Wanafunzi wajawazito
kupewa elimu mbadala
21/07/2009

Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman amesema
Wanafunzi wapatao 14 wamefunga ndoa huko Visiwani Zanzibar. Akasema
wanafunzi hao walioana wao kwa wao msimu uliopita. Waziri amesema hayo
alipokuwa akisoma bajeti ya Wizara hiyo katika mwaka wa fedha wa
2009/2010 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika mjini
Zanzibar.
Akasema
tatizo la ujauzito (mimba) bado linaendelea kujitokeza Visiwani na
kuitaka jamii kushirikiana na Serikali kudhibiti vitendo hivyo kwa vile
vinavuruga maendeleo ya wanafunzi ambao ni taifa la kesho.
Kadhalika
Waziri amesema katika mwaka uliopita, kesi 44 za ujauzito zilipokelewa
ambapo kati ya hizo, 14 zilikuwa zikiwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi
kupeana ujauzito, amesema waziri Haroun,
“Mheshimiwa Spika, kati ya kesi
zilizopokelewa, 14 ziliwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi”. Hata hivyo
amesema wanafunzi waliohusika na sakata hilo wote walifukuzwa shule kwa
vile kitendo hicho hakiwaruhusu kuendelea na masomo kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo
Waziri alisema mpango wa kutoa elimu mbadala umeshaanza utekelezaji wake
Zanzibar ili kuwawezesha wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo
kupata elimu ya ufundi.
Alifafanua
kuwa katika mwaka uliopita, wanafunzi 61 waliweza kuingia katika mpango
huo na wanaendelea kupatiwa mafunzo ya ufundi ikiwemo ufundi seremala,
ushonaji. Alisema jumla ya wanafunzi 41 walihitimu mafunzo yao kwa mwaka
uliopita.
Akasema
sheria inawaruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kwa bahati mbaya, kama
vile kubakwa au mazingira yasiyokuwa rasmi kuendelea na madarasa ya
elimu mbadala lakini sio kwa wanafunzi waliobeba ujauzito kwa hiari yao
na aliliomba bunge lisaidie katika jambo hilo.
|