Mhariri mahiri wa Habari
Leo afariki dunia
09/01/2009

Aliyekuwa Mhariri wa 'HabariLeo', Cassian
Kigeso Malima (44), amefariki dunia. Taarifa iliyotolewa jana na Mhariri
Mtendaji wa TSN Media Group, Issac Mruma, ilisema Malima alifariki dunia
jana jioni katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikokuwa
amelazwa tangu Jumamosi iliyopita.
Malima ambaye hivi karibuni alipandishwa
cheo kuwa Mhariri Msaidizi wa Magazeti ya Mwisho wa Wiki ya Kampuni ya
TSN Media Group, alijiunga na kampuni hiyo Oktoba 10, 2004 akiwa
Mwandishi Mkuu Daraja la Pili.
Baadaye alipanda cheo na kuwa Mhariri wa
Habari wa Daily News na kuwa mmoja wa waanzilishi wa 'HabariLeo' baada
ya kuteuliwa Agosti mosi 2006 kuongoza timu iliyoanzisha gazeti hili la
Kiswahili linalomilikiwa na Serikali.
"Alitegemewa sana katika utendaji kazi,
lakini pia alikuwa mcheshi na rafiki wa kila mtu … aliheshimu kila mtu,"
ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mruma katika taarifa yake alisema
kampuni imepoteza si tu mfanyakazi, bali rafiki aliyekuwa tayari kubeba
jukumu lolote alilopewa na alikuwa mtiifu kupindukia.
Mkewe Malima, Hellen Maro, ambaye walizaa binti, Elizabeth, alifariki
dunia Mei 19, 2006. Malima alizaliwa Mwanza Julai 14, 1965, alipata
elimu yake ya msingi katika shule mbalimbali nchini, kati ya mwaka 1972
na 1979; elimu ya sekondari katika Sekondari ya Mwanza kati ya 1980 na
1983.
Alipata elimu ya sekondari ya juu katika Shule ya Sekondari ya Lake
Mwanza kati ya 1984 na 1986 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Rostav
State cha Urusi kati ya mwaka 1988 na 1994 na kuhitimu Shahada ya
Uzamili katika Uandishi wa Habari.
Katika uhai wake, Malima alifanya kazi katika Mamlaka ya Bandari
Tanzania (THA) kati ya 1987 na 1988; Mwandishi wa Habari Uhuru/Mzalendo
tangu Mei 1988 hadi 1996 alipokuwa Mhariri.
Machi 1998 hadi Septemba 1999 alikuwa Mhariri wa Habari wa Gazeti la
Mtanzania na kuwa Mhariri wa Mtanzania na Mtanzania Jumapili kati ya
Septemba 1999 hadi Julai 2003 na kisha Mhariri wa Habari wa The African
tangu Julai 2003 hadi Oktoba 2004 alipojiunga na TSN.
Aliwahi pia kuwa kiongozi katika vyama mbalimbali kitaaluma ndani na nje
ya nchi ikiwa ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa
Habari za Bunge Tanzania, mbali na kuhudhuria semina, makongamano,
warsha na kampeni mbalimbali nje na ndani ya nchi.
Mruma alisema mipango ya mazishi inafanywa na taarifa kamili itatolewa
baadaye. Mungu amsamehe madhambi yake - AMEN.
|