MV Kigamboni yakwama
kivukoni
30/10/2008

Chini ni MV Kigamboni
ikiwa imekwama baada ya kuparamia gati kivukoni, na juu pichani, umati
wa wasafiri wakigombea kuingia kwenye MV Alina leo (jana) asubuhi upande
wa Kigamboni.

HABARI KAMILI:
Mamia ya
wakazi waishio maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam leo (jana)
wamepata adha ya usafiri baada ya kivuko cha MV. Kigamboni kukwama
katika eneo la Feri ya kigamboni kuanzia majira ya saa 11.30 (kumi na
moja na nusu) alfajiri.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi wa eneo hilo
wamesema kuwa adha hiyo imetokana na uzembe wa nahodha wa kivuko hicho
ambaye ameshindwa kuangalia hali ya bahari ikoje.
“Nahodha
anatakiwa kujua tarehe kama hizi na majira kama yale ni kipindi cha maji
kupwa hivyo hakutakiwa kuipandisha pantoni juu lakini yeye hakuzingatia
hilo akalipandisha juu na kuchelewesha kulitoa na matokeo yake ndio haya
tunayoyaona”, alilalamika Feisal Ally ambaye ni mvuvi.
Wavuvi
hao pia walishauri ni muhimu kwa manahodha wa vyombo vya majini waelewe
na kuzingatia majira ya bahari hii itawasaidia kuepukana na matatizo
mbalimbali kama ya kushindwa kuendesha vyombo vyao.
Kuzama
kwa kivuko hicho kumesababisha msongamano mkubwa wa watu waliokuwa
wanaelekea maeneo ya mjini na Kigamboni hivyo wale waliokuwa na fedha za
kutosha pamoja na ujasiri waliweza kupanda mitumbwi kwa kulipa nauli ya
Tshs. 500 hadi Tshs. 1000.
Naye
Mohamed Abdulla mkazi wa Kigamboni alieleza kwa masikitiko makubwa kuwa
amelazimika kutoa Tshs. 2000 kukodisha mtumbwi ili aweze kuvuka ng’ambo
ya pili na kuwahi katika kongamano la haki za binadamu linaloendelea
huko Ubungo Plaza”.
Baadhi
ya madereva wa magari yaliyokuwemo ndani ya pantoni hiyo walisema kuwa
baada ya pantoni kuwashwa ilishindwa kuondoka baada ya hapo ilikuja TUG
ya mamlaka ya bandari na kuivuta mara tatu kitu ambacho hakikusaidia
kwani mara zote tatu kamba ilikatika.
Baada ya
pantoni hiyo kushindwa kuondoka watu waliokuwepo ndani walianza kushuka
kwa haraka kwa kuhofia kuzama hali iliyopelekea baadhi ya watu
kukanyagana na kuumizana. Kutokana na hali hiyo Aneth Kasongo alianguka
na kukanyagwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na hivyo kuumia mguu wa
kulia.
Ndani ya
Pantoni hiyo kulikuwa na magari 16 ambapo hadi waandishi wa habari hizi
wanaondoka eneo la tukio magari 14 yalikuwa hayajatolewa na madereva
wake walikuwa wanasubiri maji yajae ili pantoni iweze kutoka na kuyatoa
magari yao.
Hata
hivyo msongamano huo wa watu ulipungua baada ya kivuko kidogo cha M.V
Alina kufanya kazi kwa haraka ya kuvusha abiria tu kwani huku askari wa
Jeshi la wananchi na Polisi wakiendelea kuimarisha hali ya usalama
katika eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo Mtendaji mkuu wa vivuko nchini, Frednand Mishama,
alisema kuwa ofisi yake inasikitishwa na hali hiyo iliyojitokeza na pia
kupongeza juhudi zilizochukuliwa mpaka sasa za kujaribu kuweka hali sawa.
Mishama
aliendelea kusema kuwa taarifa rasmi juu ya tukio hilo itatolewa ndani
ya siku tatu kuanzia leo (jana) kuelezea chanzo cha tatizo hilo baada ya
kufanya uchunguzi wa kina. Kuhusu kukitoa kivuko hicho amesema
wanasubiri bahari ijae ili waweze kuitoa.
Tatizo
la kukwama kwa kivuko hicho limekuwa la muda mrefu na kuwa kero kwa
wakazi wa Kigamboni, hivyo basi kutokana na hali hiyo wameiomba serikali
ikamilishe kivuko kipya haraka iwezekanavyo ili lisije lisije likatokea
janga kubwa zaidi ya haya yanayotokea hivi sasa.
Kutokana
na maelezo yaliyotolewa na wavuvi pamoja na wenyeji wa Kigamboni wanadai
kuwa kwa tarehe za hivi karibuni maji yanakupwa kuanzia majira ya saa
kumi na moja na nusu alfajiri na kujaa kuanzia majira ya saa sita mchana
hivyo basi baada ya maji kujaa pantoni inaweza kutoka na kuendelea
kufanya kazi kama kawaida.
|