Ajali ya meli Zanzibar
02/06/2009








MELI ya
mizigo ya inayomilikiwa na Kampuni ya Seagul, MV Fatih, imepinduka na
kuzama katika Bandari ya Malindi, Zanzibar. Inasadikiwa baadhi ya watu
wamefariki na watu wengine wamejiokoa katika ajali hiyo ambapo mamilioni
ya mali yanasadikiwa kupotea.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Bakari Khatib Shaaban
amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo, na kusema kwamba Meli hiyo ilikuwa
tayari imeshafunga gati katika Bandari ya Malindi majira ya saa 4.00
kamili uski juzi usiku na abiria waliokuwemo walikuwa wanataka kushuka
lakini ghafla ilipinduka na kuzama baharini.
Kamanda
Shaaban alisema hadi jana mchana ni maiti za watu watatu tu ndizo
zilizoonekana ikiwemo ya mtoto mdogo wa kiume, na watu wazima mwanamke
na mwanaume ambao hawakuweza kufahamika majina yao kamili kutokana na
hakna jamaa waliozitambua maiti hizo. Waliookolewa katika ajali hiyo ni
pamoja na Machano Mkinai Mkaazi wa Mkwajuni na Kitiba Mussa Kitiba, wa
Gamba Mkoa wa Kaskazini 'A' Unguja, Halima Mussa wa Arusha, Hassan Omar,
Maulid Abdalla, wote wa Kisiju Mkoa wa Pwani.
Wengine
ni Fatma Ali Salum, wa Kinyasini Wete kisiwani Pemba, Hawa Juma Saleh wa
Rukwa Tanzania Bara, Zainab Ali Kitiba, Tandale Dar es Salaam, Sharifa
Hamad wa Wingwi Pemba, Ramadhan Juma Mohammed Tandale na Omar Khamis
Mohammed wa Vinguguti Dar es Salaam.
Amesema
baada ya kutokea tukio hilo polisi walitaka maelezo ya Nahodha wa Meli
hiyo, Ussi Ali ambaye wanamshikilia kwa maelezo zaidi lakini lakini
maelezo yake yanaonesha wasi wasi kwa jeshi la polisi kutokana na kuwepo
utatanishi mwingi katika maelezo ya Nahodha huyo.
Kamanda
Shaaban alisema kwamba awali Nahodha alisema katika meli yake kulikuwa
na abiria 25 na wafanyakazi 13, lakini Polisi inatilia shaka taarifa
hizo kwani yawezekana Meli hiyo ilibeba abiria wengi na mizigo hivyo
wanaendelea kumhoji Nahodha huyo hadi hapo maelezo jeshi la polisi
litakapopata maelezo ya kuridhisha kutoka kwa Nahodha huyo.
"Jeshi
la polisi halijaridhishwa na maelezo ya Nahodha bado hasa katika idadi
za abiria alizozitoa lakini bado tunaendelea kumuhoji kwani
hatujaridhika na taarifa yake". Alisema Kamanda huyo.
Kamanda Shaaban alisema jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi wa
kina ili kujua chanzo cha ajali hiyo na haitosita kuwachukulia hatua
wanaohusika na kuwataka wananchi kutulia na kuacha vyombo vya sheria
kufanya kazi zao kwa wazi. Hali katika Bandari ya Zanzibar baada ya
ajali hiyo kutokea ilikuwa kitahanani kwa wananchi wakiwemo
wafanyabiashara waliokuwa eneo hilo wakisubiri mizigo yao na jamaa zao
jambo ambalo lilisababisha msongomano mkubwa kiasi cha kuwafanya Polisi
kuwatawanya kwa kurusha risasi hewani.
Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi lililazimika kuweka doria kali
katika maeneo yote huku wakishirikiana na baadhi ya askari wa vikosi
vyengine kutokana na baadhi ya vibaka kujipenyeza na kuanza kuvuna mali
zilizokuwemo katika Meli hiyo.
Kazi za utafutaji wa maiti nyengine iliendelea kwa siku nzima ya jana
baada ya
wazamiaji zaidi ya 30 wa KMKM kuifanya kazi hiyo baada ya kuwasili saa
8.00 za usiku wa juzi.
Kazi hiyo, baada ya kupatikana kwa maiti tatu ilisita kwa usiku huo,
iliendelea tena asubuhi kuanzia saa nne ambapo waokoaji hao waliamua
kutumia mbinu mbalimbali za kuwawezesha kuingia ndani ya meli hiyo
lakini hadi saa saba mchana walikuwa bado hawajafanikiwa kuingia ndani
ya meli hiyo
Akisimulia mkasa wa ajali hiyo kepteni aliyekuwa akiendesha meli hiyo
Ussi Ali Ussi, alisema wakati akiingia Bandarini ghafla aliona meli hiyo
ikijaa maji na kulala upande wa
kushoto. Alisema alianza safari yake saa 10.00 jioni kutoka Dar es
Salaam na kuja Unguja ambapo aliwasili saa 3.30 usiku lakini akiwa
njiani alipata tatizo la usukuni kutoenda vizuri akiwa karibu na kufika
Bandarini hapo.
Akiendelea alifahamisha ndani ya meli hiyo alibeba mizigo yenye uzito
watani 40, abiria 25 na wafanyakazi wake walikuwa ni 13 ambapo watatu
aliwaona baada ya meli hiyo kuzama lakini kwa wakati huo wa usiku
hakujua wapi walipo. Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Waziri
Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa viongozi waliofika katika eneo la
bandari na Zanzibar kuonana na abiria waliookolewa na kushuhudia ajali
hiyo.
Rais Karume aliwataka mafundi wanafanyakazi ya uokozi kuona kuwa
wanajitahidi kuhakikisha kuitafuta miili zaidi kama bado imo ndani ya
meli hiyo.
Katika bandari hiyo umati mkubwa ulikuwa umesheheni huku mamia ya watu
wakiwa wamekaa nje ya geti la gati wakitaka kuingia ndani kushuhudia
jamaa zao na ajali hiyo ambayo jambo ambalo limesababisha msongamano
mkubwa bandarini hapo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe
alimweleza Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi
Vuai Nahodha, kwamba juhudi za uokoaji inaendelea kwa kushirikiana na
Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Polisi na wadau wengine
wanaojitolea kusaidia uokozi huo.
Jumbe alisema bado ni mapema kuielezea serikali juu ya hatua za kuweza
kuchukuliwa zaidi kwa vile wameanza kuifanya kazi hiyo ambapo imekuwa
ngumu kutokanana na meli hiyo kuwa na mzigo mkubwa kiasi ambacho
kimekuwa kikiwapa usumbufu waokowaji.
Kutokana na kuwepo kwa umma wa wananchi katika eneo la bandari Shirika
la Bandari liliamua kufunga milango yake yote ya Bandari hiyo kwa
usalama wa watu huku waandishi wa habari wakipata kazi kubwa katika
ufanyaji kazi zake kutokana na vikwazo walivyokuwa wakiwekewa katika
eneo hilo.
Jumbe alisema kwamba baadae watajaza upepo Meli hiyo iliyozama kwa
kutumia kifaa maalum ili mizigo na watu waliokuwepo waweze kuja juu
ambapo kazi hiyo itafanywa baada ya maji kujaa kwani kwa wakati huo maji
yalikuwa yanakupwa na kazi hiyo ingeshindikana kufanyika.
Waziri Kiongozi aliwataka Viongozi wa Bandari kuieleza Serikali ni
msaada gani wanaohitaji ili kuweza kufanikisha uokoaji wa mizigo, watu
na meli hiyo ambapo Shirika la Bandari lilisema limejipanga vyema
kukabiliana na janga hilo. Wakati shirika la bandari likitoa ahadi hiyo
hadi sasa hakuna msaada uliopatikana wa kutoa maiti zilizokuwa ndani ya
meli hiyo huku Rais wa Zanzibar akilitaka shirika hilo kuomba msaada
shirika la bandari la Dar es Salaam kuja kusaidia kuwaokoa watu waliomo
ndani ya meli hiyo.
Habari zaidi kutoka kwa abiria walionusurika katika ajali hiyo wamedai
kuwa ndani kulikuwa na watu wengi wanaokisiwa kufikia 100, lakini
Nahodha wa Meli hiyo anapingana na idadi hiyo na kusisitiza kwamba meli
yake ilikuwa na idadi ndogo ya abiria. Halima Mussa mkazi wa Arusha
ambaye amenusurika katika ajali hiyo alisema kwamba wakati tukio hilo
linatokea alikuwa tayati ameanza kushuka ndani ya Meli hiyo, lakini
ghafla aliona ikipinduka wakati ikiwa imefunga gati na baadae akiwa
katika maji alijikuta ameshikilia kitu.
"Mimi namshukuru Mungu kwa sababu nilikuwa nashuka lakini ghafla
nikajikuta nimo katika maji lakini baadae nikakamata kitu bila kukijua
ni kitu gani nilichoshikilia na nikaaza kupiga mayowe ya kutaka msaada
na huku nyuma yangu nasikia sauti nyengine watu wakiomba msaada. Kuna
watu waliokuwepo katika maji ndio wakanisaidia kwa kunambia shikilia
hivyo hivyo hicho kitu na kunitaka ninyooshe mikono ndio waliponiokoa na
kunileta juu" alisema Halima Mussa huku akihema.
Watu waliofika katika bandari ya Malindi yameilaumu serikali kwa
kushindwa kuchukua hatua za dharura za kuweza kukabiliana na shughuli
hiyo ambapo ajali imetokea majira ya saa 4 usiku lakini hadi saa tisa
ndipo waokoaji waliopofika huku wakiwa hawana vifaa vya uokoaji. "Ni
dharau za hali ya mwisho hii maana ajali tokea saa 4 usiku lakini hawa
watu wa KMKM wanakuja sa 9 hawana chochote cha kuweza kuwasaidia kuokoa
abiria matokeo yake wamekuja na kuondoka kwa kisingizio cha kuongojea
maji yakupwe" amesema Ali Haji Mkaazi wa Jang'ombe ambaye ana jamaa yake
katika meli hiyo.
Naye Kepteni Juma wa meli ya Sea Bus amesema ipo haja ya kuwa na timu
nzuri ya waokoaji na diver ili waeze kuwaokoa watu pindipo inapotokea
ajali kama hiyo kwani.
"Lazima tuwe na timu nzuri ya divers wasaidie kuokoa lakini pia tax
force ni muhimu kuwepo kwa ajili ya maafa kama haya na kufuata madili ya
kazi ni kitu cha lazima kwa sisi manahodha ili kunusuru maisha ya watu"
alisema Kepteni huyo.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwaambia waandishi kwamba
wakati umefika hivi sasa kuhakikisha serikali inalifanyia kazi tatizo
hilo ambalo linaweza kuathiri wananchi wengi kwa kuziwajibisha taasisi
husika kwa vile meli hiyo tayari hapo
awali ilipata hitilafu na kulazimika kushusha abiria katika Bandari ya
Mkokotoni baada kupata maharibiko ikitokea Pemba.
Maalim Seif alisema ipo haja kwa serikali hivi sasa kuvifanyia ukaguzi
vyombo vya usafiri kwa kuona inatenganisha huduma kati ya vile
vinavyotoa huduma baharini.
Meli hiyo ambayo inamilikiwa na Said Mbuzi imeelezwa kuwa ilibeba mizigo
mbali mbali ikiwemo Trekta, gari mbili, magunia ya unga wa ngano, sukari,
mchele, magunia ya viazi, ya nyanya, mifuko ya saruji, magodoro na
bidhaa nyengine ambazo zote zimezama huku wajanja wakitumia nafasi hiyo
kuopoa bagodoro na bidhaa nyengine na kukimbia nazo nchi kavu.
Tukio za kuzama kwa Meli hiyo ambayo uzamaji wake unafanana sana na ule
wa
MV Bukoba linatokea wiki moja tu katika kumbukumbu ya kuzama kwa MV
Bukoba mwezi Mei mwaka 1999 ambapo watu kadhaa walifariki dunia na kweka
historia ya Tanzania katika ajali mbaya za meli zilizowahi kutokea
nchini.
|