![]() |
Your community website |
![]() |
||||||
|
|
|
|||||||
|
|
||||||||
|
|
||||||||
|
|
||||||||
|
NEWS |
||||||||
|
|
|
|||||||
Hotuba ya Mhe. Kikwete juu ya Utumishi wa Umma28/01/2008
Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye uzinduzi wa awamu ya pili ya programu ya kuboresha utumishi wa umma, Dar es Salaam, ya tarehe 28 Januari 2008.
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma;
Waheshimiwa Mawaziri;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Waheshimiwa Wabunge;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Viongozi wenzangu wa Siasa;
Wageni Waalikwa na
Ndugu Wananchi:
Awali ya yote napenda kukushukuru wewe, Mheshimiwa Waziri kwa
kunialika na kunipa heshima hii kubwa ya kuzindua Awamu ya Pili ya
Programu ya Kuboresha Utumishi wa Umma. Nafurahi kujumuika nanyi leo
katika tukio hili muhimu linalotupeleka katika hatua ya juu zaidi
katika jitihada zetu za kuboresha utumishi wa umma nchini.
Tangu miaka ya tisini (1990s) Serikali imekuwa ikifanya maboresho ya sekta ya utumishi wa umma. Maboresho hayo yamekuwa yakilenga katika kuubadili utumishi wa umma ili uwe mhimili imara wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika nchi yetu, badala ya kuwa kero na kizuizi cha jitihada za Serikali za kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Waziri;
Kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako, mipango yote ya kuboresha
utumishi wa umma iliyokwishatekelezwa imezaa matunda
yanayoonekana. Programu ya Kuboresha Utumishi Serikalini (Civil
Service Reform Programme) imefanikisha lengo lake kuu la kuwa na
Serikali ndogo, yenye ufanisi wa hali ya juu na inayolenga kutoa
huduma bora kwa wananchi. Serikali imefanikiwa kwa kiwango
kikubwa kuainisha upya majukumu yake. Tofauti na ilivyokuwa huko
nyuma, hivi sasa Serikali imebakia na majukumu yake ya msingi
yanayohusu utawala, ulinzi na usalama na usimamizi wa uchumi wa
nchi. Maboresho hayo pia yamesaidia sana katika kupunguza
gharama za uendeshaji wa Serikali. Ajira holela na ajira hewa
Serikalini zimedhibitiwa.
Hali kadhalika, maslahi ya watumishi wa umma yamekuwa
yanaboreshwa kwa kutambua ujuzi na uzoefu wa watumishi pamoja na
kuzingatia uwezo wa Serikali kiuchumi. Muundo wa Serikali
umeboreshwa na madaraka zaidi yamepelekwa kwenye ngazi za chini
waliko wananchi wengi. Hatua hizi zimesaidia katika kuimarisha
na kuboresha utendaji wa Serikali pamoja na utoaji wa huduma
muhimu kama vile maji, afya, elimu na nyinginezo.
Mheshimiwa Waziri;
Katika hotuba yako pia
umeelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji
wa Awamu ya Kwanza ya Programu ya Kuboresha Utendaji Kazi
Katika Utumishi wa Umma (Public Service Reform Programme).
Programu hiyo ilizinduliwa rasmi mwezi Juni, 2000 na
kumalizika Desemba, 2007.
Mafanikio yaliyopatikana ni
makubwa na ya kujivunia. Napenda kuitumia nafasi hii
kukupongeza wewe Mheshimiwa Waziri na watumishi wote wa
Ofisi yako kwa kazi nzuri mliyoifanya na mnayoendelea
kuifanya.
Mafanikio
yaliyokwishapatikana yametokana na juhudi zenu hivyo
niruhusuni niseme hongereni sana na ahsanteni sana.
Ni jambo la kuleta faraja
kuona mifumo ya kuboresha utendaji kazi katika taasisi za
umma imewekwa na upangaji wa mipango na bajeti za Wizara,
Idara na Wakala za Serikali nao umeboreshwa. Maslahi na
mazingira ya kazi ya Watumishi wa Umma yameboreshwa na
matumizi ya teknolojia ya kompyuta katika shughuli za
Serikali yameongezeka. Mfumo wa wakala wa Serikali
umeanzishwa kwa shughuli kadhaa za serikali na sekta binafsi
imekuwa inahusishwa kwa baadhi ya shughuli. Mambo haya
yameipunguzia serikali mzigo na kuongeza ufanisi.
Suala la maadili ya
utumishi wa umma limepewa uzito stahili. Kanuni za maadili
ya utumishi wa umma zimeandaliwa na mafunzo yamekuwa
yanatolewa.
Mheshimiwa Waziri, Wageni
waalikwa; Lakini, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna kazi
kubwa ya kufanya mbele yetu. Licha ya jitihada zetu za
kuboresha huduma tunayoitoa kwa umma bado kuna mapungufu
ambayo hatuna budi kuendelea kuyatafutia ufumbuzi. Kwa mfano,
bado kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu huduma
zisizoridhisha kwa baadhi ya Idara za Serikali.
Pia yapo malalamiko
yahusuyo ubabaishaji na vitendo vya rushwa. Mengi ya
malalamiko hayo yanaelekezwa kwenye sekta za elimu, afya,
usalama wa raia, utoaji haki, mambo ya ndani na ardhi. Vile
vile bado kuna tatizo la tija duni katika utumishi wa umma.
Baadhi ya sababu zinazosababisha kuendelea kwa hali hii ni
kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa uwajibikaji katika ngazi zote
za taasisi za Serikali, uchache wa watumishi wenye sifa na
uzoefu wa kutosha na uongozi usiokuwa mbunifu.
Mheshimiwa Waziri na
Wageni Waalikwa;
Nimefurahi kusikia
kwamba matatizo haya na mengineyo ambayo sikuyataja
yamezingatiwa katika uandaaji wa Mpango wa Utekelezaji
wa Awamu ya Pili ya Programu hii.
Nimetiwa moyo, kusikia
kwamba kwa kiwango kikubwa uendeshaji wa programu hii
utaamuliwa, kuendeshwa na kusimamiwa na taasisi za umma
zenyewe na kwamba maboresho yatakayoidhinishwa
yataingizwa kwenye mipango na bajeti za taasisi hizo kwa
ajili ya utekelezaji. Matarajio yangu ni kuwa kila
taasisi ya umma itachambua kwa makini maboresho
yanayoihusu na kuyaainisha kwenye mipango yake na
kuyatekeleza kwa ukamilifu ili kuboresha zaidi huduma
kwa umma.
Nimefurahi pia kusikia
kwamba tatizo la kutowajibika litashughulikiwa katika
awamu hii ya maboresho. Hii ni pamoja na kuandaa
utaratibu wa uwajibikaji wa taasisi zote za umma katika
ngazi zote. Ombi langu kwenu ni kuwa tuharakishe
uandaaji wa utaratibu huo ili ukamilike mapema.
Tusichukue muda mrefu sana kwa kazi ya uandaaji. Naamini
kuwa utaratibu huu tukiutekeleza vizuri utasaidia sana
katika kuimarisha utendaji wa Serikali na kutoa huduma
kwa wananchi kwa jumla.
Ndugu Viongozi na
Wageni waalikwa;
Jambo lingine
ambalo napenda kulisisitiza hapa ni haki ya wananchi
kupata huduma nzuri kutoka kwa watumishi wa umma na
haki yao kudai huduma hiyo. Utumishi wa umma upo kwa
ajili ya kuwahudumia wananchi. Huduma itolewayo ni
haki yao, siyo fadhila. Hivyo kila mwananchi anayo
haki ya kudai kupatiwa huduma iliyo bora. Na
watumishi wa umma wanao wajibu wa kutoa huduma bora
kwa wananchi.
Ni kwa msingi huo
nimefarijika kusikia kwamba mpango huu unalenga
katika kuwawezesha wananchi na wateja kwa ujumla
kuwa na uelewa wa upatikanaji wa huduma za umma na
kufahamu haki zao za kupata huduma bora. Hili ni
jambo jema, naomba tuliimarishe. Nafurahi pia
kusikia kwamba katika awamu hii ya Programu
kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na kujenga
utumishi wa umma wenye nidhamu na unaozingatia
maadili.
Hili nalo ni jambo
muhimu sana. Hakuna mafanikio bila nidhamu kazini.
Na mtumishi wa umma asiyezingatia nidhamu na maadili
ya kazi yake hawezi kuwa na ufanisi. Naomba suala la
nidhamu na maadili tulipe uzito mkubwa zaidi ili
kujenga uadilifu wa hali ya juu katika utumishi wa
umma hapa nchini.
Mheshimiwa
Waziri, Wageni Waalikwa;
Kuhusu
kuboresha maslahi ya watumishi wa umma napenda
kusisitiza mambo mawili. Kwanza, kwamba
tumemekuwa tunayaboresha kwa nyakati mbalimbali
lakini lazima tuendelee kuboresha. Pili, kwamba
msingi wake ni tija yaani tija ya mtumishi mmoja
mmoja na tija ya wengi katika taasisi na nchi
nzima kwa jumla. Sote tunatambua kuwa maslahi
bora yanategemea sana kukua kwa uchumi wa nchi
yetu. Pia yanategemea ufanisi katika ukusanyaji
wa mapato ya Serikali. Uchumi unaokua kwa kasi
na umakini katika ukusanyaji wa kodi ndivyo
pekee vitakavyoiwezesha Serikali kuwalipa
watumishi wake vizuri. Lazima tufanye hayo.
Hivyo, nawasihi
ndugu zangu wote tuliomo kwenye utumishi wa umma
tujitume zaidi, tufanye kazi kwa bidii na
maarifa zaidi ili kuimarisha uchumi wa nchi yetu.
Kila moja wetu atimize wajibu wake ipasavyo,
tena kwa wakati. Tusikwepe wajibu wetu na kwamba
tuache tabia ya kutoa visingizio visivyokwisha
kwa kutokutimiza malengo tuliyojiwekea. Naamini
sote tukiyafanya hayo nchi yetu itapiga hatua
kubwa na ya haraka. Hii itatuwezesha kuboresha
zaidi maslahi ya watumishi wa umma nchini mwetu.
Mheshimiwa
Waziri, Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa;
Nafurahi kuona
kwamba Mpango huu mpya umelipa umuhimu stahili
suala la kuimarisha uongozi katika utumishi wa
umma. Nchi yetu inahitaji viongozi makini,
wabunifu, wanaoona mbali na wachapa kazi hodari.
Viongozi walio
makini katika kusimamia utekelezaji wa mipango
na maamuzi mbalimbali ya Serikali yahusuyo
maeneo yao ya uongozi. Kwa sababu hiyo
nimependezwa na uamuzi wa kuanzisha mfumo wa
kutambua na kuandaa viongozi kupitia utaratibu
wa mafunzo ya mara kwa mara. Bila ya shaka
utaratibu huu utasaidia sana katika kujenga kada
ya viongozi na watendaji bora wanaohitajika sana
katika utumishi wa umma. Nawaomba muangalie
uwezekano wa kuanzisha Chuo cha Taifa cha
Uongozi kitakachotoa mafunzo kwa viongozi na
watendaji kama njia mojawapo ya kuimarisha
uongozi na utendaji Serikalini.
Mheshimiwa
Waziri;
Ili Mpango
wa kuboresha utumishi wa umma uweze
kufanikiwa kuna mambo kadhaa ambayo hayana
budi yafanyike. Kwanza, Ofisi yako lazima
iendelee na kazi ya kuwaelimisha watumishi
wa umma kuhusu umuhimu wa kubadilika kifikra
na kimtazamo. Hii inatokana na ukweli kwamba
sehemu kubwa ya maboresho ya utumishi wa
umma yanalenga katika kubadilisha taratibu,
tabia na utamaduni wa kazi uliozoeleka kwa
muda mrefu. Hivyo kubadilika kifikra na
kimtizamo ni jambo la lazima. Lazima sisi
tulio katika utumishi wa umma tubadilike.
Tuache
umangimeza na kujiona kuwa sisi ni mabwana
mkubwa na wananchi si lolote. Tutambue kuwa
tupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na
siyo vingenevyo. Hivyo kazi ya kuwaelimisha
watumishi ili kutambua wajibu wao huo iwe ni
ya kudumu.
Nawaomba
msichoke kuifanya. Pili, hakikisheni kuwa
raslimali watu kwa maana ya watumishi wa
umma, inaendelezwa. Shirikianeni na taasisi
nyingine za umma katika kubuni na kutekeleza
mipango ya mafunzo kwa kada mbalimbali za
watumishi wa Serikali. Mazingira ya kazi
duniani yanabadilika kila siku. Kila kukicha
kuna mambo mapya. Hivyo watumishi wa umma
nao wanastahili kujengewa uwezo
utakaowawezesha kwenda na wakati.
Tunahitaji kuwa na watumishi wa umma
wenye uwezo na ujuzi wa kutosha.
Watumishi ambao wanajua wanalolifanya na
siyo kubahatisha. Tujipange vizuri
kuwawezesha watumishi wa Serikali kupata
mafunzo stahiki yatakayowawezesha
kufanya kazi zao kwa kujiamini na
ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Waziri, Wageni waalikwa;
Tatu,
hapana budi kuongeza kasi ya kuanzisha
na kutumia teknolojia za kisasa za
habari na mawasiliano katika shughuli za
Serikali. Katika dunia ya leo mambo
mengi yanaendeshwa kwa kutumia mtandao
wa kompyuta. Serikali nyingi duniani
zinaendesha mambo yake mengi kupitia
mtandao wa aina hiyo (serikali mtandao).
Nasi hatuna budi kufanya hivyo kwani
itasaidia sana katika kuboresha na
kurahisisha mawasiliano ndani ya
Serikali na baina ya Serikali na
wananchi. Pia itapunguza urasimu
ambao bado ni moja ya vikwazo vya
ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu ya serikali. Vilevile,
itasaidia katika vita dhidi ya
rushwa kwa sababu vitu vingi
vitakuwa wazi na havihitaji
mazungumzo ya ana kwa ana baina ya
mtoa huduma na mpokea huduma.
Mheshimiwa Waziri na Wageni
Waalikwa;
Programu hii tunayoizindua leo
itakuwa ya manufaa kwa wananchi
ikiwa tu mabadiliko
tunayoyakusudia yataongeza ubora
katika utoaji wa huduma kwa umma.
Hivyo lengo letu kubwa liwe ni
kuimarisha ubora wa hudumu
tunazozitoa kwa Watanzania. Kama
nilivyosisitiza katika hotuba
yangu ya kuhitimisha sherehe za
siku ya utumishi wa umma za
mwaka jana, watumishi wa umma
lazima tudhamirie kuhakikisha
kuwa huduma za leo ni bora
kuliko za jana na zile za kesho
ziwe bora zaidi kuliko za leo.
Naamini tukifanya hivyo tutaweza
kabisa kufikia lengo letu la
kujenga utumishi wa umma mahiri,
utumishi wa umma ulio adilifu na
sikivu na utumishi wa umma
unaoweka mbele maslahi ya umma.
Nawasihi wote tuitumie programu
hii ya maboresho kama nyenzo ya
kutufikisha kwenye lengo letu
hilo.
Hitimisho
Mheshimiwa Waziri; Viongozi
na Ndugu Wananchi Wenzangu;
Nitakuwa mwizi wa fadhila
kama nitamaliza hotuba yangu
bila ya kuwashukuru wale
wote waliojitolea kuchangia
kwa hali na mali katika
utekelezaji wa Programu hii.
Wenzetu hao ni pamoja na
Benki ya Dunia (WB), Benki
ya Maendeleo ya Afrika na
Serikali za Uingereza,
Canada, Denmark, Ireland na
Japan. Aidha nawashukuru
wengineo wote waliofanikisha
Programu hii kwa namna moja
au nyingine. Kwao wote
nasema asanteni sana.
Tunathamini sana mchango wao.
Tunawaomba wandelee kutuunga
mkono.
Baada ya kusema hayo, sasa
ninayo heshima ya kutamka
kwamba Awamu ya Pili ya
Programu ya Kuboresha
Utumishi wa Umma
imezinduliwa rasmi.
Vile vile natamka kwamba
Jengo la Mtandao na Tovuti
Mpya ya Utumishi
vimezinduliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza!!
|
||||||||
|
Custom Search
|
||||||||
|
|
|
|||||||
|
©
www.zenjydar.co.uk - Since 2007 |
|
||||||||