Karume ahimiza Wakulima
kushirikiana
20/06/2009

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
Dk. Amani Abeid Karume amewahimiza wakulima wa Unguja na Pemba
kushirikiana ili kuongeza uzalishaji wa chakula.
Rais Karume aliyasema hayo alipofanya
ziara katika bonde la mpunga la Cheju lililopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa
Kusini Unguja na kuzindua uvunaji wa mpunga katika bonde hilo.
Aliwataka wakulima kuendelea kushirikiana
kwa pamoja katika kuimarisha kilimo kwa kutambua kuwa uimarishaji wa
kilimo utazidisha uzalishaji wa chakula na kuweza kukabiliana na tatizo
la chakula lililopo ulimwenguni.
Akiwahutubia wakulima wa mpunga katika
bonde hilo, Karume alisema Serikali iko katika juhudi za kuimarisha
kilimo ikiwamo miundombinu.
Alisema juhudi za kuliimarisha bonde hilo
zitaendelea kuchukuliwa kwa kuwa limewekwa katika Mpango maalum wa
kilimo cha umwagiliaji maji katika visiwa vya Unguja na Pemba kwenye
eneo lenye ukubwa wa hekta 8,500.
Karume aliahidi kupeleka jenereta kwenye
bonde hilo mara taratibu za kuwekwa mabomba kumalizika.
|