Jeetu Patel akiri na
mabilioni ya pesa za EPA
31/05/2009

WAFANYABIASHARA Jayant Kumar maarufu kama
Jeetu Patel na Devendra Patel wamekiri mahakamani kuwa kampuni ya Bencon
Internatinal Limited inayodaiwa kujipatia fedha katika Akaunti ya Madeni
ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni ya kwao. Wafanyabiashara
hao walikiri hayo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati
walipokuwa wakisomewa maelezo ya awali ya kesi yao.
Maelezo hayo yalisomwa na wakili wa
serikali, Timon Vitalis mbele ya jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza
kesi hiyo Ruwaich Meela, Grace Mwakipesile na John Kahyoza. Washitakiwa
hao walikiri kuwa wao ni kati ya wakurugenzi wa kampuni hiyo ambayo
ilianzishwa hapa nchini Aprili 4 mwaka 2005. Pia Jeetu Patel na
mshitakiwa mwingine Amit Nandy walikubali kuwa kampuni hiyo ilianzishwa
hapa nchini Aprili 4 mwaka 2005 na kwamba wao ndio waliokwenda kufungua
akaunti benki.
|