Rais afungua milango ya
maswali na maoni kwa Wananchi
13/09/2009

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amefungua milango mipya ya kuwasiliana na
Wananchi wa Tanzania kwa njia ya simu na barua/pepe kwa kuwapa fursa ya
kutoa Maswali na Maoni juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea nchini
pamoja na uongozi wake.
Kwa mara ya kwanza kabisa, rais ameamua
kukutana kichwa kwa kichwa "Live" na wananchi kwa kupitia TV ya taifa
TBC. Programu hiyo ilipangwa irushwe hewani mida ya mchana, lakini
haikuwezakana kwasababu rais alikuwa kafunga ndani ya Mwezi Mtukufu wa
Ramadhan na kuomba iwekwe mida ya usiku baada ya Iftar.

BAADHI YA MASWALI KWA RAIS NA BAADHI YA
NUKUU MUHIMU KAMA IFUATAVYO:-
Richmond na Kagoda
“Kwenye kupambana na Ufisadi na rushwa sina
urafiki wala ndugu ”Ni kweli Richmond ilikuwa ni Ghost Company au
maruani. Nililiona tatizo toka mwanzo nikamwagiza Waziri wa Fedha,
usiwachukulie dhamana hawa, nikamtania ipo siku utakuja kujinyonga
utakuta pesa zimeondoka hawa jamaa hawapatikani na kampuni inaweza kuwa
hewa ”Ni kweli Kuna matatizo katika kuwachukulia hatua maafisa
waliohusika na sakata zima hili kikao cha bunge cha Novemba kitakuwa na
majibu ya hili”.
Nyaraka za dini
“Zimetustusha na kutusikitisha sana, lakini hofu yetu ni uchaguzi ujao
wa 2010 - kwamba kwa sasa watu watapiga kura kwa maelekezo ya viongozi
wao wa dini, nadhani hii si sahihi, tutakaa chini na viongozi hawa wa
dini zote tuzungumze nao muda bado upo”.
Mafisadi Papa
"Mafisadi wakubwa wana maarifa makubwa pia ya
kujificha, hata hivyo tunafanya juhudi kubwa kupambana nao”.
Uhasama wa Wabunge wa CCM
“Kumekuwa na chuki za wazi wazi kati ya wabunge wa CCM na serikali yao
na hata wabunge kwa wabunge wenyewe kiasi cha mtu kutoaminiana hata
Kuacha kinywaji chake mezani kwa hofu kuwa kinaweza kuwekewa kitu kibaya.
Tumeunda timu ya wazee watatu Mzee Mwinyi, Mkapa na Kinana ili kuangalia
hilo”.
Swala la Mafuta Zanzibar
"Hatuna sababu ya kulumbana juu ya hili, linajadilika na linaweza
kuondolewa kama lilivyoingizwa katika mambo ya muungano mwaka ule 1968”.
Kuhusu Kesi ya Zombe
"Sheria imechukua mkondo wake, lakini sisi kama serikali hatukuridhika
hivyo tumekata rufaa juu ya maamuzi ya kesi ile mahakama ya rufaa
tunasubiri”.
Kuhusu Mikoa ya pembezoni
"Kwangu hakuna mikoa ya pembezoni, juhudi za makusudi zinafanywa
kuwaunganisha mikoa yote kwa lami, hasa Kigoma, Kagera na Lindi,
wamechelewa lakini si kwamba tumewatupa, hakuna tuliyempuuza”.
Uhuru wa Vyomba vya habari
“Mfumo wenye uhuru wa kusema, watu kutoa maoni yao naupenda sana kuliko
wa kuwabana watu, na sitofanya jitihada za kuzuia uhuru huo maadamu
unafata maadili ya uhandishi”.
Migomo
“Migomo ni haki ya wafanyakazi, hainisumbui”.
Kuwaziba midomo wabunge wa CCM
“Hakuna jitihada zozote za kuwaziba wabunge
midomo, tunataka waseme, waikosoe serikali yao".
Shule za kata
“Ni kweli kuna tatizo la utekelezaji wake
lakini tunafanya jitihada za dhati kuondoa hilo, likiwemo la Walimu,
Vifaa vya kufudishia, Vitabu na Vifaa vya maabara”.
Maisha Bora kwa kila Mtanzania
“Kwetu hii ni mambo mawili, kwanza huduma za kijamii na kiuchumi na pili
kuongezeka kwa kipato, tunajitahidi katika huduma za jamii kama afya,
elimu, maji na miundombinu na katika kuongeza kipato tatizo kubwa ni
mfumuko wa bei, hili ni tatizo kubwa sana, na kiini chake ni bei za
vyakula, tunapambana nalo hili tulikuwa na SDP na sasa tumeanzisha
Kilimo Kwanza lengo likiwa kujaribu kupambana na hili”.
Safari za Nje
“Nasafiri kwa manufaa ya Taifa, Misaada yote tuliyopata inatokana na
safari hizi, ukijifungia ndani utapata wapi haya? Zinafaida nyingi sana
hizi safari".
Kuhusu Kipindi cha Muulize
Rais
Rais Jaka ya Kikweye alimalizia kwa
kusema “Mfumo huu ni kitu kipya na kimekuwa na manufaa sana, na nadhani
ni wazo zuri na nitaliendeleza, huu ni mwanzo tu”.
|