kuhusu wapi
wataishi wakimbizi hao.
Hata
hivyo, amesema kuwa wakimbizi hao hawataruhusiwa kukaa katika eneo hilo
la Ulyankulu, na badala yake watahamishiwa katika sehemu mbali mbali
nchini.
“Tuachia
mchakato uendelee wa kuwapa uraia wa Tanzania kama wanazo sifa za kupata
uraia huo. Lakini lazima kusema kuwa wakishakuwa wamekubaliwa kuwa raia
wa Tanzania watasambazwa nchi nzima, kwa sababu hawaombi kuwa raia wa
Ulyankulu, bali raia wa Tanzania,” amesema Rais Kikwete.
Ameongeza: “Wajue na wajulishwe kuwa wanaomba kuwa raia wa Tanzania, na
siyo kubakia Ulankulu. Vinginevyo, wakiendelea kubakia katika eneo la
sasa la ukimbizi wataendelea kuwa wakimbizi. Lakini kwanza tuangalie
maombi yao na kuyachambua vizuri.”
Akizungumzia suala la mauaji ya albino kwenye kikao hicho, baada ya kuwa
amepongezwa na wilaya kwa msimamo wa Serikali yake kuhusu mauaji hayo,
Rais amesema kuwa ni ujinga kudhani kuwa ukikata na kupata kidole cha
albino basi utaweza kupata utajiri.
“Sasa
kama utajiri si wangeupata albino wenyewe kwa sababu wao wanacho kila
kitu, wanayo mikono, wanazo nywele, wanavyo vidole, sasa kwa nini kama
viungo hivyo vinaleta utajiri wasiwe matajiri wakubwa wa nchi yetu,”
ameuliza kwa mshangao Rais Kikwete.
“Ni
lazima watu wanaotaka kuwa matajiri wajue kuwa utajiri ni matokeo ya
kufanya kazi kwa bidii, kwa maarifa na kwa nidhamu na siyo kuchuna ngozi
ama kukata na kukimbia na viungo vya albino,” amesema Rais Kikwete.
Rais pia
ameonyesha mshangao wake kwa baadhi ya watu na taasisi zinazoilaumu
Serikali kutokana na mauaji ya albino.
"Kuilaumu
Serikali kwa ukatili huu siyo jawabu. Hakuna mtu wa Serikali
anayewashauri wauaji hao wa albino kuwafukuza wenzetu hawa na kuwakata
viungo vya miili yao.
La
msingi ni kwa taasisi zote, watu binafsi na Serikali,kushirikiana
katika kutafuta jawabu la ujinga huu.”
|