Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Gharama za kwenda Hijja zapanda Tanzania

24/07/2009

USAJILI wa mahujaji kwa ajili ya safari ya kwenda kwenye ibada ya Hijja ya mwaka huu wa 1430AH wa Kiislamu umeanza, huku gharama za kwenda Hijja zikipanda kidogo ikilinganishwa na mwaka jana.

Gharama za safari ya Hijja kwa mwaka jana ilikuwa ni dola za Marekani 3,150 lakini mwaka huu imepanda kidogo na kufikia dola 3,200 za Marekani.

Hiyo ni kwa mujibu wa viwango vya gharama vya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), lakini katika taasisi nyingine gharama imepanda zaidi ya dola 3,200 za Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Bakwata Makao Makuu, afisa wa idara ya Hijja, Muhidin Hassan alisema, mahujaji wanatarajiwa kuondoka nchini kuelekea Makka, Saudi Arabia, “Hatujajua tarehe rasmi ya kuondoka kwa Mahujaji, lakini wataondoka ndani ya Novemba na kurudi nchini Disemba mwaka huu,” alisema na kuongeza, “Usajili umeanza na maandalizi yanaendelea vizuri kwa sababu watu wanajitokeza kupitia akaunti zetu kutanguliza gharama zao na ni matumaini yetu ukifika mwezi Oktoba tutakuwa na Mahujaji wengi waliokamilisha gharama zao.”

Alisema, gharama ya kila kichwa itakuwa ni dola 3,200 za Marekani ambayo itatumika kwa ajili ya usafiri wake wa ndege kwenda na kurudi Makka, na malazi katika nyumba zilizopo karibu kabisa na misikiti mitukufu ya Makka na Madina.

“Pia fedha hizo zitatumika kwa chakula kwa siku zote atakazokaa nchini Saudi Arabia, Matibabu na kuchinja siku ya Idd na mavazi maalumu ya Hijja (Ihraam),” alisema Hassan na kuongeza.

“Pia fedha hizo hizo zitatumika kwa ajili ya ziara katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina, usafiri wa ndani nchini Saudia na mahema katika sehemu zote atakazokaa.”

Aidha, aliwataka Waislamu wote nchini walioweka nia ya kwenda kutekeleza ibada hiyo kwa mwaka huu, kujisajili mapema katika ofisi za Bakwata makao makuu na matawi yake nchini kote ili kuweza kuratibu safari hiyo mapema.

“Wakijisajili mapema itatusaidia kujua idadi na kiasi cha mahitaji kwa Mahujaji wetu kwa siku zote watakazokaa Makka na Madina - kwa ajili ya ibada ya Hijja,” alisisitiza.

Ibada ya Hijja inafanyika katika mwezi wa 12 (Dhulhijja) kwa mwaka wa Kiislamu na ni mara moja tu kwa kila mwaka, na kila Muislamu mwenye uwezo analazimika kufanya ibada hiyo angalau mara moja katika maisha yake.

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©