Mabaki ya mabomu ya
Mbagala kulipuliwa
05/05/2009

Kesho kuanzia saa tisa alasiri Jeshi la
Wananchi litalipua masalia ya mabomu yaliyobaki katika ghala la jeshi
hilo katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), 671 Mbagala
kuepusha uwezekano
wa mabaki hayo kuleta madhara zaidi.
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi amesema leo
kwamba kazi hiyo itafanywa na wataalamu wa Jeshi na hakutakuwa na
madhara yeyote kwa watu kwani yatalipuliwa kiufundi. Lakini alisema watu
itabidi kuanzia muda huo wakae mita 500 kutoka eneo la Kambi hiyo.
Kiasi
cha watu 25 wamepoteza maisha yao katika mlipuko huo wa mabomu uliotokea
wiki iliyopita, na mamia walijeruhiwa. Takriban watoto 200 walipotezana
na familia zao, ingawa hivi sasa karibu wote wamerudi makwao.
Mh.
Mwinyi amesema wananchi wasiwe na wasiwasi kwani zoezi hilo litafanyika
kwa umakini. Amesema kwanza kabisa kutakuwa na milipuko miwili midogo
kwa ajili ya kutoa tahadhari. Baada ya hapo amesema itafuatia milipuko
mingine ya mfululizo ya nguvu kiasi; na itaendelea hadi saa 11 jioni.
Mh.
Waziri amewaomba wananchi waondoke maeneo hayo na kuwa umbali wa mita
500 kutoka kambi ya Mbagala na kusisitiza kwamba wananchi wasiwe na hofu
kwani zoezi litaendeshwa kwa utaalamu. Silaha zitakazoharibiwa ni pamoja
na masalia ya risasi, baruti, viwashio na mabomu ambayo hayakuweza
kulipuka siku ilipotokea ajali.
Mh.
Mwinyi amesema mabomu 75 ya kutupa kwa mkono aina ya 'Stick Hand
Grenades' na dazeni kadhaa za viwashio pamoja na fyuzi zake
zitateketezwa. Alisema mabomu hayo inabidi yaharibiwe eneo hilo kwa
sababu yanaweza kulipuka wakati wa kuyahamisha na kuleta madhara kwa
watu watakao yahamisha.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Lukuvi alisema wananchi waendelee na
kazi zao kama kawaida kwani zoezi hilo halitaweza kuingilia kazi za
watu.
Lukuvi
alisema hata wanafunzi waendelee kwenda shule kama kawaida na kusitokee
kisingizio chochote cha wanafunzi au watu kushindwa kwenda kwenye
shughuli zao au shuleni.
Naye
Mkuu wa Usalama wa JWTZ, Brigedia Generali Paul Mella alisema kambi ya
Mbagala ina wanajeshi 200 ambao watasaidia kuwaelekeza wananchi kabla ya
ulipuaji wa mabomu kuanza.
|