Vitambulisho vya ukaazi
kutotumika kwenye mitihani Zanzibar
19/08/2009

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),
imesema kitambulisho cha Mzanzibar mkaazi, havitatumika kufanyia
mitihani ya taifa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Elimu na
Mafunzo, Haruna Ali Suleiman wakati akizungumza na wanafunzi walimu na
wazazi katika uwanja wa polisi Madungu kwenye shamra shamra za kilele
cha Elimu bila ya Malipo kwa skuli za maandalizi.
Alisema wizara yake inawataka wanafunzi
waliofikia, kujiandikisha ili kupata kitambulisho hicho kwa vile ni
wajibu wao lakini kwa sasa hakitatumika kwa ajili ya mitihani yao.
Mapema, Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Juma
Kassim Tingwa, aliwataka walimu wakuu wa skuli za sekondari kisiwani
Pemba kufika ofisi za wilaya kupata ratiba ya uandikishaji wa
vitambulisho hivyo ili wawaruhusu wanafunzi wao kwa siku tu za zamu zao
kuwapa nafasi wanafunzi hao kupata masomo yao na kuondoa misongomano
kwenye ofisi hizo isiyokuwa ya lazima.
|