Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Kibaki avunja ukimya

15/06/2009

BAADA ya kukaa kimya kwa muda mrefu tangu mgogoro wa kisiwa cha Migingo kilichopo ndani ya ziwa Viktoria kinachogombewa kati ya nchi yake na Uganda uanze kunguruma, Rais Mwai Kibaki ameamua kuvunja ukimya huo na kutaka mazungumzo yanayohusu kisiwa hicho kuitishwa mara moja.

Rais Kibaki alivunja ukimya huo mwishoni mwa wiki wakati akiwahutubia waombolezaji katika kijiji cha Sichei kilichopo eneo la Bungoma, kaskazini mwa nchi hiyo waliokuwa wamehudhuria kwa ajili ya mazishi ya mama mzazi (Bi Esther Nekesa aliyefariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 85) wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Bw. Michael Kijana Wamalwa.

Rais Kibaki alisema kwamba timu ya pamoja ya wachunguzi ndiyo itakayosema ukweli kuhusu mipaka kati ya Kenya na Uganda na akaonya kuwa ni bora waiache tume hiyo ifanye kazi yake bila kuingiliwa.

Mbali na kutaka mazungumzo hayo yakome, Kiongozi huyo wa Kenya aliwakemea wabunge wa Bunge la nchi hiyo kuacha kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia wa Uganda pamoja na kiongozi mwenzake, Rais. Yoweri Museveni,akisema kuwa mashambulizi hayo ni lazima yakome mara moja.

“Tumechoka kuona wabunge wakijiingiza kwenye malumbano kuhusu Migingo utadhani hakuna mambo mengine muhimu yanayoiathiri nchi. Hali hii imezidi na nitaka malumbano haya yakome mara moja,”alisema Rais Kibaki.

Akizungumzia kuhusu msuada uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wanaoipinga Uganda ambao unamtaka Rais Kibaki kutumia nguvu za kijeshi kukikomboa kisiwa hicho chenye mvutano endapo jitihada za kidiplomasia zitakwama, alisema kwamba jambo hilo haliko katika mipango yake.

“Vita haitatupeleka kokote. Uganda na Kenya ni majirani na wenye lengo moja la kuwa na siasa moja ya shirikisho na wala sio siasa ya pesa nane,"alisema Rais Kibaki.

Alisema, kitu ambacho mataifa yote mawili yanakihitaji kwa sasa ni kila mmoja kufanya mazungumzo na mwenzake na sio kupoteza wakati kuzungumzia kuhusu nani mmiliki halali wa kisiwa cha Migingo.

Rais Kibaki alisema kwamba makubaliano waliyotiliana sahihi na Rais Museveni mjini Arusha yanaonesha wazi jinsi gani walivyoamua kulitafutia ufumbuzi suala hilo la Migingo na akaongeza kwamba hivi sasa fungu linakusanywa ili kutengeneza njia ya kisasa ya reli inayoziunganisha nchi hizo mbili.

“Inaniumiza sana kuona wabunge wanamdhalilisha kiongozi wa Waganda. Rais Museveni ana ufahamu kuliko ninyi nahitaji msitishe udhalilishaji kama huo,” alisema Rais Kibaki.

Alisema, njia nzuri ni kwa raia wa Kenya kuzungumza na raia wenzao wa Uganda ili kutafuta njia mbadala ya kuinua uchumi.

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©