Hakuna uhaba wa wese
nchini - EWURA
12/01/2009

Wakati hali ya upatikanaji
wa mafuta ya petroli kuwa tete kwa vituo vingi Dar es Salaam, vituo
vingine vilikuwa na hali ya kuweza kusaidia kusukuma magurudumu ya
magari kwa kusaidia gurudumu la maendeleo katika jiji la Dar es Salaam.
Kama ikionekanavyo pichani juu kituo cha Big Bon cha Mtaa wa Msimbazi
kuendelea na huduma hiyo kama kawaida.
Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kuwa hakuna
uhaba wa mafuta nchini licha ya baadhi ya vituo vinavyouza nishati hiyo
kufungwa.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji EWURA) Bw. Michael Mshighwa alisema kuwa mamlaka
imefikia hatua ya kuzungumzia hali hiyo baada ya kuwasiliana na wadau (wasambazaji)
wakuu wa Mafuta ambao kimsingi wana takwimu sahihi zinazoonyesha
kutokuwepo kwa tatizo la ukosefu wa nishati ya mafuta nchini
“Leo
asubuhi tulikuwa na mkutano na wafanyabiashara wakubwa wa mafuta nchini
(wholesalers) ambao wamekanusha taarifa za kuwepo kwa tatizo la uhaba wa
mafuta na kusisitiza kuwa vituo vyao vya kusambazia bado vina
mafuta”Alisema Mshinghwa.
Kuhusu
hali inayoendelea hivi sasa ya ukosefu wa mafuta katika baadhi ya vituo
jijini Dar es salaam na ile iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita,
alisema EWURA imeliona hilo na kwa sasa inatathimini mwenendo wa
utekelezaji wa bei mpya za uuzaji wa mafuta zilizotolewa na mamlaka hiyo
zilizoanza kutumika jana.
Ameongeza kuwa baada ya hapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa
yeyote yule atakayekaidi agizo hilo la kuuza nishati ya mafuta kinyume
na bei elekezi kama ilivyotolewa na EWURA.
“Tumetoa
bei mpya za mafuta zitakazofutwa hivyo tunategemea ushirikiano kutoka
kwa wauzaji katika vituo vya mafuta, baada ya hapo tutajua kama hali ya
ukosefu wa mafuta wikiendi hii ulikuwa ni mgomo wa wauzaji au walikuwa
wanasubiria bei mpya tulizozitoa, kinyume na hapo sheria itachukua
mkondo wake” Alisisitiza
Bw. Mshighwa aliendelea kusisitiza kuwa wadau wote wanaouza mafuta
wamekwisha sambaziwa waraka huo unaoonyesha bei mpya za mafuta
zinazotakiwa kutumiwa.
Pia alisema wadau wengi wamekuwa wagumu kutekeleza matakwa ya serikali
kutokana na mazoea waliyokuwa nayo ya kutoingiliwa katika uuzaji wa
mafuta na kutokana na soko huria kwa muda mrefu na kuongeza kuwa wengi
huwa hawapendi kudhibitiwa.
Hali ya
ukosefu wa mafuta katika baadhi ya vituo vya mafuta hapa nchini kutokana
na kutolewa kwa bei mpya zinazotakiwa kufuatwa na wafanyabiashara wa
mafuta umeleta adha kubwa kwa wamiliki wa magari, wasafiri na watumiaji
wa vyombo mbalimbali vinavyotumia nishati hiyo.
|