Ikulu yavunja ukimya juu
ya madai ya Richmond
03/08/2009

SIKU chache baada ya baadhi ya
wanasiasa kumhusisha Rais Jakaya Kikwete na kashfa ya utoaji wa zabuni
kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC, Ikulu imetoa msimamo wa
kumtetea huku ikitaja mambo manne ambayo alihusika nayo.
Msimamo huo wa Ikulu ulitolewa jana na
Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo kwenye mkutano na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, jana, akisisitiza Rais Kikwete hakuhusika
kwa namna yoyote ile ya kufanikisha zabuni hiyo kutolewa kwa kampuni
hiyo tata.
"Katika siku za karibuni kumekuwepo na
maneno na vijembe ati kuwa, kuna mkono wa Rais Jakaya Kikwete katika
kutoa tenda (zabuni) ya kuzalisha umeme wa dharura iliyopata Kampuni ya
Richmond," alisema Luhanjo akisisitiza:
"Tunapenda kusema tena kwa msisitizo
kuwa maneno hayo si ya kweli na hayana msingi wowote. Rais hajahusika na
uamuzi wa tenda hiyo kupewa Richmond kama vile ambavyo hakuhusika na
kupewa tenda kwa Kampuni za Aggreko na Alstom."
Luhanjo alitaja mambo manne ambayo Rais
Kikwete alihusika katika suala zima la ukodishaji wa mitambo ya
kuzalisha umeme ikiwemo ya Richmond: Kwanza, katika kuamua Tanesco
itumie mitambo ya kukodi kuzalisha umeme na serikali igharamie
ukodishaji huo.
Suala hilo lilikuwa lazima liamuliwe na
yeye kwa sababu lilikuwa linahitaji serikali kugharamia ukodishaji. Kama
si hivyo lisingefikishwa kwake kwani ni jambo ambalo lingekuwa juu ya
Tanesco kuamua kukodisha na kulipia. Gharama hizo hazikuwa zimepangwa
katika bajeti ya serikali, hivyo ilikuwa ni lazima kupata idhini ya rais
ya kutafuta hizo pesa na kuzitumia kwa ajili hiyo.
Pili, Rais alihusika katika kuzungumza
na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kuwaomba wakubali sehemu ya pesa
waliyopanga kuipa Tanzania kama msaada kutokana na mpango wa msamaha wa
madeni itumike kugharamia ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Walikubali, na USD 225 milioni
zilitumika kukodisha mitambo ya Kampuni za Aggreko, Alstom na Richmond (ambayo
baadaye ikawa Dowans) na matumizi mengine ya dharura za umeme. Matumizi
hayo mengine yalijumuisha pia ununuzi wa mitambo ya aina ya Watsilla ya
kuzalisha megawati 100 za umeme pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia.
Mitambo hiyo imeshanunuliwa, kufungwa na tayari inazalisha umeme.
Tatu, Rais alihusika katika vikao vya
Baraza la Mawaziri vilivyojadili matatizo ya upungufu mkubwa wa umeme
nchini na kuamua hatua mbalimbali zichukuliwe kukabiliana na tatizo hilo.
Moja ya hatua zilizoamuliwa kuchukuliwa, ni hii ya kukodisha mitambo ya
kuzalisha umeme. Katika vikao hivyo vya Baraza la Mawaziri alitoa
maelekezo ya mambo ya kuzingatiwa katika zoezi zima la kupata makampuni
au watu watakaotoa huduma hiyo. Hususan, rais alisisitiza kuwa pamoja na
udharura uliokuwepo Kanuni na Sheria ya Ununuzi wa Umma zizingatiwe.
Nne, Rais alikataa Kampuni ya Richmond
isipewe malipo ya awali (down payment) ya USD 10 milioni na kutaka
ukweli kuhusu uaminifu na ukamilifu (integrity) wa kampuni hiyo
ujulikane. Rais alikataa maombi yaliyopelekwa kwake na Wizara ya Nishati
na Madini ya kumwomba aagize Wizara ya Fedha, iilipe kampuni hiyo fedha
hizo.
Rais aliagiza Wizara ya Fedha ibaki na
msimamo wake na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Tanesco
wafanye mambo mawili. Kwanza, wafanye utafiti zaidi kujua undani wa
Kampuni ya Richmond.
Isije kuwa ni kampuni bandia wakapewa
fedha wakatokomea nazo na mitambo isipatikane na hakuna namna ya kuipata
kampuni wala wahusika wake. Pili aliagiza wawatake viongozi wa Kampuni
ya Richmond kwanza walete mitambo, ikishafika, ndipo walipwe. Maagizo
hayo ya rais yalizingatiwa na Kampuni ya Richmond ikapewa sharti hilo.
Lakini, ikashindwa kulitekeleza na kuishia kuingia mkataba na Kampuni ya
Dowans iliyokuja kuleta hiyo mitambo badala yake.
Hivyo ndivyo alivyohusika rais katika
suala zima la ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwa
makampuni ya Aggreko, Alstom na Richmond. Kama kweli kungekuwa na mkono
wake wa upendeleo kwa Kampuni ya Richmond kupata tenda, iweje tena yeye
ndiye akatae kampuni hiyo isilipwe fedha za kianzio mpaka kuifanya
ishindwe kazi? alisema bwana Luhanjo.
|