Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Wanafunzi wateketea na moto Iringa

23/08/2009

WANAFUNZI 12 wa kike katika Shule ya Sekondari ya Idodi, wilayani Iringa, wamekufa kwa kuteketea kwa moto na wengine 23 wamejeruhiwa vibaya katika tukio hilo lililotokea kipindi cha usiku.

Habari za awali zilisema kufa na kujeruhiwa kwa wanafunzi hao, kumetokana na moto ulioteketeza bweni lao, saa 8 (nane) usiku wakati wakiwa wamelala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, aliwataja waliokufa katika tukio hilo la kusikitisha kuwa ni, Matilda Mtewele wa kidato cha kwanza, kutoka Tungamalenga,

Digna Ndunguru wa kidato cha pili, kutoka Songea na Cheka Kuyaa, wa kidato cha pili, kutoka Makifu, wilayani Iringa.

Wengine ni, Cesiliana John wa kidato cha pili, kutoka Kitisi, Iringa, Lazia
Kihwele wa kidato cha pili, kutoka Mahuninga,Witnes Mbilinyi wa kidato cha pili, kutoka mjini Iringa,
Stela Mwigavila wa kidato cha pili, kutoka Makifu na Salha Abdula wa kidato cha tatu kutoka Dar es
Salaam.

Marehemu wengine wametajwa kuwa ni, Jesca Wissa wa kidato cha tatu kutoka Idodi, Maria Ndole wa kidato cha nne kutoka Makifu, Adelphina Kwama wa kidato cha kwanza kutoka Makifu na Elizabeth Mtavila wa kidato cha kwanza kutoka Mapogolo.


Kamanda Mangalla alisema chanzo cha moto huo ni mshumaa uliokuwa ukitumiwa na
mwanafunzi, Naomi Mnyali, ambaye alisahau kuuzima, baada ya kumaliza kusoma usiku huo.

Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi, Mkuu wa shule hiyo, Raymond Mlasu, alisema bweni lililoteketea kwa moto, lilikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 461 na kwamba lilikuwa na vyumba 25.
Msalu alisema shule hiyo ina jenereta linalotumika kutoa huduma kati ya 12 jioni hadi saa 5 usiku.

Alisema walipozima jenereta kabla ya tukio hilo, mwanafunzi huyo aliwasha mshumaa ili kujisomea,
lakini alipopatwa na usingizi, alisahau kuuzima, jambo lililosababisha moto ulioteketeza bweni na hatimaye vifo vya wanafunzi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Oscar Gabone,
alisema hospitali hiyo imepokea majeruhi 14 na wengine tisa wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Idodi.

Gabone aliwataja majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kuwa ni, Anoda Pambamaji, Lucy Sawani, Evamary Calus, Anna Mlowoka, Glad Mponzi, Lela Mkuya, Mwinzarubi Elias, Helena
Mapunda, Irene Mponzi, na Pisca Malele.

Wengine ni, Faraja Sodike, Helena Barugu, 
Upendo Nyamaduke, Veronica Nyamla na Sabrina Abdurahaman.

Kwa mujibu wa Dk Gabone, majeruhi waliolazwa katika Kituo cha Afya cha Idodi
ni, Esta Zayumba, Lucy Luvanda , Faraja Palino na Ares Ndaga.




Wanafunzi Sabrina na Irene walisema vifo vya wanafunzi wenzao vimechangia na bweni hilo kuwa na mlango mmoja wa kutokea. 




Walidai kuwa katika hatua za awali za moto huo, walinusa harufu ya
petroli na kwamba walipojaribu kutoka nje, walisukumwa na mtu
asiyefahamika, lakini kutoka nje ya jengo.




Walisema hawakuweza kutambua jinsia wala sura ya mtu huyo ingawa alivaa sweta lenye kofia. Kamanda Mangalla alisema polisi na Idara ya Zimamoto, zinaendelea na uchunguzi kuhusu kiini cha moto huo.

Janga hilo limewacha zaidi ya watoto 400 wakiwa hawana malazi, ambapo Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Assas, Salim Abri alijitolea kutoa magodoro 200 na mablangeti 200 kuweza kuwasitiri wanafunzi hao.

"Ni kweli nimetoa vifaa hivyo baada ya kusikia zaidi ya watoto 400 hawana malazi," alisema Salim Abri bila kufafanua.

Kutoka Moshi, Daniel Mjema anaripoti kuwa serikali imeahidi kugharamia mazishi ya wanafunzi hao.

Kwa mujibu wa Mjema, ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe alipokuwa akizungumza na Mwananchi, mjini Moshi.

Waziri hiyo alisema pamoja na kugharamia maziko ya wanafunzi hao, serikali pia itafanya kila linalowezekana kuwatumia madaktari bingwa kuokoa maisha ya wanafunzi wengine 13 waliojeruhiwa vibaya na moto huo.

"Ni tukio la kusikitisha sana,naishiwa maneno ya kusema, lakini tukio hili ni baya sana tumepoteza vijana wetu wapendwa pale, lakini pia tuna vijana 15 wameungua vibaya sana tuwaombee wapone haraka"alisema Profesa Maghembe.

Profesa Maghembe alisema siku zote kifo kinasababisha masikitiko na majonzi mengi katika familia, jamii, binafsi na kwamba serikali inaungana na familia ya vijana hao katika msiba huu mkubwa.

Profesa Maghembe alisema tukio hilo limewarejeshea Watanzania huzuni na kuwakumbusha tukio lingine baya la moto ulioua wanafunzi wa kike 43 katika Shule ya Sekondari ya Shauritanga, mwaka 1994.

Kiini cha tukio hilo la Shauritanga mkoani Kilimanjaro, bado hakijatangazwa hata baada ya kikosi cha wataalamu wa uchunguzi cha Scotland Yard kilichoshirikiana na wataalamu wa ndani.

Profesa Maghembe alisema wiki iliyomalizika jana imekuwa ni mbaya sana kwa wizara yake kutokana na matukio mbalimbali ya kuhuzunisha likiwamo la kuuawa kwa mwanafunzi wa sekondari ya Umbwe, mkoani Kilimanjaro.

Exuper Kachenje anaripoti kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ametoa salamu za rambirambi kufuatia vifo vya wanafunzi hao wa Shule ya Sekondari ya Idodi. Hali kadhalika, ametoa pole kwa majeruhi wa ajali hiyo mbaya.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, waziri mkuu, alisema kwa niaba ya serikali na yeye binafsi, amesikitishwa na kuhuzunishwa na tukio hilo na kuwaomba wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi kigumu cha majonzi.

"Kwa niaba ya serikali na mimi binafsi, natoa salamu za rambirambi kwa vifo vya wanafunzi, vilivyotokana na ajali hiyo, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na tukio hilo, nawaomba wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, kuwa wavumilivu na wavute subira katika kipindi kigumu cha majonzi," alisema Pinda katika taarifa yake.

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©