Kesi ya twin towers za BoT
yaanza
27/01/2009

MAOFISA
wa ngazi za juu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na
Deogratius Kweka, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kutumia vibaya
madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni
200.
Mbele ya
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Hadija Msongo jana, Wakili wa Serikali
John Lwabuhanga alidai kuwa Liyumba ambaye ni Mkurugenzi wa Utumishi na
Utawala wa BoT na Kweka ambaye ni Meneja Miradi wa BoT, wanakabiliwa na
mashtaka ya kutumia vibaya madaraka wakiwa watumishi wa umma.
Akiwasomea mashitaka, wakili huyo alidai katika mashitaka ya kwanza
dhidi ya Liyumba kuwa, katika siku tofauti kati ya mwaka 2001 na 2006,
akiwa mtumishi wa umma BoT, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuchukua
uamuzi wa kuandaa ujenzi wa jengo la BoT bila kufanya makubaliano na
Bodi ya Uongozi wa BoT.
|