Kikwete atembelea Sudan
07/09/2008

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewasili
katika mji mkuu wa Sudan wa Khartoum mchana wa leo (Jumapili, Septemba
7, 2008) kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, Rais Kikwete na ujumbe
wake wamelakiwa na mwenyeji wake, Rais Omar Bashir na mkewe, Widad
Babiker.
Rais ambaye ameambatana na mkewe, Mama Salma Kikwete amewasili Khartoum
akitokea moja kwa moja Swaziland ambako alihudhuria sherehe za miaka 40
ya uhuru wa nchi hiyo na sherehe za miaka 40 pia ya kuzaliwa kwa Mfalme
Mswati wa Tatu.
Viongozi hao wawili baadaye leo watakula futari na baada ya hapo
wataingia moja kwa moja katika mazungumzo yatakayofanyika kwenye Ofisi
ya Rais Bashir kwenye jengo la Friendship Hall.
Kesho Rais Kikwete amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na
Mwenyekiti wa Bunge la Sudan, Ahmed Ibrahim Eltahir na Makamu wa Rais,
Ustaz. Ali Osman Mohammed Taha.
Kabla ya kuondoka nchini Sudan kurejea nyumbani, Rais Kikwete atakutana
kwa mazungumzo mengine na Rais Bashir kabla ya viongozi hao wawili
kuzungumza na waandishi wa habari.
Inatarajiwa kuwa viongozi hao wawili watazungumzia masuala yanayohusu
uhusiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na Sudan, na kuhusu masuala ya
Afrika na kimataifa.
Mwaka huu, Tanzania na Sudan zilishirikiana katika kuchangia jeshi la
AU, ambalo lilikwenda Comoro kumng’oa kiongozi mwasi, Kanali Mohammed
Bakari kutoka Kisiwa cha Anjoun.
Kuhusu masuala ya Afrika , inatarajiwa kuwa Rais Bashir atamweleza mgeni
wake na mwenyekiti wa AU kuhusu hali ilivyo katika eneo Darfur na
jitihada zinazofanywa kupunguza mateso ya wananchi wa eneo hilo la
Sudan.
Katika hilo, viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia mipango ya kuundwa
kwa jeshi la pamoja la AU na kimataifa kwenda kulinda amani katika eneo
hilo la Darfur.
Pia viongozi hao watajadili amri iliyotolewa mwaka huu ya kukamatwa kwa
kiongozi huyo wa Sudan na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya
Uharifu (ICC) kutokana na mchango wa Serikali yake katika Darfur.
Pia Rais Kikwete anatarjiwa kupata maelezo ya undani kutoka kwa mwenyeji
wake kuhusu maendeleo ya jitihada za kuleta amani ya kudumu katika eneo
la Kusini mwa Sudan.
|