Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Tutatumia njia nyingine ya kuzalisha umeme - Pinda

07/06/2009

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda, amesema Tanzania imelenga kutumia njia mbadala za kuzalisha umeme badala ya kutegemea nguvu ya maji kama njia pekee ya kuzalisha nishati hiyo.

Alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi wa Uratibu wa Kanda wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Akmel Akpa alipokutana naye nyumbani kwake Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu alisema pamoja na umeme unaotokana na maji, serikali pia imeanza kutumia vyanzo vingine vya kuzalishia nishati hiyo na kuvitaja vyanzo hivyo kuwa ni jua, upepo, mawimbi ya bahari, gesi asilia na nishati mbadala inayozalishwa kwa kutumia takataka na mimea.

“Mimi sikujua kama mawimbi ya bahari yanaweza kuzalisha umeme na nilihofia usalama wa mitambo kwa sababu ya chumvi nyingi kwenye maji ya bahari, lakini wataalamu wamenihakikishia kuwa ni jambo linalowezekana kufanyika bila matatizo makubwa,” alisema.

Alisema inasikitisha kuona watu wa maeneo ya vijijini wakikosa huduma za umeme na kuwafanya wategemee mno mafuta ya taa ambayo ni ghali mno na kuni kama vyanzo vya nishati.

Alisema matumizi ya kuni, yamekuwa yakichangia mno kuharibu mazingira na moshi unawaumiza macho wazee ambao pia huishia kuitwa wachawi.

“Tumeanzisha Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini (REA) kwa sababu tumepania kuinua hali za maisha katika maeneo ya vijijini kwa sababu huko ndiko kutakuwa na uzalishaji mkubwa kulingana na malengo ambayo serikali ya awamu ya nne imejiwekea na hasa hili la kuinua kilimo,” alisema.

Alisema ili kuharakisha utekelezaji wa mpango huo, serikali ilipitisha sheria ya umeme vijijini, ili watu mbalimbali kutoka sekta binafsi ambao watakuwa na uwezo wa kuzalisha nishati hiyo waruhusiwe kufanya hivyo.

Aliipongeza UNIDO kwa kusimamia miradi ya uzalishaji nishati ya gesi asilia katika kiwanda cha kusokota mkonge cha Katani kilichopo Hale, mkoani Tanga, ambacho kinazalisha kilowati 150 kwa kutumia makapi ya mkonge.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa UNIDO alimweleza waziri mkuu juu ya kuwepo kwa haja ya bara la Afrika kujikita katika uzalishaji wa nishati ili liweze kujihakikishia kuwepo kwa huduma hiyo muhimu kwa miaka 20 hadi 30 ijayo.

Alisema upatikanaji wa uhakika wa huduma ya nishati utaliwezesha bara la Afrika kujikita katika biashara ya mazao ya kilimo na usindikaji wa mazao, mambo ambayo alisema UNIDO imeamua kuyasimamia kikamilifu.

“Tunapaswa kusukuma jambo hili kama ajenda mpya kwa bara la Afrika. Uhakika wa nishati utatuhakikishia maendeleo ya bara letu, tutakuwa na uhakika wa kuuza bidhaa zetu kwa sababu tutakuwa tumeziongeza thamani kwa kuzisindika na pia itatupa uhakika wa kipato,” alisema.

Alisema pia kuna haja ya kuwa na kauli mbiu mpya ya ’fursa za utajirisho’ kama kauli mbadala ya 'mkakati wa kupunguza umaskini' na kwamba zikiandaliwa fursa za kuwawezesha watu kupata ajira na kuuza bidhaa zilizosindikwa ni lazima watu wataweza kuondokana na umaskini.

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©