Nyayo za Binadamu wa kale
zaonekana Tanzania
26/09/2009

Wizara ya Maliasili
na Utalii, inapenda kuujulisha umma kuwa nyayo zingine za Binadamu wa
Kale (Zamadamu) zimeonekana katika mwamba ulioko katika Kempu ya Engare
Sero iliyoko karibu na Ziwa Natron Mkoani Arusha.
Nyayo hizo ambazo
zinakadiriwa kuwa na umri wa miaka 120,000 ziligunduliwa mwaka 2006 na
mfanyakazi wa Kempu ya Engare Sero, Gerald, na mpwa wa mmiliki wa Kempu
hiyo, Juliana Von Mutirs, waliokuwa katika matembezi ya jioni katika
kempu hiyo.
Wawili hao, mara
baada ya kuziona nyayo hizo walimtaarifu mmiliki wa kempu hiyo Bw. Tim
Leach ambaye aliwasiliana na mtaalamu wa akiologia kutoka Chuo Kikuu cha
Pennsylvania, Marekani, Dk. Godwin Mollel na mshauri wake kutoka Chuo
Kikuu cha Rutger cha Marekani, Dk. Carl Swisher, kuja nchini kuchunguza
nyayo hizo.
Mwaka 2008,
wataalam hao wakiongozwa na Bw. Jim Brett wa Taasisi ya Elimu ya
Uhifadhi iliyoko Pennsylvania, walipata kibali cha kufanya utafiti
katika eneo zililopo nyayo hizo. Walichukua sampuli ya majivu na sehemu
ya nyayo kutoka kwenye nyayo nyingi zilizopo eneo hilo kwa ajili ya
kuzifanyia uchunguzi kwenye maabara ya Malikale nchini Marekani.
Jopo hilo la
wataalam 7 wakiwemo Watanzania wawili, Dk. Godwin Mollel na Godfrey
Ollemoita wanaendelea na utafiti kuhusu nyayo hizo za Engare Sero ambazo
zinaonyesha dhahiri unyayo na alama za vidole vyake. Hadi sasa jumla ya
nyayo 57 zimeshafukuliwa katika eneo hilo.
Kwa kuwa nyayo hizo
zina umri wa miaka 120,000, huu ni uthibitisho kuwa hizo ndizo nyayo
kongwe kuliko zote zilizowahi kugunduliwa za binadamu anayefanana na
kizazi hiki ajulikanaye kisayansi kama Homo Sapiens.
Nyayo hizi ziko
kwenye mwamba imara zaidi ukilinganisha na ule ambao Nyayo za Laetoli.
Nyayo za Laetoli zipo Tanzania pia na baada ya kuangaliwa na wanasayansi
tofauti duniani, zinakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 3.6
iliyopita (Laetoli, pichani chini).

Mwezi Agosti 2009,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ladislaus Komba na
Mkurugenzi wa Mambo ya Kale, Bw. Donatius Kamamba, walitembelea eneo la
Ziwa Natron kujionea nyayo hizo, na sasa Wizara inaandaa utaratibu wa
kuzihifadhi nyayo hizo za Binadamu wa Kale.
Dk. Ladislaus
Komba,
Katibu Mkuu
|