Hotuba ya Rais Kikwete kwa
wananchi - Oktoba 2008
31/10/2008

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Jakaya Kikwete akizungumza na taifa kupitia utaratibu wa hotuba za
kila mwisho wa mwezi. Hotuba hizi hutolewa na mwenyewe Rais Jakaya
Mrisho Kikwete kila mwisho wa mwezi kwa dhumuni la kujulisha wananchi
mikakati, migogoro na maendeleo mbalimbali ya nchini Tanzania. Hotuba
hiyo hutolewa kwa njia ya Televisheni na Redio nchini Tanzania.
HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI YA RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI TAREHE 31 OKTOBA, 2008:
Ndugu
Wananchi;
Tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia rehema zake tunapata
fursa ya kuzungumza mwisho wa mwezi huu Oktoba kwa mujibu wa utaratibu
wetu mzuri. Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kuzungumza nanyi kwa
sababu ya kuwa New York, Marekani kwa shughuli za kila mwaka za Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa.
Suala la OIC:
Ndugu
Wananchi;
Hivi karibuni kumekuwepo na mjadala usiofurahisha kuhusu suala la
Jumuiya ya Kiislamu (OIC) kufuatia taarifa iliyotolewa Bungeni na kwenye
vyombo vya habari na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mheshimiwa Bernard Membe.
Nasema
isiyofurahisha kwa sababu mjadala huo unaelekea kuchukua sura ya
malumbano baina ya waumini wa dini zetu kuu na kupandikiza chuki baina
ya serikali na wafuasi wa dini hizo. Ni mjadala unaosikitisha sana jambo
ambalo napenda kuwasihi Watanzania wenzangu tusiuendeleze na wala
tusiuendekeze.
Unaweza kulipeleka taifa letu mahali
pabaya.
Napenda
kukumbusha kuwa mwaka 1993 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitakiwa
kujiondoa kutoka kwenye jumuiya ya OIC baada ya kujiunga kwa hoja kwamba
hilo ni shirika la kimataifa ambalo wanachama wake ni mataifa, hivyo kwa
hapa nchini kama kungekuwepo na kujiunga iliyostahili kufanya hivyo ni
Serikali ya Muungano.
Hayo
ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilijiondoa kwenye OIC na kuiachia
Serikali ya Muungano kushughulikia jambo hilo na kuamua ipasavyo.
Tangu
wakati huo Zanzibar wamekuwa wanasubiri uamuzi wa Serikali ya Muungano.
Kila wakati wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa
wanaliuzia suala hilo. Hivi sasa jambo hilo limekuwa mojawapo ya kero
kubwa za Muungano zinazoshughulikiwa na Kamati ya pamoja ya Waziri Mkuu
na Waziri Kiongozi. Kwa mujibu wa muundo wa Serikali ya Muungano kila
kero ya Muungano ina Wizara yake inayohusika nayo kushughulikia. Kwa
suala hili ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ndiyo
inahusika. Wizara imeamua kufanya utafiti wa jambo lenyewe na
wakishakamilisha utafiti huo watoe ushauri kwa Serikali zetu mbili kwa
uamuzi.
Ndugu
Wananchi;
Nijuavyo mimi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
haijakamilisha kazi yake ya utafiti na hivyo haijawasilisha Serikalini
matokeo ya utafiti wao pamoja na mapendekezo yao kwa ajili ya
kutafakariwa na kuamuliwa ipasavyo. Kwa sababu hiyo basi Serikali
haijafanya uamuzi wowote kuhusu suala la OIC kwa vile hatujapokea
mapendekezo yoyote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa. Wizara haijamaliza kazi yake.
Katika
hali hii, nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na subira. Tuwaache Wizira
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wafanya kazi yao kwa utulivu
ili waishauri Serikali kwa hekima na busara.
Aidha,
napenda kuwaomba pia hapo Wizira itakapokamilisha kazi yake (sijui lini)
na kuyafikisha mapendekezo yake Serikalini, tuiache Serikali yetu nayo
itafakari kwa utulivu ili ifanye uamuzi ya hekima utakaojenga na
kulihakikishia taifa letu umoja, amani, utulivu na upendo miongoni mwa
raia wa nchi yetu.
Ndugu
zangu;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa siku zote mimi na
wenzangu wote Serikalini tunatambua unyeti wa suala la OIC. Aidha,
tunatambua dhamana yetu ya kuwa makini katika kufikia uamuzi na kwa
uamuzi wenyewe tutakaoufanya kuhusu suala hili. Kamwe hatutafanya uamuzi
ambao utavuruga mambo na kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi
yetu, Serikali zetu na watu wake.
Hivyo
narudia kuwasihi Watanzania wenzangu tuiache Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa ilifanyie kazi kwa ukamilifu suala hili.
Tujiepushe na vitendo au kauli ambazo zitawatia watu hofu na kujenga
chuki miongoni mwa raia wa nchi yetu wanaopendana na kujenga chuki na
kutoaminiana baina ya raia na Serikali yao inayowapenda na kuwathamini.
Madai ya Malimbikizo ya Walimu:
Ndugu
Watanzania wenzangu;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia leo, linahusu madai ya malipo ya
walimu kuhusu malimbikizo ya mishahara, nauli za likizo na posho za
uhamisho na kujikimu. Kama sote tujuavyo Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
kiliiarifu Serikali nia yake ya kuitisha mgomo wa walimu wote nchini
iwapo madai ya walimu yapatayo shilingi bilioni 16.4 (bilioni 12.2 kwa
ajili ya walimu wa shule za msingi na bilioni 4.2 kwa walimu wa shule za
sekondari na vyuo vya walimu) yatakuwa hayajalipwa yote ifikapo tarehe
15 Oktoba, 2008.
Baaada
ya kupata taarifa hiyo Serikali iliwasiliana na uongozi wa juu wa CWT
kwa nia ya kufanya mazungumzo nao kuhusu madai yao. Bahati nzuri uongozi
wa CWT ulikubali, hivyo mazungumzo yakafanyika baina ya Serikali na CWT.
Upande wa Serikali uliwakilishwa na
wajumbe 12 kutoka Wizara za Utumishi, Fedha na Mipango, TAMISEMI na
Elimu na Mafunzo ya Ufundi na upande wa CWT uliwakilishwa na wajumbe
saba (7).
Kiongozi
kwa upande wa Serikali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Hawa Ghasia na upande wa CWT
kiongozi alikuwa Ndugu Yahaya Msulwa ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama
cha Walimu, Tanzania.
Katika
mazungumzo hayo ukiacha suala la madai ya malipo yalikuwepo pia masuala
mengine matano yafuatayo:
1.
Kupandishwa madaraja (vyeo).
2. CWT kushirikishwa katika uhakiki wa madai ya walimu.
3. Kuundwa kwa Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Sekta ya Elimu
(Teachers Joint Staff Council).
4. Kuandaliwa kwa Taratibu za Uendeshaji wa Utumishi wa Walimu (Teachers
Service Scheme) na
5. Kuwarudisha kwenye Orodha ya Malipo (Payroll) walimu waliofutwa
kwenye orodha hiyo.
Baada ya siku 15 za mazungumzo muafaka ukafikiwa juu ya masuala yote
sita na makubaliano hayo ya pamoja kutiwa saini na Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe kwa niaba ya
Serikali na Katibu Mkuu wa CWT, Ndugu Yahaya Msulwa kwa niaba ya Walimu.
Jambo
lililotushangaza na kutusikitisha sote ni kauli ya Rais wa CWT, Ndugu
Gratian Mkoba tarehe 08 Oktoba, 2008 kwamba mgomo unaendelea.
Tena
akasisitiza kuwa mgomo huo hauna muda maalum mpaka mwalimu wa mwisho
atakapokuwa amelipwa.
Nilimuagiza Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi kuwa, wawatafute viongozi wa CWT kuzungumza nao kuwasihi
waache kuendelea na mgomo, lakini juhudi zote hazikuzaa matunda.
Waling’ang’ania kuendelea na mgomo na ndipo tukaitumia haki yetu kwa
mujibu wa Sheria ya Kazi Na. 6 ya mwaka 2004 kuomba Mahakama kuu kitengo
cha Kazi iamuru mgomo usiwepo na kuwataka viongozi wa CWT warudi kwenye
mazungumzo na Serikali. Viongozi wa CWT wanapinga uamuzi huo wa Mahakama
Kuu na kutaka waendelee na mgomo. Tupo mahakamani tunasubiri uamuzi wa
Mahakama kuhusu rufaa ya CWT.
Ndugu
wananchi;
Najua wapo walioushangaa uamuzi wa Serikali wa kwenda mahakamani na wapo
pia watu waliotukejeli kwa uamuzi wetu huo. Kwanza kabisa ni haki ya
mwajiri kufanya hivyo na mahakama ndicho chombo chenye mamlaka ya kuamua.
Lakini, pia, tumefanya hivyo kwa nia njema ya kunusuru janga ambalo
mfumo wa elimu ungelikuta nchini kwa mgomo huo ambao ungekuwa wa aina
yake.
Maana
kuendelea kuwepo mpaka mdai wa mwisho atakapolipwa wakati inawezekana
baadhi ya wadai wanaweza kuwa na vithibitisho ambavyo vinaweza
kukataliwa na mlipaji kwa kutokuwa halali ni sawa na kuwa na mgomo wa
kuchukua muda mrefu sana.
Unaweza usiwe na ukomo kwani ubishi
kuhusu uhalali wa stakabadhi ya mdai unaweza kuchukua muda mrefu.
Vinginevyo ichukuliwe kuwa, kila anachodai mwalimu ni sahihi kilipwe na
Serikali. Hilo nalo ni gumu kwani upo ushahidi wa kuwepo kwa stakabadhi
za kughushi.
Ndiyo
maana sisi katika Serikali tumeyaafiki makubaliano ya kufanya uhakiki wa
pamoja utakaoshirikisha CWT na Serikali.
Nilipokuwa Tabora hivi karibuni nilielekeza kuwa uhakiki huo ufanywe
shule kwa shule na mwalimu kwa mwalimu; usifanywe kwa kukagua mafaili tu
katika maofisi ya Maafisa Elimu na Utumishi. Kufanya hivyo kutatupa
taarifa iliyo sahihi ya nani anadai nini. Itasaidia kung’oa mzizi wa
fitina. Hakutakuwepo na kudaiana kusikokwisha.
Vilevile,
itatusaidia kujua uweli wa walimu waliopo na wako wapi. Kuna minong’ono
ya kuwepo walimu hewa ambao pesa zao hutolewa kila mwezi. Pia, wapo
walimu waliotangulia mbele ya haki ambao bado wamo kwenye orodha ya
utumishi na mishahara yao huendelea kutumwa na hairejeshwi.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kuitumia nafasi hii kuwahakikishia walimu na wananchi wote wa
Tanzania, kuwa Serikali inawathamini na kuwajali walimu. Serikali ya
Awamu ya Nne inaweka kipaumbele cha juu sana kwa maendeleo ya elimu,
ndiyo maana bajeti ya elimu ndiyo bajeti kubwa kuliko zote. Inachukua
asilimia 19.8 ya bajeti yote ya Serikali. Watanzania wote ni mashahidi
wa nguvu kubwa tuliyoielekeza katika elimu ya sekondari, elimu ya juu na
elimu ya ufundi. Mimi na viongozi wenzangu kuendeleza elimu ni agenda
yetu kuu.
Katika
juhudi hizo tunatambua nafasi na umuhimu wa Mwalimu. Hatuwezi kua watu
tunaohimiza upanuzi wa elimu lakini tunampuuza mwalimu. La hasha! Mara
nilipoingia madarakani, katika mkakati wa kuboresha maslahi ya watumishi,
kundi tuliloanza nalo ni walimu na tumeendelea kulipa kipaumbele kila
tuliposhughulikia makundi mengine.
Katika
mkakati wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma tulitambua kuwa
hatutaweza kufanya hivyo kwa watumishi wote kwa wakati mmoja. Tukaona
tukienda kwa makundi tunaweza. Kundi la kwanza tuliloanza nalo ni walimu.
Natambua haja ya kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini,
ni nia yetu kufanya hivyo. Tumekuwa tunafanya hivyo katika miaka mitatu
hii na tutaendelea kufanya hivyo miaka ijayo.
Pamoja
na hayo, mwezi April, 2008, tumewalipa Walimu Shs. 7.2 bilioni, sehemu
kubwa ikiwa ni madeni ya nyuma kabla sisi hatujaingia madarakani.
Huu ni ushaidi kwamba tunawajali walimu.
Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kupuuza maslahi ya walimu.
Uchumi wa Dunia:
Ndugu
Wananchi;
Katika hotuba yangu ya Tanga wakati wa sherehe za kuzima Mwenge na
maadhimisho ya miaka 9 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius
Nyerere, nilizungumzia hali ya uchumi wa dunia na hasa wa mfumo wa fedha
unaozikabili nchi zilizoendelea. Nilielezea hofu yangu kuhusu athari
ambazo zinaweza kutokea kwa nchi yetu ikiwa uchumi wa dunia utaendelea
kuyumba kufuatia misukosuko ya kifedha ya kimataifa. Nilisema kuwa
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani huenda nayo ikakumbwa na
madhara yatokanayo na kuyumba huku kwa uchumi wa dunia.
Nilieleza kuwa nchi yetu inaweza kuathirika kwa njia zifuatazo:
Kupungua
kwa mauzo yetu ya nje kwenye masoko ya nchi za Magharibi kwa sababu ya
kupungua kwa uwezo wa watu na nchi hizo kununua bidhaa na huduma. Mazao
yetu ya biashara tunayouza nje yanaweza kuathirika kwa ajili hiyo;
Kuna uwezekano wa kupungua kwa mapato
yanayotokana na utalii, kutokana na kupungua kwa watalii kutoka mataifa
hayo kwa sababu watu wa nchi hizo kuathiriwa na mgogoro wa kifedha
unaozikumba nchi zao. Wapo watu wengi ustawi wao wa kifedha na kiuchumi
umeshuka kwa sababu ya kuanguka kwa masoko ya hisa na mabenki na
kufilisika kwa makampuni.
Kuna
wasiwasi kwamba uwezo wa nchi za Magharibi kutoa misaada kwa nchi yetu
utapungua, kutokana na fedha nyingi kutumika katika kuokoa vyombo vya
fedha katika nchi zao. Nilitoa mfano kuwa, katika wiki chache zilizopita,
nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji, Iceland na
Sweden, zimetangaza kutoa jumla ya dola za kimarekani trilioni 1.8
kusaidia kuyaokoa baadhi ya mabenki yaliyopata msukosuko.
Msukosuko huu unaweza kusababisha kupungua kwa mikopo ya kibiashara au
kuongezeka kwa gharama za mikopo kutoka nje, na hivyo kupungua kwa uwezo
wa mabenki yetu kukopesha.
Vilevile
kuna wasiwasi wa uwezekano wa kupungua kwa uwekezaji kutoka nje. Huenda
uwekezaji hapa nchini kutoka Afrika ya Kusini na Kenya ukapungua kwa
kuzingatia kuwa nchi hizo zina mahusiano zaidi na mtandao wa masoko ya
fedha ya kimataifa.
Pamoja
na hofu ya kupungua kwa uwekezaji kutoka nje, kuna uwezekano mkubwa wa
kupungua kwa kiwango na kasi ya uwekezaji wa ndani kutokana na kupungua
kwa uwezo wa taasisi zetu za fedha kukopesha. Wakati mwingine ni hofu ya
hayo yanayotokea duniani.
Na
mwisho msukosuko huu unaweza kusababisha kupungua kwa fedha zinazotumwa
na Watanzania walioko nje ya nchi yetu.
Ndugu
Wananchi;
Tangu nilipozungumzia suala hili kule Tanga, bado hakujawa na unafuu
wowote katika uchumi wa dunia licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na
mataifa makubwa kurekebisha hali hiyo. Uchumi wa nchi tajiri duniani
umeendelea kuyumba kwa maana ya kupungua na kudorora.
Hali
hiyo imeanza kuleta athari katika biashara ya kimataifa. Mahitaji ya
mafuta yameanza kupungua na kusababisha kushuka kwa bei ya mafuta katika
soko la dunia. Hali inaweza kuwa hivyo hivyo hata kwa bidhaa zetu
tunazouza nchi za nje.
Kadhalika, tunaendelea kuyasihi mataifa makubwa kiuchumi na nchi tajiri
kwa jumla zinazokabilia na matatizo haya yaendelee kuchukua hatua
madhubuti na za haraka kurekebisha hali iliyojitokeza katika mfumo wa
kifedha wa kimataifa.
Aidha,
tunasisitiza umuhimu wa kuutazama upya mfumo wa kifedha wa kimataifa
unavyofanya kazi kwa nia ya kurekebisha kasoro zilizopo. Naamini kufanya
hayo kutatuhakikishia kwamba msukosuko unaoikumba dunia hivi sasa
utapatiwa ufumbuzi na kwamba utaepukika na hautatokea tena siku za usoni.
Madhara yake ni makubwa kwa uchumi wa nchi zetu changa na maisha ya watu
wetu.
Kwa
mantiki hiyo napenda kutumia fursa hii kuungana na viongozi wengine
duniani katika kukaribisha wazo la Rais George Bush wa Marekani la
kuitisha mkutano maalum wa kimataifa wa kuzungumzia tatizo la kifedha la
kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba, mkutano huo utatoa ufumbuzi wa
kudumu wa tatizo hili. Bahati mbaya Afrika imesahaulika katika mkutano
huo. Hii ni dunia yetu sote yanayotokea popote yanatuhusu sote.
Mauaji ya Maalbino:
Ndugu
zangu, Watanzania wenzangu;
Tarehe 19 Oktoba, 2008 nilipewa heshima ya kupokea maandamano ya kulaani
na kupinga mauaji ya wenzetu wa jamii ya Maalbino. Katika maandamano
hayo nilielezea kusikitishwa kwangu na matendo hayo ya kikatili na ya
aibu kwa nchi yetu. Siku ile nilitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki
na kushirikiana katika mapambano haya halali ili kwa umoja wetu tuweze
kukomesha mauaji ya ndugu zetu hao.
Leo
nataka kuwaelezea azma ya kuwataka Watanzania kote nchini kutoa taarifa
kuhusu watu wanaojihusisha na mauaji ya Albino nchini. Kwa maana ya
waganga, wauaji, wauzaji na wanunuzi wa viungo vya Albino.
Nawataka
Watanzania wawataje kwa siri watu hao ili Serikali ifuatilie kwa karibu
nyendo zao, kuwabana ipasavyo na kuwachukulia hatua mwafaka. Utaratibu
huu ulitusaidia sana katika mapambano dhidi ya majambazi, naamini
utatusaidia hata katika mapambano haya halali na ya haki. Baada ya muda
si mrefu tutatoa maelekezo juu ya utaratibu wa kutoa na kukusanya
taarifa hizo.
Nataka
kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali yenu haitakaa kimya wakati raia
wasiokuwa na hatia wanaendelea kuteswa na kuuawa. Albino ni mwanadamu
kama alivyo mwanadamu mwingine yeyote. Ana haki ya kuishi na kupata
hifadhi ya maisha na mali zake kutoka katika jamii. Kuwaua kwa sababu
yoyote ile si haki na ni kosa kubwa.
Isitoshe
kwa sababu wanazouliwa ni aibu kwa mhusika na fedheha kubwa kwa jina
zuri la nchi yetu. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuelimisha jamii juu
ya madhara ya fikra potofu zinazoenezwa na waganga wa kienyeji wenye
tamaa na uchu wa kujipatia utajiri. Utajiri utapatikana kwa kufanya kazi
kwa bidii na maarifa na kuwa na nidhamu katika utendaji na matumizi ya
mapato yako. Sote tunawajibika kuwafichua watu hawa ambao ni hatari
katika jamii yetu. Naomba ushirikiano wa kila mmoja wetu ili tuikomeshe
na kuondoa aibu hii.
Fedha za EPA:
Ndugu
wananchi;
Jambo la mwisho ninalotaka kuzungumzia leo linahusu urejeshwaji wa fedha
za akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu inayojulikana kwa kifupi
kama EPA. Wengi wenu mtakumbuka kuwa, nilipozungumza na Bunge tarehe 21
Agosti, mwaka huu, nilieleza kwa kirefu yaliyotokea, hatua tulizochukuwa
na mahali tulipokuwa tumefikia katika kulishughulikia suala hili.
Nisingependa kuwachosha kwa kurudia tena yale niliyoyasema.
Siku ile
nilieleza katika hotuba yangu kwamba niliwataka wale wote waliokuwa
miongoni mwa yale makampuni 13 yaliyolipwa shilingi 90,359,078,804,
waliochukua fedha ambao walikuwa bado hawajarejesha fedha hizo kufanya
hivyo ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2008. Aidha, niliagiza uchunguzi kwa
zile kampuni 9 zilizolipwa shilingi 42,656,107,417 uendelee. Kamati
iliomba idhini ya kuwasiliana na vyombo husika vya dola vya mataifa
husika ya nje ili kupata ukweli na kukamilisha uchunguzi wao.
Ndugu
wananchi;
Nilielezea pia kwamba baada ya tarehe 31 Oktoba, 2008, kwa wale ambao
watakuwa hawakuteleza, hatua za kisheria zichukuliwe. Leo ndiyo siku ya
mwisho. Napenda kuwajulisha kuwa, taarifa nilizoletewa majira ya mchana
leo, ni kuwa kiasi cha shilingi 69,326,437,650 kati ya shilingi
90,359,078,804 zilikuwa zimerejeshwa. Hii ni sawa na asilimia 76.7
(76.7%).
Kesho
tarehe 01 Novemba, 2008 taarifa kamili itatolewa juu ya kiasi halisi
ambacho kitakuwa kimerejeshwa.
Pamoja
na kufanya hivyo, nimekwishatoa maelekezo kamili kwa wale ambao
hawakutimiza malipo, Kamati ikabidhi majalada yao kwa Mkurugenzi wa
Mashtaka mara moja, kwa hatua zipasazo za kisheria.
Mkurugenzi wa Mashtaka ni idara huru ya Serikali iliyoundwa kwa mujibu
wa Katiba ya Nchi. Yeye ndiyo mwenye mamlaka ya kuendesha mashtaka
mahakamani baada ya kupokea taarifa za upelelezi kutoka kwa Jeshi la
Polisi na Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Ndugu
Watanzania wenzangu;
Kuhusu uchunguzi uliokuwa unaendelea kufanywa kuhusu yale makampuni 9,
nasubiri taarifa yao mpya kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo. Taarifa
niliyopewa wiki mbili zilizopita zinaonyesha kuwa polisi wetu bado
hawajapata majibu kutoka kwa wenzao katika nchi walizoomba msaada. Hivyo,
nakusudia kuwataka waendelee kufuatilia kwa wenzao ili hatua zipasazo
ziweze kuchukuliwa.
Ndugu
wananchi;
Kwa mara nyingine tena napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Kamati ya
Mwanasheria Mkuu kwa kazi nzuri iliyofanya ambayo mbali na kubaini namna
ya tuhuma za uhalifu zilivyofanywa, pia ilibaini wahusika na kuwabana
kiasi cha kufanikiwa kurejeshwa kwa fedha ambazo vinginevyo zingepotea
kabisa.
Lakini kubwa zaidi, nawashukuru
wananchi kwa uvumilivu na uelewa wao wakati wote serikali ilipokuwa
inalishughulikia sakata hili la aina yake katika historia ya nchi yetu.
Tumefarijika sana kwa uelewa na ushirikiano wenu. Nawaomba tuzidi
kushirikiana katika mambo yote yanayohusu mustakabhali wa nchi yetu.
Aidha,
utaratibu wa kuzigawa fedha hizo kwa ajili ya shughuli za kilimo na
miundombinu zimekamilika.
Madai ya Wastaafu Jumuiya ya
Afrika Mashariki:
Katika
hotuba yangu ya leo, sikuweza kugusia suala la madai ya wastaafu wa
iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu Serikali inaandaa tamko
rasmi litakalowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi,
Mheshimiwa Mustafa Mkullo wiki ijayo. Hivyo nawaomba sote tuvute subira.
Hitimisho:
Kabla ya
kumaliza napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa
kuendelea kuiunga mkono serikali katika mambo yote ya msingi yanayoihusu
nchi yetu. Licha ya mawimbi ya hapa na pale ambayo tunapambana nayo
katika safari yetu, tumeendelea kuimarisha umoja na mshikamano wetu
ambao ndio nguzo na mhimili wa taifa letu.
Nawaomba
tuendelee kufanya hivyo kwa kutambua kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya
kujenga nguvu ya pamoja ya kuendeleza taifa letu. Nawasihi tujiepushe na
mambo yanayoweza kutugawa na kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu
na badala yake tuimarishe maelewano, mshikamano na umoja wa kitaifa.
Mungu
Ibariki Afrika;
Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
Dar es Salaam,
31 Oktoba, 2008.
|