KIKWETE kukutana na BROWN
kabla ya G20
16/03/2009

Rais Jakaya Kikwete akiagana na Mku wa
Majeshi ya ulinzi Davis Mwamunyange (kushoto) Inspekta jenrali wa Polisi,
Said Mwema na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kabla ya kusafiri kwenda London
Uingereza kwa ajili ya ziara maalumu. Rais Jakaya Kikwete ameondoka
nchini kwenda mjini London, Uingereza kuhudhuria mkutano maalum
ulioitishwa na waziri mkuu wa Uingereza bwana Gordon Brown kujadili
kuporomoka kwa uchumi duniani.
Kikwete ni mmoja wa viongozi wachache wa Afrika walioalikwa na
Gordon Brown kwa ajili ya mkutano huo utakaofanyika kwenye jengo
la Lancaster House, kujadili kuyumba huko kwa uchumi
duniani na jinsi kunavyoliathiri bara la Afrika.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu
ilisema kwenye mkutano huo wa leo unaojulikana kama Pre-G20
London Summit Africa Outreach Consultative Meeting, Waziri
Brown anataka kupata msimamo na kuisikia sauti ya bara la Afrika,
sauti ambayo itawasilishwa katika mkutano wa mataifa ya G-20
uliopangwa kufanyika London, Uingereza mwanzoni mwezi ujao.
Kwenye mkutano wa leo, Rais Kikwete, ambaye amemaliza kipindi chake
cha uenyekiti wa Umoja wa Afrika mapema mwaka huu, atawasilisha
maazimio yaliyofikiwa katika mkutano kati ya nchi za Afrika na
Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) uliofanyika mjini Dar es Salaam
kwa siku mbili kuanzia Jumanne ya wiki iliyopita. Mkutano huo wa
kwanza wa aina yake, mbali na kujadili uhusiano kati ya Afrika na
IMF, ulijadili kwa kina kuyumba kwa uchumi duniani na mtikisiko wa
taasisi za kifedha ulivyoliathiri bara la Afrika.
Mkutano huo pia ulipendekeza njia ambazo jumuia ya
kimataifa inatakiwa kuzichukua kupunguza makali hayo kwa bara la
Afrika na katika jitihada za jumla za kupambana na umasikini na
kuwezesha kufanikisha Malengo ya Milenia (MDG's). Pichani kushoto,
Balozi wetu Uingereza Mh. Mwanaidi Maajar akimpokea
Rais mara baada ya kutua uwanja wa ndege wa Heathrow, London kutokea
Dar es Salaam tayari kwa mkutano maalumu kuhusu mtikisiko wa uchumi
duniani ulioitishwa na waziri mkuu wa Uingereza Bw. Gordon Brown.
|