Hotuba ya Rais - Machi
2009
04/04/2009

Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
- Machi 2009
Ndugu wananchi,
Kwa mara nyingine tumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kupata nafasi ya kuzungumza na taifa katika utaratibu wetu wa
kila mwezi. Naomba radhi kuzungumza nanyi leo badala ya jana kwa sababu
ya shughuli za ugeni wa Gavana-Jenerali wa Nchi rafiki ya Australia,
Mama Quentin Bryce aliyetutembelea kuanzia tarehe 30 Machi na kuondoka
leo asubuhi. Leo napenda kuzungumzia mambo matatu.
Jambo la kwanza ni mwenendo wa mvua na hali ya chakula
nchini. Jambo la pili ni hali ya upatikanaji na uzalishaji umeme nchini.
Na, la tatu ni mkutano wa Kundi la Nchi Ishirini Tajiri Duniani au
maarufu kwa jina la G-20 kwa lugha ya Kiingereza. Mkutano unaoanza kesho
(01/04/2009)
mjini London, Uingereza.
Mwenendo wa Mvua Ndugu Wananchi, Kwa kawaida hii ingekuwa
wiki ya pili katika msimu wa mvua za masika kwa maeneo yanayopata mvua
hizo. Mvua ambazo hunyesha kwa wingi na kwa saa nyingi mfululizo. Wakati
mwingine hunyesha kwa siku mbili au hata tatu mfululizo. Lakini, ninyi
na mimi ni mashahidi kuwa mpaka sasa mvua bado hazijaenea maeneo yote na
unyeshaji wake siyo kama ule tuliouzoea.
Ingawaje ni mapema mno kuoneakana tuna mashaka, lakini
hali ilivyo inatupa kila sababu ya kuwa na wasiwasi kuwa huenda mvua za
masika zitanyesha chini ya wastani. Hata wenzetu wa Idara ya Utabiri wa
hali ya Hewa wanaonyesha hofu kuwa huenda mvua za masika zisiwe nzuri
kama tunavyotarajia.
Ndugu Wananchi; Bahati mbaya sana Mikoa inayopata mvua za
masika hivi sasa hazikupata mvua nzuri wakati wa msimu wa mvua za vuli
mwaka wa jana. Kwa sababu hiyo kilimo katika mikoa hiyo kimeathirika,
mavuno yamekuwa chini ya wastani na wako baadhi ya wakulima ambao
hawakujaaliwa kupata chochote kabisa.
Katika hali hiyo basi, kama katika msimu wa masika hali
itakuwa chini ya wastani, ni dhahiri kwamba kutajitokeza tatizo kubwa
kwa upande wa upatikanaji wa chakula na mapato ya wakulima kwa
jumla.Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inafuatilia kwa karibu hali
hii na tumekuwa tunajiandaa kuchukua hatua zipasazo.
Tathmini tuliyoifanya baada ya kumalizika kwa msimu wa
mvua za vuli katika mikoa 9 ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro,
Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Kagera zinaonesha kuwa watu wapatao
279,607 katika wilaya 20 watakabiliwa na upungufu wa chakula katika
kipindi cha miezi ya Aprili na Mei 2009.
Mipango ya usambazaji wa chakula katika wilaya hizo zenye
upungufu inaendelea vizuri. Serikali inaendelea na itaendelea, kukusanya
taarifa za hali ya chakula kutoka wilaya zote nchini na kuzifanyia
uchambuzi na kutazama namna ya kuboresha hali ya upatikanaji wa chakula.
Tutaendelea kutumia akiba yetu ya chakula kuwahudumia wananchi wenzetu
watakaokabiliwa na upungufu wa chakula.
Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kwamba tutafanya
kila tuwezalo kuhakikisha hakuna mtu atakayekufa kwa njaa. Aidha,
napenda kuzihimiza Halmashauri za wilaya zote nchini kuendelea kutuma
Wizara ya Kilimo na Chakula taarifa za hali ya mazao na chakula za
wilaya zao kila wiki ili kuwezesha Serikali kujua hali ya chakula nchini.
Nawataka Wakuu wa Wilaya kulisimamia ipasavyo zoezi hilo.
Na, Wakuu wa Mikoa wahakikishe linafanyika.Wizara ya
Kilimo na Chakula itafanya tathmini ya awali ya hali ya mavuno na
chakula kuanzia mwezi ujao. Wanategemea kukamilisha ripoti hiyo mwezi
Juni, 2009. Hii pia itaiwezesha Serikali kujipanga kukabiliana na hali
ya chakula na mavuno itakayojitokeza.
Wito kwa Wananchi
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua fursa hii kurudia kusisitiza mambo
matano yafuatayo:- Kwanza, kwamba kwa wenzetu wa mikoa ya Rukwa, Ruvuma,
Iringa, Mtwara, Kigoma na Kagera ambako mvua imekuwa nzuri, tuitumie
vizuri fursa hii kuhakikisha kuwa mavuno yamekuwa mazuri.
Pili, kwamba katika mikoa yenye matatizo ya upungufu wa
mvua naomba wananchi watumie mvua zinazonyesha hivi sasa kupanda mbegu
zinazokomaa kwa muda mfupi hasa wapande mazao yanayohimili ukame. Kwa
ajili hii, tutilie maanani mazao ya viazi, muhogo, mtama na uwele. Hii
itatusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa chakula nchini iwapo litatokea.
Tatu, tutumie kwa tahadhari kubwa chakula tulichonacho
nchini. Uhaba wa mvua ukiendelea, hali ya upatikanaji wa chakula nchini
haitakuwa nzuri mwaka huu. Na ukizingatia kwamba hali ya chakula duniani
kwa ujumla pia siyo nzuri ni muhimu wananchi wenzangu tukawa waangalifu
katika kutumia chakula tulichonacho. Ni muhimu kufanya hivyo kwani
inawezekana kabisa mtu ukawa na fedha za kununulia chakula nje ya nchi,
lakini ukakosa chakula cha kununua.
Nne, kwa kuwa mazao ya nafaka ndiyo yatakayoathirika
zaidi na mwenendo wa mvua, napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza na
kuwahamasisha watanzania wenzangu kwamba sasa tuongeze matumizi ya
vyakula visivyo vya nafaka, kama vile, ndizi, muhogo na viazi.
Na, Tano, tuongeze bidii na tija kwenye uzalishaji wa
mazao ya chakula ili tujitosheleze kwa chakula na kuuza akiba nje ya
nchi. Tuzingatie kanuni za kilimo bora na tutumie pembejeo za kisasa.
Aidha, nawaomba tuendelee kuomba dua Mwenyezi Mungu atujalie mvua
itakayonusuru mazao mashambani na kutuepusha na tatizo la upungufu wa
chakula mwaka huu.
Hali ya Upatikanaji wa Umeme NchiniNdugu Wananchi,Kwa
takriban miezi mwili sasa umeme umekuwa gumzo kubwa hapa nchini. Mjadala
umekuwa wa namna mbili.
Kwanza umehusu nia ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO)
kununua mitambo ya Kampuni ya Dowans pale Ubungo. Na, pili, umehusu mgao
wa umeme unaoendelea tangu tarehe 26 Machi, 2009 mpaka sasa hasa hapa
Dar es Salaam na wilaya jirani.
Mgao wa Umeme
Ndugu Wananchi, Kiini cha kuwepo kwa mgao wa umeme ni
kuharibika kwa mitambo miwili ya kuzalisha MW 53 za umeme katika kituo
cha kuzalisha umeme cha SONGAS.
Jumamosi tarehe 28 Machi, 2009 mtambo mmoja wenye uwezo
wa kuzalisha MW 20 ulitengemaa hivyo upungufu umebaki MW 33 kutoka
kwenye mashine ya pili.
Taarifa niliyopewa leo ni kuwa hitilafu yake ni kubwa
hivyo huenda ikachukua mpaka wiki mbili au tatu au zaidi kutengemaa.
Maana yake ni kwamba mgao utaendelea kuwepo kwa kipindi hicho. Hivyo,
Ndugu zangu, mgao huu hauna uhusiano na ile hadhari aliyoitoa Dkt. Idris
Rashid, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alipokuwa akizungumzia suala la
Dowans kuwa nchi inaweza kuingia kwenye giza siku za usoni.
Ndugu Wananchi; Kwa mujibu wa wataalamu wa TANESCO, mfumo
wetu wa umeme nchini, kwa sasa, hauna ziada ya umeme unaosubiri kutumika
kama akiba. Kutokana na hali hiyo, kunapotokea upungufu wowote wa
uzalishaji wa umeme kwa sababu yoyote ile, kama huu uliotokea tarehe 26
Machi, 2009, husababisha kuwepo kwa mgao wa umeme kwa watumiaji.
Umeme wote unaozalishwa hapa nchini hutumika na wala
mahitaji halisi hayajatoshelezwa. Kimsingi umeme unaopatikana na
kutumika ni chini ya mahitaji (supressed demand). Ni asilimia 14 tu ya
Watanzania ndiyo wanaopata na kutumia umeme wakati watu wengi sana
wanaohitaji umeme bado hawajapata.
Ndugu Wananchi; Wakati wote Serikali kwa kushirikiana na
TANESCO imekuwa na mipango ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme
nchini. Kwa upande wa uzalishaji kumekuwepo hata na ratiba ya lini,
kituo kipi na cha ukubwa gani kinaratajiwa kuwepo. Utekelezaji wa
mipango hiyo ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo sasa.
Mwaka 2007, kufuatia matatizo makubwa ya umeme
unaozalishwa kwa nguvu ya maji, mpango huo ukaboreshwa na kuongezwa
ujenzi wa vituo vya kutumia gesi asilia na makaa ya mawe. Utekelezaji wa
mpango wa uzalishaji wa umeme kwa mujibu wa uboreshaji uliofanywa mwaka
2007 uko nyuma ya wakati.
Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia
makaa ya mawe Kiwira umechelewa kwa sababu ya ugumu wa kupata mikopo
kutoka kwenye vyombo vya fedha. Kiini cha tatizo ni hofu inayotokana na
taarifa hasi kuhusu mradi huo. Mradi wa kuzalisha megawati 300 kutokana
na gesi asilimia ya Mnazi Bay unacheleweshwa na matatizo ya sasa ya
kudorora kwa uchumi wa dunia ambapo nimeambiwa kwamba wabia muhimu
wamejitoa kwa sasa.
Ndugu Wananchi,
Kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo ni dalili kuwa
baada ya muda si mrefu hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa mbaya hata
kama mitambo yote ya sasa itakuwa inafanya kazi kwa ukamilifu. Kwa sasa
mahitaji yanaongezeka kwa asilimia 10 – 15 kwa mwaka. Hili ni ongezeko
kubwa sana ambalo linahitaji kusiwepo kukwama kokote.
Kwa nia ya kutaka kupunguza makali ya tatizo hilo, ndipo
uongozi wa TANESCO ukaona waombe kununua mitambo ya Dowans ambayo wakati
huo ilikuwa inatangazwa kuuzwa.
Uamuzi huo ukazua mtafaruku mkubwa ambao sina haja ya
kuelezea kwa kirefu kwani wengi wetu tunaufahamu vizuri. Baada ya kuona
ugumu wa kuendelea na nia hiyo, uongozi wa TANESCO umechukua uamuzi wa
kuachana na nia yao hiyo.
Ndugu Wananchi;
Katika taarifa yake ya kutamka uamuzi wa kuachana na nia
ya kununua mitambo ya Dowans, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alielezea
hofu yake kwamba uamuzi huo unaweza kusababisha nchi kuwa gizani hapo
baadaye.
Taarifa hiyo imeleta hofu kubwa katika jamii. Nataka
kuwatoa hofu na kuwahakikishia Watanzania wenzangu wote kuwa Serikali
itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa nchi yetu haifikii hatua hiyo.
Tutahakikisha kuwa nchi haiwi gizani na kwamba umeme wa ziada unaotakiwa
utapatikana na shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma zitaendelea
kama kawaida.
Ndugu Wananchi;
Tayari Wizara ya Nishati na Madini imeshaanza kuchukua
hatua ambazo zinaonesha kuwa na mwelekeo wa kutia matumaini. Naamini
tutafanikiwa. Tukiwa tayari, taarifa itatolewa. Penye nia pana njia.
Napenda kutumia nafasi hii kusema mambo mawili. Kwanza,
kwamba, nawapongeza viongozi wa TANESCO kwa uamuzi wao wa busara wa
kuachana na nia yao ya kununua mitambo ya Dowans. Wameyasoma vizuri
mazingira na nyakati na kufanya uamuzi muafaka.
Pili, niwaombe wanasiasa wenzangu kuwa, maadam waliokuwa
na nia ya kununua mitambo hiyo hawanayo tena, suala hili limemalizika.
Sioni sababu ya kuendelea kulumbana, kutiana vidole machoni na kutoleana
maneno makali na mengine hata hayastahili kusemwa. Tumekuwa tunawatia
hofu wananchi kwa jambo lisilokuwepo tena.
Nawaomba muzihifadhi nguvu zenu na bongo zenu ili
muwafanyie wananchi mambo yenye tija kwao. Wanalo jukumu kubwa la
kujiletea maendeleo kwa lengo la kujiondoa kwenye umaskini na kuwa na
hali bora ya maisha yao.
Uongozi wetu wanasiasa unahitajika sana katika juhudi zao
hizo. Tuelekeze nguvu zetu na maarifa yetu huko. Wapeni pumzi wananchi
kutokana na malumbano haya.
Mkutano wa G-20
Ndugu Wananchi;
Jambo la mwisho ambalo ningependa kuliongelea leo hii ni
kuhusu msukusuko wa uchumi wa dunia na hasa mkutano wa Kundi la Nchi
Ishirini Tajiri Duniani (G-20) ambao unategemewa kufanyika kesho tarehe
2 Aprili na kumazika tarehe 3 Aprili, 2009 mjini London, Uingereza.
Mkutano huu umeitishwa kutafuta njia za pamoja za
kukabili kudorora kwa uchumi duniani. Mataifa haya tajiri ishirini,
ambayo yanamiliki asilimia 85 ya uchumi wa dunia ni pamoja na Marekani,
Uingereza, China, Japan, Ujerumani, Ufaransa, Afrika ya Kusini,
Australia, Uturuki, Brazil, Canada, Argentina, Mexico, Indonesia, India,
Italy, Urusi, Korea Kusini, Umoja wa Nchi za Ulaya na Saudi Arabia.
Ndugu Wananchi;
Uchumi wa dunia sasa hivi unapita kwenye kipindi kigumu
kuliko wakati wowote katika historia ya dunia. Hali hii isipodhibitiwa
kwa haraka na kwa umakini itakuwa na athari kubwa ya kushusha viwango
vya hali ya maisha ya watu katika nchi zote duniani tajiri na maskini.
Matajiri watakuwa maskini na maskini watakuwa fukara zaidi.
Kama nilivyosema katika hotuba zangu zilizopita, kiini
cha kudorora huku kwa uchumi wa dunia ni machafuko na kuanguka kwa mfumo
wa fedha wa kimataifa. Tatizo lilianzia nchini Marekani na kuenea katika
mataifa tajiri ya Ulaya na Asia.
Mabenki makubwa na madogo yameanguka na kufilisika.
Viwanda vikubwa na vidogo pamoja makampuni makubwa na madogo
yamefilisika na kufungwa. Mamilioni ya watu wamepoteza ajira na
wanaendelea kupoteza ajira.
Maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza nyumba zao za kuishi.
Kwa ujumla, mamilioni ya watu katika mataifa tajiri wanaishi maisha ya
mashaka. Wengi maisha yao yameanza kuporomoka. Nchi zetu hazihusiki na
kuzuka mwa matatizo haya lakini, athari za kudorora kwa uchumi wa dunia
zinatukumba sote.
Tayari tunashuhudia kupungua kwa bei na mahitaji ya
bidhaa za nchi zetu kwenye soko la dunia, kupungua kwa idadi ya watalii
na kupungua kwa uwekezaji na vitega uchumi kutoka nje. Aidha, mapato ya
fedha za kigeni na mapato ya Serikali nayo yanapungua. Mambo haya
hatimaye yatasababisha kushuka kwa uchumi wa nchi zetu, watu kupoteza
ajira na kipato na hali za maisha za watu katika nchi zetu kuporomoka.
Kunahitajika hatua thabiti zichukuliwe na hatua hizo
ziwahusishe na kunufaisha wadau wote. Nchi tajiri duniani zinao wajibu
mkubwa zaidi. Kwanza, zina wajibu wa kuhakikisha kuwa wanadhibiti hali
ili uchumi wa nchi zao usiendelee kudorora. Pia zinao wajibu wa
kuzisaidia nchi kama zetu ziweze kukabiliana na athari za kudorora kwa
uchumi wa dunia. Nchi tajiri zimekuwa zinachukua hatua za kunusuru
uchumi wa nchi zao na bado wanaendelea.
Bahati mbaya nchi zetu maskini ambazo hazina uwezo wa
kuwa na mipango kama hiyo, pamoja na ukweli kwamba nazo pia zinaihitaji
sana, bado hazijasaidiwa.
Ndugu Wananchi;
Mkutano wa kesho wa Mataifa 20 Tajiri Duniani umeitishwa
kujadili hatua zaidi za kuchukua kuzuia mambo yasiwe mabaya zaidi na
kufanya uchumi ukue. Pia wanakusudia kuzungumzia njia za kuepuka maatizo
kama haya yasitokee tena duniani. Katika mkutano wa kesho pia
watazungumzia namna ya kuzisaidia nchi maskini za Afrika na zile
zinazoendelea ziweze kujihami na kukabiliana na athari za matatizo ya
uchumi wa dunia.
Katika mkutano wao wa kwanza, uliofanyika Washington,
Marekani, jambo hili halikufanyika. Wakati ule nikiwa Mwenyekiti wa
Umoja wa Afrika (AU), nilimwandikia Rais George Bush wa Marekani, ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa mkutano ule, kumuomba wayaangalie maslahi ya
Afrika, lakini hatukufanikiwa. Tulipata ahadi kuwa katika mkutano
utakaofuata jambo hilo litazingatiwa.
Tunamshukuru Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. Gordon Brown
kwa kutimiza ahadi yake aliyonipatia kuhusu kujali maslahi ya Afrika
pamoja na kutoa fursa ya ushiriki na sauti ya Afrika kuwepo katika
mkutano huu wa pili.
Kwa nia ya kupata maoni ya Waafrika hasa kuhusu matakwa
na matarajio ya Afrika katika mkutano wa G-20, Waziri Mkuu wa Uingereza,
tarehe 16 Machi, 2009 aliitisha mkutano maalum baina yake na viongozi
kadhaa wa Afrika mjini London, Uingereza. Mkutano huo uliohusisha
viongozi wa nchi za Tanzania, Liberia, Afrika Kusini, Ethiopia, Kenya,
Rwanda, Botswana, Misri, na Cape Verde ulikuwa na manufaa makubwa.
Ndugu Wananchi,
Nilitumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni na mapendekezo ya
mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu za Afrika
na Shirika la Fedha Duniani (IMF) uliofanyika hapa Dar es Salaam kuanzia
tarehe 10 hadi 11 Machi, 2009.
Mapendekezo hayo yalikuwa msingi wa mazungumzo yetu
katika mkutano wetu na Bw. Gordon Brown. Kwa muhtasari, matarajio ya
Afrika katika mkutano wa G-20 ni kwa Afrika kusaidiwa kujikinga na
kukabili madhara ya kudorora kwa uchumi wa dunia.
Miongoni mwa mambo ambayo tuliyasisitiza ni haja ya
kuanzishwa mfuko maalum ambapo fedha zake zitatumika kuzisaidia nchi za
Afrika kuchukua hatua za kunusuru uchumi wao kama wafanyavyo mataifa
tajiri.Kwa maneno mengine tuliunga mkono pendekezo la Benki ya Dunia na
kutaka Mkutano wa G-20 ukubali kwamba asilimia 0.7 ya fedha walizotumia
kugharamia mipango yao ya kuchochea uchumi wao (stimulus packages)
zitengwe kwa ajili ya kusaidia kuchochea kukua kwa uchumi kwa nchi za
Afrika.
Pili, tulisitiza kuwa nchi tajiri zisipunguze misaada ya
maendeleo kwa nchi maskini. Badala yake misaada hiyo iongezwe kama
walivyoahidi kwenye mikutano ya Monterrey, Gleneagles na kwingineko.
Tatu, tulisema kwamba tunatarajia pia misaada kwa Afrika,
na uwekezaji kutoka nje vitaelekezwa katika kujenga na kuboresha
miundombinu, kuleta mapinduzi katika kilimo, kukuza biashara miongoni
mwa nchi za Kiafrika na baina yake na nchi nyingine za dunia na kusaidia
zaidi makundi katika jamii ambayo yanahitaji msaada zaidi (vulnerable
groups).
Nne, kwamba nchi tajiri duniani pamoja na Taasisi za
Kimataifa za Fedha Duniani zilegeze masharti na kupunguza urasimu wa
kupata fedha za misaada na mikopo kwa kutambua kwamba hiki ni kipindi
kugumu na cha dharura. Aidha, masharti ya kukopa kutoka vyombo vingine
vya fedha yalegezwe pia.
Tano, kwamba nchi tajiri zisaidie nchi za Afrika kujenga
mitaji ya vyombo vya fedha vya kikanda kama vile Benki ya Maendeleo ya
Afrika. Na, la sita, kwamba, nchi tajiri zitakubaliana kuruhusu uwazi
katika mabenki yao na taasisi zao za fedha ili kuwezesha nchi za
Kiafrika kufuatilia na kurudishiwa fedha, majumba na rasilimali
zilizoporwa kutoka katika bara letu na kuhifadhiwa kisirisiri katika
mabenki ya nchi tajiri.
Ndugu Wananchi,
Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu Gordon Brown kwa
kuyapokea mapendekezo haya ya Afrika kwa moyo mkunjufu na kuahidi
kuyafikisha na kusaidia kuyatetea katika kikao hicho. Pia tunamshukuru
amepokea rai ya Afrika ya kuwakilishwa kwenye mkutano huo kwa kumwalika
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meles Zenawi, ambaye atatuwakilisha kwa
kofia yake ya Uenyekiti wa NEPAD.
Ndugu Wananchi;
Mkutano huu wa G-20 ni muhimu sana kwani unalo jukumu la
kihistoria la kuuokoa uchumi wa dunia. Kwa msemo wa Kiswahili tungeweza
kusema kuwa kazi ya mkutano huu ni ya kufa na kupona. Mkutano
ukifanikiwa, sote tumenusurika.
Ukishindwa sote tutakuwa mashakani na tunaweza kuangamia.
Tuwatakie viongozi wa G-20 heri na fanaka tele katika mazungumzo yao.
Hatima ya maisha na ustawi wa dunia na watu wake uko mikononi mwao.
Mwisho
Ndugu Wananchi;
Mwisho kabisa napenda kuelezea masikitiko yangu kwa ajali
tatu zilizotokea hivi majuzi. Ya kwanza, ni ile ajali ya magari
iliyotokea mkoani Mbeya. Ya pili, ni ile ya treni mbili zilizogongana
mkoani Dodoma. Na ya tatu ni ajali ya mgodi kufukia wachimbaji, wilayani
Geita. Kwa ajali zote hizo tatu, moyo wangu uko pamoja na familia za
wafiwa na waliojeruhiwa. Majonzi yao ndio majonzi yangu. Na machungu yao
ndio machungu yangu.
Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu
wetu hao mahali pema peponi. Amin! Aidha, tunawaombea majeruhi waweze
kupona haraka na kuendelea na juhudi zao za ujenzi wa Taifa. Kuhusu
ajali ya treni, tutachukua hatua za kisheria kwa wote waliosababisha
ajali hiyo.
Tayari wahusika, wakiwemo dereva wa treni ya mizigo,
Mastesheni Masta na askari wawili waliokuwa kwenye treni ya mizigo
wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za uzembe na kusababisha mauaji.
Aidha, Serikali imeunda Tume ya kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Kwa upande wa ajali ya mgodi, napenda kuwahakikishia kuwa
Serikali itafanya kila tuwezalo kusaidia juhudi za uokoaji. Ni kwa nia
hiyo, nimeagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kusaidia juhudi hizo, na
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja, yupo Geita kwa ajili
hiyo.
Naomba nimalize kwa kuwashukuru na kuwapongeza wananchi
na viongozi wote walioshiriki, na wanaoendelea kushiriki, kwa hali na
mali katika juhudi za uokoaji.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
|