Tanzania hatarini kukosa
rubani Mzalendo
19/03/2009

Kutokana na rubani wengi kuzeeka wa
Tanzania, Tanzania inaweza kujikuta haina hata rubani mmoja mzalendo
katika miaka mitano ijayo. Kutokana na hali hiyo, serikali imeshauriwa
kuweka mkakati kamambe wa kutoa mafunzo kwa marubani wengi zaidi ili
kuepuka aibu hiyo.
Ushauri huo ulitolewa juzi jioni na
Mohamed AbdulKarim, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Utalii
Tanzania, wakati akichangia kwenye mkutano wa wawekezaji wa ndani
ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).
Abdulkarim alisema inapendeza zaidi iwapo
ndege za Tanzania zitakuwa zinarushwa na marubani na wahudumu wazalendo.
"Kuwa na ndege za serikali kunaleta maana zaidi iwapo kutakuwa na
marubani na wahudumu wazalendo na hata vyakula vya Kitanzania ikibidi
viwepo," alisema.
Pia, alisema wakati Tanzania inapata Uhuru
ilikuwa na rubani mmoja hali iliyolazimu nchi za Afrika Mashariki
kuanzisha mkakati wa kufundisha marubani na wahandisi wa ndege. Alisema
watu kumi kutoka Afrika Mashariki walikuwa wakipewa mafunzo kila mwaka
hadi jumuiya hiyo ilipokufa mwaka 1977.
Abdulkarim alisema hata baada ya kuvunjika
jumuiya hiyo, Serikali ya Uganda yenyewe iliendelea na mkakati wa
kufundisha marubani wazalendo. Aliendelea kusema kuwa serikali lazima
iwe na mkakati huo wa kugharamia mafunzo kwa marubani kwa maslahi ya
nchi kwa kuwa, watu wa hali ya chini hawawezi kumudu gharama za mafunzo
hayo.
Alisema kuna wakati Tanzania ilikosa
kabisa marubani na ililazimika kutumia wale waliokuwa jeshini. "Marubani
hawatoshi na waliopo wamezeeka hivyo lazima tuwe na mkakati thabiti wa
kufundisha watanzania urubani".
|