Dinosaur wa Tanzania
kurejeshwa nchini
17/07/2009

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe ametofautiana na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Shamsa Mwangunga kuhusu kurudishwa nchini kwa mjusi mwenye urefu wa mita
za mraba 22 (Dinosaur) aliyechukuliwa na Wajerumani mwanzoni mwa miaka
ya 1900.
Wakati Waziri Membe akisema mpango wa
serikali kumresha mjusi huyo nchini bado thabiti, Mwangunga alisema
serikali inaangalia kama kuna uwezekano huo ama kumwacha mjusi huyo
nchini Ujerumani.
Hata hivyo, Waziri Mwangunga alieleza
ingawa jambo hilo bado linaangaliwa kwa makini, ni bora mjusi huyo
akabaki Ujerumani kupunguza gharama za maandalizi ya kumleta na
kumhifadhi nchini.
Alisema serikali inatakiwa kujenga jengo
la ghorofa tatu kwa ajili ya kumhifadhi mjusi huyo aliyechukuliwa nchini
enzi za ukoloni kati ya mwaka 1918 na 1919 kutoka Kijiji cha Mipingo
mkoani Lindi.
Kwa mujibu wa Waziri Mwangunga, mjusi huyo
anaweza kuendelea kubaki Ujerumani na Tanzania kukusanya mapato
yatokanayo na mjusi huyo akiwa huko kwani gharama za kumrudisha nchini
ni pamoja na kubomoa mifupa yake, kuisafirisha na kuiunda upya.
“Tunajaribu kuangalia kama kuna umuhimu wa
kumrudisha mjusi huyo ama abaki Ujerumani, alisema Mwangunga akijibu
swali la Mbunge wa Masasi, Raynald Mrope".
Mrope alitaka kujua sababu za serikali
kuchelewa kumrudisha mjusi huyo kama ilivyoshauriwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni (UNESCO) baada ya serikali ya
Ujerumani kuendelea kukusanya mapato mengi kutokana na mjusi huyo.
Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa alisema, uamuzi wa kurudisha mifupa ya mjusi
huyo bado upo na serikali imeiandikia nchi ya Ethiopia kuomba wataalam
wa kumsafirisha.

“Nchi ya Ethiopia iliunda kamati
iliyofanikisha kurudisha nguzo za kihistoria nchini humo,” alisema Membe
akielezea wanachama wa kamati hiyo wanaweza kushirikiana na Tanzania
kuona namna ya kumrudisha mjusi huyo.
Picha ya mjusi (Dinosaur) iliyotumika
pichani juu, si picha halisi ya mjusi anayezungumziwa, lakini ZENJYDAR
imetumia picha hiyo kama ni mfano mojawapo wa 'Dinosaur' waliokuwepo na
wanaopatikana Amerika ya Kaskazini (North America), Australia na
Tanzania.
|