Salamu za mwaka mpya
kutoka kwa Rais wa Tanzania
02/01/2009

Ndugu Wananchi:
Hatimaye imewadia ile siku ya kuuaga mwaka mmoja na
kuukaribisha mwingine. Leo tunauaga mwaka 2008 na kuukaribisha mwaka
2009.
Kwanza kabisa, naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu
aliyetujaalia uhai na kutuwezesha kuiona siku hii adhimu salama. Ni
wajibu wetu kumshukuru Muumba wetu kwani wapo wenzetu wengi
hawakujaaliwa kuiona siku ya leo kwa vile wametangulia mbele ya haki.
Wakati tukikumbushana wajibu wetu wa kumuomba Mwenyezi Mungu awape
marehemu wetu hao mapumziko mema, tumuombe pia awape nafuu na kuwaponya
wenzetu wote wanaougua maradhi mbalimbali ili wajumuike nasi katika
shughuli za ujenzi wa taifa letu.
Ndugu Wananchi;
Mwaka wa 2008 tunaoumaliza leo ulikuwa mwaka wa aina yake kwa taifa letu
na katika historia ya uongozi wangu. Ulikuwa ni mwaka ambao tumepata
mafanikio mengi mazuri na mengine ya kihistoria katika nyanja mbalimbali
za maisha ya wananchi wa Tanzania na taifa letu. Lakini, pia kulikuwepo
na changamoto au matukio machache ambayo yalisababisha baadhi ya watu
ndani na nje ya nchi yetu wapate shaka juu ya hatima ya umoja, amani na
utulivu wa nchi yetu. Umoja, amani na utulivu ndiyo nguzo kuu na sifa
kubwa inayoitofautisha na kutambulisha Tanzania miongoni mwa mataifa
barani Afrika.
Ndugu Wananchi;
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tumeumaliza mwaka huu kwa usalama,
amani na utulivu. Tuzidi kumuomba baraka na rehema zake, katika mwaka
2009, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, utulivu na watu wake waishi
kwa upendo, umoja, masikilizano, mshikamano na ushirikiano kama ndugu wa
taifa moja.
Pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu, hatuna budi kutambua kuwa
dhamana ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa tulivu na yenye
amani na upendo miongoni mwa watu wake ni yetu wenyewe. Ni ukweli ulio
wazi kuwa katika mwaka huu tunaoumaliza sasa baadhi yetu tumekuwa
tunafanya vitendo au kutoa kauli ambazo zilikuwa zinalielekeza taifa
kubaya. Tena tulikuwa tunafanya hivyo kwa ajili ya kuendeleza manufaa
binafsi ya kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa tutajiepusha na mambo hayo
katika mwaka 2009. Nawasihi viongozi wenzangu wa kisiasa na wa kijamii
tubadilike, tuweke mbele maslahi ya taifa ili tuiepushe nchi yetu na
mabalaa ambayo baadhi ya wenzetu yaliwakuta.
Hali ya Uchumi wa Nchi na Dunia
Ndugu Wananchi;
Kwa jumla hali ya uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2008 ilikuwa ya kiwango
cha kuridhisha. Lakini, hali ingekuwa bora zaidi kama uchumi wa dunia
usingepata misukosuko iliyoupitia sasa. Kwa sababu ya matatizo makubwa
yanayoukabili uchumi wa dunia, baadhi ya malengo tuliyojiwekea kuhusu
ukuaji na mwenendo wa uchumi wetu yameathiriwa
Mfumuko wa Bei
Ndugu Wananchi;
Bei kubwa za mafuta zilizokuwepo kwa karibu miaka miwili mfululizo na
hasa katika miezi kumi ya mwanzo ya mwaka huu zilipokuwa juu sana,
imekuwa kichocheo kikubwa cha kupanda sana kwa mfumuko wa bei na ukali
wa maisha hapa nchini. Aidha, kupanda sana kwa bei za vyakula
tunavyoagiza kutoka nje kama vile ngano, mchele na vinginevyo viliifanya
hali ya mfumuko wa bei kuwa mbaya zaidi
Tulikuwa tumejiwekea lengo, kwa mfano, katika bajeti
iliyopita kuwa tutateremsha mfumuko wa bei hadi kuwa asilimia 4.5 mwezi
Juni, 2008 kutoka asilimia 5.9 ya mwezi Juni, 2007. Badala yake mfumuko
wa bei ukawa asilimia 9.3 mwezi Juni, 2008 na kupanda hadi asilimia 12.3
ilipofika mwezi Novemba, 2008. Hivi sasa bei za mafuta zimeshuka kuanzia
Oktoba, 2008 na hivi leo zimefikia dola za Kimarekani 38.4. Hali
kadhalika, bei za baadhi ya vyakula nazo zimeshuka. Lakini, itachukua
muda mpaka manufaa ya hali hiyo kuonekana kwa uchumi wa nchi yetu na
wananchi wake.
Ndugu Wananchi;
Wakati mwingine hali huwa hivyo kwa sababu ya ukaidi na tamaa ya
wafanyabiashara. Nimekwishawaagiza Mawaziri wahusika kuzibana mamlaka
husika kutimiza ipasavyo wajibu wao kwa mujibu wa mamlaka waliyopewa
kisheria kuwalinda wananchi dhidi ya wafanyabiashara wa aina hiyo.
Wakati huo huo narudia kuwataka wafanyabiashara watoe ushirikiano
unaostahili kwa maslahi ya wateja wao na taifa kwa jumla. Aidha,
nazitaka mamlaka husika kutokuchelewa wala kuchelea kuchukua hatua
zipasazo kwa wafanyabiashara wakaidi.
Ndugu Wananchi;
Kutetereka kwa mfumo wa fedha wa kimataifa na kuanguka kwa masoko ya
hisa katika mataifa yaliyoendelea kumesababisha uchumi wa nchi hizo
kudhoofika. Hali hiyo imekuwa na athari za namna na viwango mbalimbali
kwa uchumi wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Nilikwishalieleza siku za nyuma na napenda kurudia kusema
kuwa sekta ya fedha hapa nchini bado ni tulivu. Haijaathiriwa na
misukusuko inayoikumba sekta ya fedha ya kimataifa. Zipo sababu kuu
mbili.
Kwanza, kwamba, sekta yetu ya fedha na soko la mitaji
havijaunganishwa na mfumo wa fedha wa kimataifa na masoko ya hisa ya
kimataifa. Hivyo basi, hakuna athari za moja kwa moja zinazotukuta hapa
nchini kwa sasa.
Pili, kuna usimamizi mzuri wa soko na sekta ya fedha
unaofanywa na Benki Kuu. Mpaka sasa, juhudi hizo za Benki Kuu zimesaidia.
Hata hivyo, tunatambua haja na hoja ya kuendelea kuwa makini. Inaelekea
matatizo ya mfumo wa fedha na uchumi katika nchi zilizoendelea
yatachukua muda mrefu kutengemaa. Hatujui siku za usoni mambo ya
yatakuwaje.
Serikali itaendelea kushirikiana na Benki Kuu kuzuia athari
za soko la fedha duniani zisitufikie au kama zitatufikia, basi makali
yake yawe nafuu. Kwa sasa mfumo wa ufuatiliaji (surveilance) na ule wa
kutoa tahadhari ya mapema (early warning system) vinafanya kazi ipasavyo.
Tuko tayari kuchukua hatua zaidi kama hapana budi.
Ndugu Wananchi;
Athari za hiyo Tsunami ya uchumi wa dunia, kama ilivyoitwa na baadhi ya
watu, kwa uchumi wetu tumeanza kuziona kwa baadhi ya sekta. Tuchukue kwa
mfano, sekta ya utalii. Katika mapumziko yangu ya mwisho wa mwaka huu
nilitembelea mbuga zetu za hifadhi ya wanyama za Tarangire, Ziwa Manyara,
Ngorongoro na Serengeti ya Kusini. Katika mazungumzo yangu na viongozi
wa hoteli, hifadhi hizo na wale wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
nimeelezwa jinsi idadi ya watalii ilivyopungua na mapato yao kushuka kwa
kati ya asilimia 7 na 18.
Aidha, nimezungumza na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya
kuchambua pamba na viongozi wa Bodi ya Pamba. Wote wamenieleza tabu
wanayoipata ya kuuza pamba yao nje. Pia wanaelezea jinsi bei ya pamba
ilivyoshuka katika soko la dunia. Katika kipindi cha mwezi Machi hadi
Julai, 2008 bei ya pamba ilikuwa senti 82 za dola za Kimarekani kwa
paundi na kushuka hadi senti 45 kwa paundi kwa sasa.
Hali kwa zao la kahawa nayo siyo nzuri. Nimeambiwa kuwa kati
ya mwezi Agosti, msimu wa kahawa ulipoanza, na tarehe 18 Disemba 2008,
bei ya kahawa ya Arabica kwenye soko la dunia, imeshuka kutoka dola za
Kimarekani 158 hadi 104 kwa gunia la kilo 50. Hii ni sawa na anguko la
asilimia 34. Katika kipindi hicho hicho, bei ya kahawa ya robusta
imeshuka kutoka wastani wa dola za Kimarekani 93.6 hadi dola 65.46 kwa
gunia la kilo 50. Hii ni sawa na anguko la asilimia 30.
Ndugu Wananchi;
Hata kwa mazao mengine nayo kwa jumla, hali ni hiyo hiyo ya kupungua kwa
mauzo nje na kushuka kwa bei. Matatizo tunayoyapata sisi kwa mazao yetu
ndiyo yaliyoikuta bidhaa ya mafuta. Kwa sababu ya uchumi kutetereka
katika nchi za Marekani, Ulaya Magharibi, Japan, China na India mahitaji
ya mafuta yamepungua na bei ya mafuta imeanguka kupita kiasi.
Ndugu Wananchi;
Kupungua kwa mauzo nje na bei ya bidhaa zetu pamoja na kupungua kwa
watalii kuna athari kwa uchumi wa nchi yetu. Mapato yetu ya fedha za
kigeni yatapungua jambo ambalo litapunguza akiba yetu ya fedha za kigeni,
hivyo kuathiri uwezo wetu wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Aidha,
mapato ya Serikali kwa kodi zitokanazo na mauzo hayo yatapungua, hivyo
kuathiri uwezo wa Serikali wa kutimiza majukumu yake ya kiutawala na
kiuchumi. Isitoshe ajira chache zilizopo katika sekta husika zitapungua
na kusababisha watu hao kuwa na hali mbaya kiuchumi.
Ndugu Wananchi;
Hali mbaya ya uchumi wa dunia inasababisha uwekezaji wa kutoka nje nao
kuathirika. Baadhi ya wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza nchini
wameahirisha nia yao. Ukiacha hofu inayotokana na hali mbaya ya uchumi
wa dunia, wengine wamekuwa wanapata ugumu wa kupata mikopo kutoka katika
mabenki. Mabenki yamekuwa yanasita kukopesha na pale yanapokopesha
masharti yake huwa magumu kiasi cha kuwakatisha tamaa wakopaji.
Ndugu Wananchi;
Nimezitaja baadhi tu ya athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia kwa uchumi
wa nchi yetu ili tutambue kuwa tupo kwenye mazingira magumu na hali ya
baadae ni ya mashaka. Tunaweza kunusurika kwenye eneo moja lakini
tukaathirika kwenye maeneo mengine kwa sababu uchumi wetu ni uchumi wa
dunia ya utandawazi. Kutokana na athari hizo inakadiriwa kuwa
hatutafikia malengo yetu ya kukua kwa uchumi mwaka huu 2008 na hata
mwaka ujao wa 2009. Inakadiriwa kuwa uchumi utakua kwa asilimia 7.7
badala ya 7.8 mwaka huu na mwakani utakua kwa asilimia 7.3 badala ya
asilimia 8 iliyokadiriwa.
Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda sote tutambue kuwa kuna kila dalili kuwa mwaka 2009 huenda
tutatumia muda mwingi na nguvu nyingi kukabili athari za machafuko ya
uchumi wa dunia. Kwa ajili hiyo, hatuna budi kutambua hivyo mapema na
kuwa tayari kusimama kidete kukabiliana na athari zake. Sisi katika
Serikali tunafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea duniani na hapa
nchini na kuamua hatua za kuchukua. Tutaendelea kupashana habari. Maombi
yangu kwenu wananchi wenzangu ni uelewa wenu na ushirikiano wenu. Umoja,
mshikamano na ushirikiano wetu wakati huu ndivyo vitakavyotukinga na
kutuvusha katika tatizo hili kubwa.
Ndugu Wananchi;
Yapo mambo kadhaa ambayo hatuna budi kufanya katika kukabiliana na hali
hii tete hapa nchini. Miongoni mwa hayo lipo suala la kujenga uwezo wa
ndani wa kujitegemea kwa mambo fulani fulani kama vile chakula na bidhaa
muhimu kwa matumizi ya watu. Pili, linalolingana na hilo, ni suala la
kukuza utalii wa ndani na kutafuta vyanzo vipya vya watalii kama vile
Mashariki ya Kati na Asia. Tatu, kukuza masoko ya ndani kwa bidhaa zetu
na masoko ya kanda kama vile SADC na EAC. Wakati mwigine tunahangaikia
masoko ya mbali wakati soko lipo hapa ndani au nchi jirani.
Ndugu Wananchi;
Kwangu mimi kauli mbiu muafaka kwa mwaka 2009 ni “Mwaka wa Kuhami na
Kukuza Uchumi wa Taifa”. Bahati nzuri kauli mbiu hii inawiana na mpango
wangu wa kazi nilipoingia madarakani. Nilikuwa nimepanga kuwa, katika
nusu ya kwanza ya kipindi changu cha uongozi tuelekeze nguvu zetu katika
upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii, na nusu ya pili
tushughulikie kukuza uchumi. Nafurahi kwamba, tumefanikiwa kuweka
misingi madhubuti ya kisera na mipango ya uhakika ya utekelezaji kuhusu
elimu, afya, barabara, maji na umeme vijijini. Utekelezaji wake
unaendelea na changamoto yetu kubwa ni upatikanaji wa fedha za kutosha
kutekeleza malengo tuliyojiwekea.
Nashukuru kwamba ufanisi mkubwa tulioupata katika ukusanyaji
wa mapato ya ndani na misaada ya washirika wetu wa maendeleo tumeweza
kupata mafanikio tuliyoyapata mpaka sasa. Hata hivyo mahitaji ya
rasilimali bado ni makubwa. Ni wajibu wetu kuendelea kutafuta.
Ndugu Wananchi;
Kuanzia mwaka 2009 Serikali itaelekeza nguvu katika kukuza uchumi wa
nchi kwa lengo la kuongeza mapato ya nchi na wananchi wake. Bahati mbaya
au nzuri yanayotokea sasa duniani yanasisitiza haja na hoja ya kufanya
hivyo. Pia, yameongeza jambo jipya la kufanya, nalo ni la kuhami uchumi
usitetereke.
Kilimo Kipaumbele cha Kwanza
Ndugu Wananchi;
Katika agenda yetu ya kukuza uchumi, kilimo kimepewa kipaumbele cha
kwanza. Tunafanya hivyo kwa sababu nzuri na za msingi kabisa. Kwanza,
tunataka kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa chakula na tunakuwa na
ziada ya kutosha. Katika mazingira ya sasa ambapo bei za vyakula duniani
ziko juu, kuwa na upungufu wa chakula na kulazimika kuagiza kutoka nje
kutazua matatizo makubwa nchini. Mfumuko wa bei utatushinda kuudhibiti.
Pili, kilimo kitatupatia malighafi ya viwanda vya kusindika
mazao ya kilimo na kuzalisha bidhaa kamili zinazotokana na mazao ya
kilimo. Kuendeleza viwanda vya aina hii ni kipaumbele chetu cha pili
katika agenda yetu ya kukuza uchumi wa taifa. Lazima tuanze safari ya
kuuza nje mazao ya kilimo yakiwa yameongezewa thamani kuliko kuyauza
yakiwa ghafi kama tufanyavyo sasa. Tutafanya kila liwezekanalo kuvutia
wawekezaji wa ndani na nje ili kufanikisha azma yetu hiyo.
Tatu, kilimo ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni
kwa nchi, mapato ya serikali kupitia kodi na ni tegemeo la watu wengi
nchini kwa uhai wao. Asilimia 8.5 ya fedha za kigeni hutokana na mazao
ya kilimo na asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo kilimo
ndiyo shughuli yao kuu ya kuwapatia mapato na maisha yao.
Hali ya Chakula
Ndugu Wananchi;
Hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni nzuri kwa miaka miwili
mfululizo sasa, yaani 2007 na 2008, na tumekuwa tunapata ziada ingawaje
ni kidogo. Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna tishio la njaa nchini.
Hata yale maeneo ambayo yamekuwa yanapata upungufu wa chakula tumeweza
kuyahudumia kwa kutumia ziada hiyo na akiba kutoka katika Hifadhi ya
Taifa ya Chakula (SGR).
Kwa mfano, tathmini iliyofanywa mwezi Septemba, 2008
inaonyesha kuwa watu 240,544 katika Wilaya 20 nchini watakabiliwa na
upungufu wa chakula kati ya Desemba, 2008 na Januari, 2009. Watu hao
watahitaji tani 7,182 za chakula ambacho tayari kimekwishatengwa kutoka
Hifadhi ya Taifa ya Chakula. Hifadhi hiyo sasa ina akiba ya tani
127,420.
Ndugu Wananchi;
Mvua za vuli hazikuwa nzuri kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga,
Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Lakini, zimekuwa nzuri kwa mikoa ya
Kagera, Mwanza na Mara. Hivyo basi mavuno ya vuli hayatakuwa mazuri
katika mikoa iliyoathirika. Hali hiyo inaweza kuongeza iadi ya watu
watakaohitaji msaada wa chakula. Hata hivyo, hakuna shaka yoyote
tutaweza kuwahudumia. Matumaini yetu na sala zetu kwa mikoa hiyo ni kuwa
mvua za masika zitakuwa nzuri. Ikiwa hivyo mzigo utapungua. Bahati nzuri
mikoa mingine inayopata mvua moja hali ya mvua ni nzuri, hivyo inatutoa
hofu ya upungufu mkubwa wa chakula nchini. Tuzidi kumuomba Mungu mvua
zinyeshe kama kawaida katika mikoa hiyo nayo.
Ndugu Wananchi;
Dhamira yetu katika kuelekeza nguvu zetu katika kuendeleza kilimo ni
kuongeza tija. Bahati mbaya kwa sasa tija iko chini sana jambo
linaloelezea hofu za upungufu wa chakula, mazao ya biashara na hali duni
ya maisha kwa wakulima wengi.
Kwa ajili hiyo Serikali imekusudia mwaka 2009 kutilia mkazo
mambo matano:
a. Upatikanaji na matumizi ya mbegu bora;
b. Upatikanaji na matumizi ya mbolea;
c. Upatikanaji wa maafisa ugani;
d. Uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji pale inapowezekana; na
e. Upatikanaji na uimarishaji wa masoko ya mazao ya wakulima.
Ndugu Wananchi;
Mambo yote hayo na mengine ambayo sikuyataja si mapya. Tumekuwa
tunayatekeleza katika miradi na programu mbalimbali za kuendeleza kilimo
nchini kama vile DADP’s, PADEP na ASDP. Tunachokusudia kufanya mwaka
ujao ni kutoa msukumo maalum wa kuendeleza kilimo kama tulivyofanya
kwenye elimu na tunavyokusudia kufanya kwa upande wa afya.
Kuhusu upatikanaji wa mbegu, tumepanga kuimarisha vituo
vyetu vya utafiti wa mbegu na kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mbegu
hapa nchini. Kwa ajili hiyo nimewaagiza Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi
la Magereza watumie sehemu ya mashamba yao kuzalisha mbegu.
Nafuraji kwamba viongozi wa idara zetu hizo tayari
wameshaelewana na wenzao wa Wakala wa Mbegu nchini kufanikisha mpango
huo muhimu. Kwa upande wa mbolea nafurahi kusema kuwa kauli yangu
niliyotoa Bungeni tarehe 21 Agosti, 2008 kuhusu pesa za EPA imeshaanza
kutekelezwa. Shilingi bilioni 30 zimetengwa kwa ajili ya mbolea ya
ruzuku na bilioni 10 kwa ajili ya madawa ya mimea. Madawa ya mifugo
yametengewa shilingi bilioni 10 na mikopo ya kilimo TIB shilingi bilioni
10.
Ndugu Wananchi;
Nafurahi pia kuwa dhamira yetu ya kuzalisha mbolea hapa nchini
inatekelezwa vizuri. Kiwanda cha kuzalisha mbolea ya phosphate pale
Minjingu, mkoani Manyara kimekamilika na kimeshaanza kazi. Wakati huo
huo mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea ya NPK hapo
Minjingu umeshaanza. Aidha, uamuzi wetu wa kujenga kiwanda cha mbolea ya
urea na ammonia kule Mtwara umefikia hatua nzuri. Kampuni ya kuwekeza
imekwishapatikana na shughuli za mchakato wa ujenzi wa kiwanda hicho
ziko mbioni.
Hatua hizi zote zitakapokamilika, ndani ya miaka miwili
ijayo, zitaiwezesha nchi yetu kuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa mbolea
katika kanda yetu ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tutatosheleza
mahitaji yetu na kuwa na ziada ya kuuza kwa wengine nchi za nje na
kujipatia fedha za kigeni.
Mifugo
Ndugu Wananchi;
Juhudi za kuongeza tija katika kilimo zitaelekezwa pia kwenye mifugo.
Nia yetu ni kuboresha ufugaji wetu ili tupate mifugo inayotoa nyama
nyingi, maziwa mengi na ngozi zilizo bora. Juhudi hizo zitajumuisha
kuboresha aina ya mifugo yetu kwa kutumia madume bora na uhamilishaji.
Pia itahusisha upatikanaji wa huduma za kinga na tiba ya mifugo, majosho,
malisho, maji, masoko ya mifugo na mazao ya mifugo. Suala la kuwa na
viwanda vya kusindika mazao ya mifugo nalo tutalipa uzito unaostahili.
Uwekezaji
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka 2009, tutaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili
kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini.
Sifurahishwi na taarifa nizipatazo kuwa mazingira ya uwekezaji na
kufanya biashara nchini bado hayajaboreka vya kutosha. Na,
linalonisumbua zaidi ni kule kuanza kujengeka dhana kuwa Tanzania
inaanza kupoteza sifa ya mahali rafiki kwa wawekezaji. Hii si dalili
nzuri, lazima tuibadili haraka iwezekanavyo.
Ndugu Zangu;
Dunia nzima hata mataifa tajiri yanavutia wawekezaji seuze siye maskini?
Uwekezaji ndiyo chachu ya kukua kwa uchumi. Bila ya uwekezaji uchumi
haukui. Wote tunaowasifia kufanikiwa kiuchumi ni kutokana na uwekezaji.
Hata China imeendelezwa na uwekezaji tena kutoka mataifa ya kibepari.
Tutayaainisha mambo yanayotufikisha hapo na kuyatafutia
majawabu. Natambua kuwepo malalamiko kuhusu usumbufu na urasimu mkubwa
katika kuwahudumia wawekezaji. Mlolongo na muda wa uamuzi ni mrefu, kuna
usumbufu upande wa kodi na tuhuma za vitendo vya rushwa zinasikika.
Wakati mwingine kauli za wanasiasa wetu zimekuwa zinawaogopesha
wawekezaji. Yote haya na mengineyo ni mambo ambayo yapo kwenye uwezo
wetu kuyarekebisha.
Tumedhamiria kuyakabili kwa dhati matatizo hayo ili tuifanye
Tanzania kuwa nchi nzuri kuwekeza. Pamoja na kusimamia kwa karibu mradi
wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania (BEST), nakusudia kuanzisha
kitengo maalum cha kusikiliza malalamiko ya wawekezaji na kuyatafutia
ufumbuzi (Investors Complaints Bureau). Kitengo hicho kitakuwa chini ya
Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na kazi yake itakuwa ni kutatua kwa haraka
malalamiko ya wawekezaji.
Mikopo ya Wajasiriamali Wadogo na SACCOS
Ndugu Wananchi,
Miaka miwili iliyopita tulianzisha mpango wa mikopo kwa wajasiriamali
wadogo wadogo ambao hawana sifa za kukopesheka katika mabenki kwa
utaratibu wa kawaida. Tumefanya hivyo ili wanyonge nao wapate fursa ya
kujiendeleza na kujikwamua. Kama tujuavyo, tulitenga shilingi bilioni
moja kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na shilingi milioni 100 kwa kila
mkoa kwa mikoa minne ya Zanzibar na milioni 200 kwa mkoa wa Mjini
Magharibi, Unguja.
Tulikubaliana kuwa mikopo hiyo itatolewa na Benki za CRDB na
NMB na asasi ndogo za fedha kama vile Benki ya Posta, PRIDE, SELF n.k.
Taarifa zinaonyesha kuwa hadi Novemba 30, 2008 jumla ya shilingi bilioni
39 zimekopeshwa na NMB (16.1bn/=) na CRDB (22.9bn/=) na watu 48,339
wamenufaika pamoja na SACCOS 192 na vikundi 137. Benki na asasi nyingine
12 zimeshakopesha SACCOS 236 na shilingi 4.6 bilioni zimetumika katika
wilaya 46 za Tanzania Bara.
Katika ziara zangu katika mikoa ya Bara nimepokea malalamiko
ya watu kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo. Moja ya jambo nililojifunza
ni kuwa, mahitaji ya mikopo ni makubwa na fedha zilizotolewa ni kidogo.
Jawabu lake ni kuongeza fedha, jambo ambalo tuko tayari kufanya.
Jambo la pili nililojifunza ni kuwa fedha zilizolipwa na
wakopaji wa awali hazijazungushwa. Jawabu lake ni kuzizungusha ili
wengine nao wakope. Tunazungumza na mabenki juu ya jambo hilo. Ni
dhamira yangu mwaka ujao wa 2009 tufanye tathmini ya kina ya mpango huu
ili tubaini mapungufu yake na mbinu za kuyarekebisha ili tuongeze fedha
na kunufaisha watu wengi zaidi wa kipato cha chini wainue hali zao za
maisha.Kwa nia ile ile ya kuwasaidia watu wasiokuwa na sifa za
kukopesheka moja kwa moja na mabenki wapate mitaji ya kufanyia shughuli
zao za kujipatia kipato, tuliwahimiza wananchi waanzishe Vyama vya
Kuweka na Kukopa. Tulipoingia madarakani kulikuwa na SACCOS 1,875 na
sasa zipo 4,780 kutokana na msukumo maalum tulioutoa kwa uanzishwaji
wake.
Fedha nyingi za akiba zimewekwa na wanachama wa SACCOS hizo
na mikopo mingi imetolewa kwa wanachama hao. Aidha, SACCOS kadhaa
zimeweza kupata mikopo ya kawaida ya mabenki na kupitia mikopo ya
wajasiriamali wadogo wadogo.
Pamoja na kujenga utamaduni mzuri wa watu kuweka akiba,
SACCOS zimekuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi na vyombo vya kutumainiwa
na wananchi wa kawaida katika harakati zao dhidi ya umaskini. Napenda
kuahidi kuwa ni makusudio yetu kuendeleza juhudi za kuimarisha na
kuanzisha SACCOS nchini.
Huduma za Kiuchumi na Kijamii
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka ujao tutaendeleza jitihada za kuongeza na kuboresha
upatikanaji wa huduma muhimu za kiuchumi na kijamii hususan elimu, afya,
maji, umeme na barabara. Kazi kubwa imefanyika na watu wengi sasa
wanapata huduma hizo, lakini bado hazijatosheleza mahitaji na viwango
vya ubora.
Tunatambua wajibu wa Serikali wa kuongeza fedha katika
bajeti za sekta hizo ili miradi mingi zaidi itekelezwe na kukidhi
mahitaji ya wananchi. Hiyo ndiyo dhamira yetu kufanya katika mwaka 2009
na miaka ijayo. Sekta ya maji na umeme vijijini tutazipa kipaumbele
stahiki.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu ya sekondari napenda kwa mara nyingine tena
kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi kwa moyo wao wa kujitolea na
kujituma. Moyo wao huo na ushirikiano wao na Serikali ndiyo siri
iliyotufanya tuendelee kupata mafanikio makubwa katika upanuzi wa elimu
ya sekondari nchini.
Hivi sasa, nchini tunazo sekondari za Serikali 3,039 kutoka
1,202 mwaka 2005 na idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 524,325 mwaka
2005 hadi 1,222,403 mwaka huu. Haya si mafanikio madogo katika kipindi
kifupi hivi.
Naomba moyo huo wa kujitolea na ushirikiano viendelee kwa
manufaa ya watoto wetu na wajukuu wetu waliopo sasa na wajao. Sisi
katika Serikali tunaahidi kuendelea kutimiza wajibu wetu katika
ushirikiano wetu huo. Tutaendelea kukabili changamoto za upatikanaji wa
walimu, vitabu, vifaa vya kufundishia, maabara na nyumba za walimu.
Tunatambua kuwa ni mzigo mkubwa lakini hatuna budi kuubeba kwa maslahi
ya taifa letu.
Matokeo ya Darasa la Saba
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka miwili mfululizo matokeo ya mitihani ya darasa la saba
yamekuwa si mazuri. Mwaka wa jana kiwango cha kufaulu kilikuwa asilimia
54.2 na mwaka huu ni asilimia 51.2. Hali hii si nzuri na hatuwezi kuacha
iendelee. Hatuna budi kujiuliza kulikoni na kutafuta majawabu muafaka.
Nimeiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya uchunguzi wa
kina ili kubaini kasoro zilizopo na kupendekeza hatua za kuchukua. Aidha,
nimemuagiza Waziri Mkuu kulisimamia suala hili kwa ukamilifu.
Barabara
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu tunaoumaliza leo, tuliendelea kutoa kipaumbele cha juu
kwa sekta ya miundombinu. Tumeongeza bajeti ya miundombinu na sasa ni ya
pili kwa ukubwa baada ya elimu. Kiasi cha shilingi bilioni 973.3
zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu nchini katika mwaka wa
fedha 2008/09. Tumeendelea kujenga barabara mpya za lami, za changarawe
na za udongo. Pia tumekarabati na kuimarisha barabara zilizopo.
Lengo letu la kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote kwa
barabara za lami sasa lina muelekeo mzuri. Mipango kwa kuunganisha mikoa
ya Lindi, Mtwara, Rukwa na Ruvuma imefikia mahali pazuri.
Hivi sasa nguvu zetu tunazielekeza kwa mikoa ya Kigoma na
Tabora ambapo naamini mpaka katikati ya mwaka 2009 sura kamili inaweza
kuwa imejitokeza. Nafurahi hata hivyo kwamba, taratibu za ujenzi wa
daraja la Mto Malagarasi zimefikia hatua za mwisho.
Tunasikitika kwamba misukosuko ya mfumo wa fedha wa
kimataifa umetulazimisha kuahirisha kutekeleza mpango wetu wa kupata
fedha kwa kutumia hati fungani (soverign bounds) kwa ajili ya kujenga
kwa kiwango cha lami barabara zetu kuu nyingi hapa nchini. Ni matumaini
yetu kuwa hali ikitengemaa tutautazama upya mpango huo.
Bandari, Reli na ATCL
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2009 tutaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu hali
katika mashirika ya reli, bandari na shirika la ndege. Hali ya huduma
hizo muhimu hairidhishi hata kidogo. Yapo matatizo ya uendeshaji ambayo
yamesababisha huduma zitolewazo kuwa za kiwango kisichoridhisha.
Tutafanya kila tuwezavyo kurekebisha mambo ili huduma hizo ziboreke na
kuwafanya watumiaji kufurahi.
Mapato ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada mwaka ujao tutaendeleza juhudi za kuhakikisha kuwa
mapato ya Serikali yanaendelea kuongezeka. Tutaendelea kuimarisha
Mamlaka ya Mapato na kuziba mianya inayopoteza mapato ya Serikali.
Napenda kutumia nafasi hii, kuwapongeza sana viongozi na
watumishi wa TRA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kukusanya mapato ya
Serikali. Pamoja na matatizo ya hapa na pale hali ya mapato ya Serikali
imeimarika.
Mara mbili katika mwaka huu wamevunja rekodi ya ukusanyaji
wa mapato ya Serikali. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi wa Juni
walipokusanya shilingi 346.7 bilioni na mara ya pili ilikuwa mwezi wa
Septemba walipokusanya shilingi 420.8 bilioni. Tunatambua na kuthamini
juhudi zao na nakusudia kuwatunza kwa mafanikio hayo mwishoni mwa mwaka
huu wa fedha.
Nidhamu ya Matumizi
Ndugu Wananchi;
Sambamba na juhudi za kuongeza na kuimarisha mapato ya Serikali hatuna
budi kuhakikisha kuwa kunakuwepo na nidhamu na uaminifu katika matumizi
ya fedha na rasilimali za Serikali. Nimelisisitiza sana jambo hili na
kuwataka viongozi wenzangu na watumishi wa Serikali kusoma na kuzingatia
maoni na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
yaliyomo katika taarifa zake za kila mwaka.
Nimeagiza Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara, Idara,
Mikoa, Wilaya na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji
kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria ya Fedha na mali za Serikali
na Kanuni zake. Kuna dalili za mabadiliko chanya, lakini hali bado si ya
kiwango cha kutufanya tufurahi sana. Mwaka ujao tutaendelea kubanana
katika jambo hili ili tufikie ufanisi unaotakiwa.
Ndugu Wananchi;
Kuanzia mwaka ujao nitawaomba wakaguzi wa mahesabu ya Serikali
kumkabidhi kwenye vyombo vya sheria mtumishi wa Serikali aliyehusika na
wizi au ubadhirifu mara watakapougundua. Najua utaratibu wa sasa hauko
hivyo. Nataka tuutazame upya utaratibu wetu wa sasa ili isaidie kujenga
nidhamu hata kama ni ya woga wa kufungwa. Itasaidia kunusuru fedha
nyingi za umma zinazotumiwa isivyo.
Ni matumaini yangu pia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali ataendeleza kwa kasi na nguvu zaidi kazi waliyoianza
ya ukaguzi wa thamani ya fedha zilizotumiwa na kulinganisha na kazi
iliyofanyika (value for money audit). Ukaguzi wa asili umekuwa unahusu
uandishi wa vitabu kwa mujibu wa kanuni za fedha. Lakini, inawezekana
kabisa vitabu vya hesabu vikaandikwa vizuri lakini pesa zikatumika
vibaya au hata kuibiwa. Tunataka ulinganifu sawia wa fedha zilizotumika
na kazi iliyofanywa.
Ndugu Wananchi;
Nimewaelekeza wenzetu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
kufanya kazi kwa karibu na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali kusaidia kupambana na wasiozingatia nidhamu ya matumizi ya
fedha na mali za umma hususan wezi na wabadhirifu wa fedha za umma.
Bahati nzuri Sheria ya Mwaka 2007 iliyounda PCCB mpya imetoa
mamlaka ya kufanya hivyo. Nimewataka wawe wakali kwa wala rushwa kama
wafanyavyo sasa, lakini pia wawe wakali kwa wale wote wanaokiuka kanuni
za fedha za Serikali. Vitendo hivyo siyo tu vinaitia hasara Serikali
bali pia vinapunguza uwezo wa Serikali kuwahudumia wananchi walioiweka
madarakani.
Nimewataka waitumie vyema sheria mpya na fursa waliyonayo ya
kuwaongezea uwezo wa rasilimali tuliyowapa kwa kutumiza ipasavyo wajibu
wao. Nimewasihi pia kwamba katika kufanya hivyo wasionee wala kupendelea
watu bali watende haki
Ulinzi na Usalama
Ndugu Wananchi,
Tunaumaliza mwaka wa 2008 hali ya ulinzi na usalama wa nchi ikiwa ya
kuridhisha. Mipaka ya nchi yetu ni salama na nchi ni tulivu. Hatuna budi
kutoa pongeza maalum kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi
nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya. Uhalifu wa makosa makubwa
ya jinai kama vile mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na unyang’anyi
wa kutumia nguvu umepungua.
Taarifa za Januari hadi Novemba, 2008 zinaonyesha kuwa
kulikuwa na matukio ya aina hiyo 8,330 ukilinganisha na matukio 10,381
katika kipindi kama hicho mwaka 2007. Huu ni ushahidi kuwa Polisi
wanafanikiwa kudhibiti uhalifu, hata hivyo bado juhudi ziongezwe ili
matukio ya uhalifu yapungue zaidi. Nafurahi pia kwamba hata ajali za
barabarani zimepungua mwaka huu ukilinganisha na mwaka wa jana.
Mwaka wa jana kulitokea ajali 16,196 kati ya Januari na
Novemba, wakati mwaka huu zimetokea ajali 5,500. Hata idadi ya watu
waliopoteza maisha imepungua kutoka 2,757 mwaka 2007 hadi 1,270 mwaka
huu.
Ndugu Wananchi;
Wakati tunawapongeza wadau na Jeshi la Polisi kwa maendeleo hayo bado
naamini kuwa ajali za barabarani pamoja na idadi ya watu wanaopoteza
maisha au kujeruhiwa na mali kuharibiwa vinaweza kupungua zaidi.
Ajali nyingi za barabarani husababishwa na makosa ya
madereva kutokuheshimu sheria ya usalama barabarani.
Lakini, pia kuna mchango wa Jeshi la Polisi hasa wale wa
usalama barabarani kutodhibiti ipasavyo madereva wazembe. Tatizo hili
lipo kwenye uwezo wa Polisi na wadau kulidhibiti.
Madereva wakubali kuzingatia na kuheshimu sheria ya usalama
barabarani. Wenye magari wahakikishe wanaajiri madereva wenye sifa nzuri.
Aidha, madereva wa mabasi ya abiria watambue kuwa wanabeba binadamu
wenzao ambao kwa kipindi chote cha safari usalama wao uko mikononi mwao.
Makosa madogo ya dereva yanaweza kuwapotezea watu uhai au
kuwapa vilema vya maisha. Lazima watambue umuhimu wa wao kuwa waangalifu.
Polisi nao lazima watimize ipasavyo wajibu wao.
Polisi lazima wawe wakali kuhakikisha sheria za usalama
barabarani zinafuatwa. Naamini Polisi wakiwa wakali tofauti itaonekana.
Mauaji ya Albino
Ndugu Wananchi;
Suala la mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino
nimekwishalisemea mara mbili tatu mwaka huu, na mara ya mwisho wakati wa
Baraza la Idd tarehe 8 Desemba, 2008. Ni mauaji na mateso ambayo hayana
sababu ya kutokea kwa sababu chanzo chake ni cha kipuuzi. Imani kwamba
kiungo cha albino kinampa mtu utajiri ni jambo la kijinga. Nirudie
kuwasihi wenzetu hawa wanaotafuta utajiri wa haraka haraka kuwa juhudi
na maarifa yao ndiyo siri ya kufanikiwa kwao na si vinginevyo. Lakini,
kwa vile wapo watu wanaoamini kuwa wakipata viungo vya albino
watatajirika na wapo waganga na wauwaji, Serikali haina budi kuchukua
hatua za kuwabana watu wote hao na kulitokomeza kabisa tatizo hili.
Tumeunda kikosi-kazi kinachojumuisha Polisi na Idara ya
Usalama wa Taifa cha kuendesha mapambano haya. Hivi sasa wanaendelea na
uchunguzi wa kina nchi nzima kuwatambua wahalifu na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya sheria. Mpaka sasa watu 91 wamekamatwa na kufikishwa
mahakamani na mapambano yanaendelea.
Kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya mapambano haya, mapema
mwaka ujao tutaendesha zoezi la kura ya maoni nchi nzima. Tutawataka
wananchi wawataje watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na mauaji au kukata
viungo vya albino. Wawataje waganga wanaohusika, wauawaji wa albino,
wauzaji wa viungo vya albino na wafanyabiashara wanaotumia viungo hivyo.
Taarifa hizo zitasaidia kuwafuatilia na kuwakamata watu hawa
waovu. Utaratibu kama huu ulitusaidia katika mapambano dhidi ya ujambazi
nchini. Naamini utasaidia kwa hili. Tunafanya matayarisho ya zoezi hilo.
Wakati utakapowadia watu wataarifiwa namna ya kushiriki. Naomba
ushirikiano wa hali ya juu wa wananchi wakati huo. Jitokezeni kuwataja
ili isaidie kukomesha aibu hii kwa taifa letu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa na sifa kubwa katika medani ya kimataifa.
Uhusiano wetu na mataifa yote duniani ni mzuri. Hatuna adui. Hali
kadhalika uhusiano wetu na mashirika ya kimataifa ya kisiasa na kiuchumi
ni mzuri.
Nchi yetu inaheshimika na kutumainiwa katika diplomasia ya
kimataifa. Tumepokea wageni wengi mashuhuri na wengine ni wa kihistoria
kama ziara ya siku nne ya Rais wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush.
Tumekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka huu.
Pamoja na ugumu wake lakini tumeifanya kazi hiyo vizuri na
yapo mambo kadhaa mazuri ambayo nchi yetu itakumbukwa nayo. Miongoni mwa
hayo ni amani ya Kenya, kurejesha umoja wa taifa la Comoro, kuongoza
vyema mijadala kuhusu masuala magumu kama yale ya uundaji wa Serikali ya
Umoja wa Afrika na kuyafikisha mahali pazuri.
Mwaka 2009 nchi yetu itakabidhi uongozi wa Umoja wa Afrika
kwa heshima na upendo mkubwa kutoka kwa wanachama wenzetu na mataifa
mengine duniani.
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa tulivu. Hii inathibitisha kuwa nchi inaweza
kuwa tulivu isipokuwa pale ambapo baadhi yetu tutakapokuwa tumeamua kuwa
isiwe hivyo. Naomba mwaka 2009 uwe tofauti.
Tuache vitendo vya kuchochea ghasia kwa kisingizio chochote
kile. Vitendo hivyo havitavumiliwa hata kidogo. Ni vizuri tukaambiana
mapema tusije tukalaumiana.
Naomba Watanzania wenzangu wote na hasa wanasiasa wenzangu
tuyatambue hayo na tujiepushe nayo. Naomba makundi ya kijamii yatambue
ukweli huo na waache kuwaendekeza wanasiasa hasidi.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalize kwa kuwakushukuru kwa mara nyingine tena Watanzania
wenzangu wote kwa ushirikiano wenu na uelewa wenu na msaada wenu kwangu
na kwa wenzangu wote serikalini katika kipindi chote cha mwaka huu
tunaouaga leo. Tumepita vipindi vya raha na vigumu kwa pamoja na
tunaumaliza mwaka tukiwa wamoja na watu wenye mshikamano.
Naomba tuingie mwaka mpya na moyo huo na tuendelee hivyo.
Nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitamshukuru Mwenyezi Mungu
kwa wema na upendo wake na kutuvusha salama mwaka 2008. Tuzidi kumuomba
atuongoze na kutuvusha salama mwaka ujao na miaka ijayo.
Mimi si Sheikh na wala si mwanazuoni, mimi ni mfuasi tu.
Lipo wazo nimekuwa napewa mara kadhaa kuwa pengine si vibaya kila
mwishoni au mwanzoni mwa mwaka tungekuwa na siku ya maombi ya pamoja
watu wote wote wa dini tukiongozwa na viongozi wa dini zetu kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa mwaka tulioumaliza na kuliombea taifa mema kwa mwaka
unaofuata.
Ni wazo linalovutia wengi lakini sidhani kuwa ni jambo la
kufanywa kwa amri ya Serikali. Nawaachia viongozi wa dini zetu
watuongoze.
Naomba tutakiane
kheri na fanaka tele katika mwaka mpya,
2009.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
|