Afya ya Kikwete - Ikulu
yavunja ukimya
10/10/2009

Mimi naitwa Dk.Peter Mfisi,ni mmoja wa
madaktari wa Mhe.Rais.Nipo Ikulu.Nimekuwa na Mhe. Rais tangu wakati wa
kampeni mwaka 2005 mpaka sasa.Mwenzangu ni Dk.Mohamedi Janabi ambaye ni
daktari bingwa wa maradhi ya moyo katika Hospitali Kuu ya Taifa
Muhimbili. Nimewaiteni waandishi wa habari kufafanua masuala muhimu
kuhusu afya ya Mhe. Rais kufuatia tukio la Jumapili iliyopita,Oktoba
4,2009, pale Mwanza.Tukio hilo
limeleta mshtuko kwa watu wengi na kuendelea kuwa jambo linalozua
mjadala kuhusu hali ya afya ya Mhe.Rais.Naelewa sababu ya wananchi kuwa
na hofu na kuwapo kwa mjadala miongoni mwao.Rais ndiyo kiongozi wetu
mkuu katika taifa na hivyo kuwa mwenye afya njema ndiyo matakwa ya kila
mwananchi.Naelewa fika kuwa kutokana na kiapo changu cha udaktari na
maadili yangu ya kazi siruhusiwi kutoa hadharani undani wa habari yoyote
inayohusu mgonjwa ninayemtibu bila ridhaa yake.Hata hivyo,kwa kuwa huyo
ni Rais wa nchi,na suala la afya yake ni kwa maslahi ya taifa na umma wa
Watanzania kwa jumla,na kwa kuwa yeye ameridhia kutolewa kwa habari za
afya yake ili watu wajue ukweli na kuondoa hofu,nimeamua kufanya hivyo.
Kama sote tujuavyo,Jumapili iliyopita,
Oktoba 4,2009 mwaka huu, Mhe.Rais Jakaya Mrisho Kikwete,akiwa anashiriki
katika sherehe za miaka 100 ya Kanisa la Africa Inland Church
Tanzania(AICT)kwenye Uwanja wa CCM Kirumba,Mwanza,aliishiwa nguvu na
kulazimika kwenda kwenye chumba cha mapumziko.Baada ya mapumziko ya
dakika 10 hivi,Mhe. Rais alirejea kwenye shughuli hiyo na kuendelea
kushirikiana na waumini wa AICT hadi mwisho wa ratiba yake. Ninapenda
kusisitiza kuwa tukio la Mwanza limetokana na Mhe.Rais kuzidiwa na
uchovu,na wala siyo kwa sababu nyingine yoyote ya kiafya.
Wakati tukio hilo linatokea
nilikuwepo,nilichukua vipimo muhimu kama daktari anavyotakiwa kufanya
linapotokea tukio kama lile kwa mtu.Vipimo vyote vilithibitisha kuwa Mhe.
Rais hakuwa na matatizo yoyote ya kiafya ambayo yangeweza kuhusishwa
kuwa chanzo cha tukio lile. Pressure yake ilikuwa 130/85mmhg ambayo ni
kiwango cha kawaida kwa mtu wa umri wake. Mapigo ya moyo wake yalikuwa
76 kwa dakika ambayo pia ni ya kawaida.Sukari kwenye damu ilikuwa
5.5mmol/l ambayo nayo ilikuwa ya kiwango cha kawaida.
Joto la mwili lilikuwa digrii 37.5
centigrade ambalo ni la kawaida.Mhe.Rais pia hakuwa na kiungo chochote
kilichoonekana kutetereka,jambo ambalo lilithibitisha kuwa hakupata
kiharusi. Kutokana na matokeo hayo,sikuona hatari yoyote ya yeye
kuendelea kushiriki katika sherehe hiyo muhimu kwa wakati huo.Ndiyo
maana niliruhusu aendelee kushiriki sherehe zile mpaka alipomaliza na
kuondoka.Baada ya kurudi Dar es
Salaam siku ile niliwasiliana na madaktari wanzangu wa hapa nchini na
nje ya nchi ambao tumekuwa tunashirikiana nao katika kuchunguza na
kufuatilia afya ya Mhe. Rais.Wote hao baada ya kuwasimulia kilichotokea
na matokeo ya vipimo nilivyomfanyia Mhe. Rais,kwa tafakuri zao hawakuwa
na wasiwasi wowote kuwa tukio hilo lilisababishwa na jambo jingine
lolote,isipokuwa uchovu. Imani yao inatokana na ukweli kuwa wanaifahamu
vizuri hali ya afya ya Mhe.Rais kwa kuwa wanahusika katika kuifuatilia
mara kwa mara.
Mmoja wao alimuona Mhe.Rais siku moja
kabla ya kuondoka New York ambapo alipata nafasi ya kuchunguza afya
yake.Mimi na mwenzangu Dk.Mohammed Janabi,ndiyo wenye dhamana ya
kuiangalia afya ya Mhe. Rais Kikwete kila siku.Tumekuwa tunafanya hivyo
kwa zamu na wakati mwingine kwa pamoja,inapobidi kufanya hivyo.Katika
kufuatilia hali ya afya ya Mhe.Rais tumekuwa pia tukimfanyia uchunguzi
wa afya yake kwa vipindi maalum hapa nchini na nje ya nchi kwa vipimo
ambavyo hapa nchini havipo.
Napenda kuwahakikishia wananchi wenzagu kuwa katika miaka hii minne
Mhe.Rais wetu amefanyiwa uchunguzi wa kina wa afya yake.Nadiriki kusema
kuwa hakuna kipimo ambacho hatujapata kukifanya katika uchunguzi wa
mambo muhimu ya afya yake.Kwa sababu ya kuwatoa hofu wananchi na kwa
vile mwenyewe anaridhia tufanye hivyo napenda kuwapa ufafanuzi kuhusu
hali ya afya ya Mhe. Rais. Katika hali ya kawaida nisingefanya hivyo kwa
sababu maadili ya kazi ya udaktari yanakataza.Naamini madaktari wenzangu
wataelewa mazingira niliyokuwa nayo. Katika kufuatilia afya ya rais
tumekuwa tunaangalia na kuchunguza mambo yafuatayo. (a) Blood Pressure:
Tunafuatilia kwa karibu sana hali ya nguvu ya msukumo wa damu (blood
pressure).
Tunampima mara kwa mara na mwenyewe
tumempa mashine ya kujipima kila siku na anafanya hivyo.Kwa jumla
pressure yake iko kwenye viwango vya kawaida. Aidha, uzito wake wa mwili
unaendena ipasavyo na urefu wake.Mhe.Rais ni mtu mwenye mazoea ya
kufanya mazoezi na yuko makini katika chakula anachokula.
Sisi tunahusika kwa ukamilifu na kuelekeza
kuhusu chakula anachokula. Hatuna matatuzi na Mhe.Rais kwa jambo
hilo.Ana nidhamu ya kujipima pamoja na mazoezi na chakula. (b) Moyo:
Tumekuwa tunafuatilia kwa karibu hali ya afya ya moyo wake. Tumemfanyia
vipimo kama vya ECHO,ECG na vinginevyo, na hatujabaini kuwepo tatizo
lolote. (c) Ubongo: Mwaka uliopita, 2008, Mhe. Rais tulimfanyia
uchunguzi wa afya ya ubongo wake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
hapa Dar es Salaam.Tulitumia kipimo cha CT – Scan na matokeo yameonyesha
kuwa hana matatizo. (d) Ini, Figo, Bandama, Kongosho:
Mhe. Rais Kikwete kila mwaka tunapomfanyia
uchunguzi wa jumla wa afya yake tumekuwa tunamfanyia kuchunguza viungo
vyake muhimu vya tumboni kama vile ini, figo, bandama na
kongosho.Tumekuwa tunafanya hivyo kwa kutumia kipimo cha ultra sound na
kwa kupima damu yake kwa kutumia vipimo muhimu.Uchunguzi huo umebaini
kuwa viungo vyote hivyo ni salama na vinafanya kazi vizuri. (e) Mfumo wa
njia ya Chakula:Mfumo mzima wa njia ya chakula (alimentary canal), yaani
koromeo la chakula, tumbo,utumbo mdogo na utumbo mkubwa nao tumeufanyia
uchunguzi wa kina kama kuna tatizo lolote katika kipindi cha miaka
miwili hii. Mwaka 2007, tulimfanyia kipimo cha colonoscopy mjini Paris,
Ufaransa, kuchunguza hali ya afya ya utumbo mkubwa.
Matokeo ya uchunguzi yalionyesha kuwa
utumbo wake mpana uko salama kabisa na hakuna matatizo yeyote. Daktari
bingwa aliyemfanyia uchunguzi huo ameshauri kuwa Mhe. Rais hahitaji
kufanya kipimo hicho tena mpaka baada ya miaka saba. Nakumbuka pia
daktari huyo alimtania Mhe.Rais kuwa angefurahi kuazima utumbo wake.Wiki
mbili zilizopita,Mhe.Rais akiwa mjini New York,Marekani,alifanyiwa
kipimo cha endoscopy kuchunguza kuanzia koromeo la chakula, tumbo,na
utumbo mdogo.Matokeo ya uchunguzi huo yametoa majibu mazuri kuwa yako
salama. Makusudio ya kufanya vipimo hivi viwili ni kuchunguza maradhi ya
kansa na viashiria vya ugonjwa huo. Bahati nzuri hana maradhi hayo na
wala hakuna dalili yoyote iliyoonyesha kuwapo viashiria vya kansa. (f)
Tezi la Shingo (Thyroid Glands): Aidha, wakati wa safari yake hivi
karibuni majuzi mjini New York, Marekani, Mhe. Rais tulimfanyia
uchunguzi wa afya ya tezi la shingo pamoja na kiwango chake cha utoaji
wa homoni.
Matokeo ya vipimo vyote vilivyofanyika
yameonyesha kuwa hakuna matatizo yoyote. (g) Tezi la Kibofu (Prostate):
Septemba, mwaka huu, 2009, tulifanya uchunguzi wa hali ya afya ya tezi
la kibofu (prostate) kwa kutumia mashine maalum na kwa kuchunguza damu
yake. Vipimo vyote hivyo vimeonyesha hali si mbaya. Tezi lake lina
ukubwa wa kawaida na hata vipimo vya viashiria vya kansa ya tezi hilo (PSA)
tunavyofanya kwenye damu vilikuwa katika kiwango cha kawaida. Mhe. Rais
hana matatizo ya prostate. (h) Macho, Masikio na Pua: Tumeshamfanyia
vipimo vya macho, masikio na pua na vyote viko salama. Mhe. Rais anavaa
mawani lakini hayo si maradhi. Watu wengi baada ya kufikia umri wa miaka
40 si ajabu huhitaji mawani. Tunapofanya uchunguzi wa macho, ukiacha ile
ya kuchunguza uwezo wa kuona, tunaangalia pressure ya macho na hali ya
viungo vya nje na ndani ya jicho. Mhe. Rais hana matatizo yoyote. (i)
Damu: Tumekuwa tunamfanyia Mhe. Rais uchunguzi wa damu yake kwa vipimo
mbalimbali vinavyotumika kutambua maradhi mbalimbali yahusuyo damu
yenyewe na mwili mzima wa mwanadamu. Tumekuwa tunafanya hivyo kila baada
ya miezi sita au panapojitokeza ulazima wa kufanya hivyo.
Tumekuwa tunafanya hivyo hapa nchini na
hata nchi za nje kwa nia ya kulinganisha matokeo yetu na kwa vipimo
ambavyo sisi hatunavyo. Matokeo ya uchunguzi wetu yameonyesha kuwa Mhe.
Rais yuko salama. Hana maradhi ya damu au kisukari,wala ukimwi, au ya
wingi wa mafuta (cholesterol),ama ya kiwango cha madini,au ya tezi la
kibofu,wala ya tezi la shingo, au ya ini, au ya homoni mbalimbali
zilizoko mwilini na mengine n.k. Jambo pekee linalojitokeza ni kwamba
Mhe.Rais ana damu nyingi. Hivyo, tumekuwa tunamshauri kupunguza damu kwa
kuchangia Benki ya Damu.Tunashukuru amekuwa anafanya hivyo karibu kila
baada ya miezi sita.Damu nyingi inaweza kuwa na madhara mwilini lakini
Mhe. Rais hajafikia kiwango cha kuwa ni tatizo la kiafya. Pia
tunamshukuru kwa kuwa mwepesi kukubali kupunguza damu ambayo tunaitumia
kuokoa maisha ya watu wengine.
Hakuna hofu yoyote. Napenda kusema
wazi watu wote wasikie na kwa ukweli kwamba mimi na daktari
mwenzangu yaani Dr. Mohamed Janabi hali ya afya ya Rais silo jambo
linalotutia shaka wala kutusumbua au kutunyima usingizi. Tatizo
pekee ambalo limekuwa likimsumbua Mhe. Rais mara kwa mara ni maumivu
ya shingo yanayotokana na kuumia zamani utotoni na wakati wa ujana.
Kuumia huko ni kwa baadhi ya pingili za uti wa mgongo, sehemu ya
shingo (cervical spine), kuathirika na kumsababishia maumivu. Mara
nyingi matatizo ya namna hiyo huwapata wanamichezo na wanajeshi.
Kutokana na shughuli wazifanyazo. Kuumia siyo jambo la
kustaajabisha.Tutakumbuka kuwa Mhe.Rais amekuwa mwana michezo
hususan mchezaji wa basketball,mpira wa miguu na hata riadha wakati
wa ujana wake.
Pia alikuwa mwanajeshi. Ili kutambua
vizuri tatizo la shingo ili tujue namna ya kumpatia tiba
tumeshamfanyia vipimo vyote muhimu vya uti wa mgongo toka juu mpaka
chini. Tumetumia x-ray,CT–Scan na MRI-Scan.Pia ameshaonwa na
madaktari bingwa wa upasuaji wa mishipa ya fahamu hapa nchini na nje.
Pamoja na kuwepo athari katika shingo,madaktari hao kwa dhati
wameshauri kuwa kwa sasa maumivu yake hayahitaji upasuaji isipokuwa
mazoezi ya viungo. Mhe. Rais amefundishwa mazoezi anayotakiwa
kuyafanya na amekuwa anayafanya kwa nidhamu ya hali ya juu.
Matokeo yake ni kupata nafuu kubwa. Ndiyo maana siku hizo haonekani
kunyoosha shingo mara kwa mara kama ilivyokuwa zamani kwa wale
wanaokumbuka. Tunafuatilia kwa karibu sana hali ya shingo
yake.Tunamfanyia vipimo vya MRI na kuonana na madaktari bingwa mara
kwa mara.
Mwisho Napenda kabla ya kumalizia nisisitize tena kwa kusema kuwa
mimi na daktari mwenzangu hatuna mashaka na hali ya afya ya
Mhe.Rais.Afya yake ni nzuri,hana maradhi yanayotishia maisha yake au
kupunguza uwezo wake wa kulitumikia taifa na watu wake.Pia maoni
yetu hayo ndiyo maoni ya madaktari wa ndani na wa nje waliowahi
kuhusika na uchunguzi wa afya yake. Napenda pia kuwahakikishia
kuwa,sisi madaktari wake, hatutachoka kufuatilia kwa karibu na kwa
umakini mwenendo wa afya ya Mhe.Rais ili tujue mapema kama kuna
jambo la kushughulikia.Kwa hili lililotokea,tutaendelea kuchunguza
kama jambo lolote lililojificha ambalo hatujalibaini. Kwa sasa
napenda kurudia kusema kuwa hakuna ushahidi wa kitaalamu wa kusema
kuwa kulikuwa na sababu nyingine zaidi ya uchovu.
Rais aliondoka New York Septemba tarehe 30 saa nane ya usiku kwa saa
ya hapa Dar es Salaam kuanza safari ya kurudi nyumbani.Aliwasili
nyumbani saa saba ya usiku wa tarehe 1 Oktoba. Njiani alisimama
London na Nairobi kuunganisha ndege. Hivyo basi,alisafiri saa 24
bila ya kulala vizuri. Isitoshe hata kwenye ndege alitumia muda
mwingi akifanya kazi. Asubuhi na mapema siku ya Oktoba 2,aliondoka
Dar es Salaam kwenda Arusha kufungua mkutano wa Wabunge wa Jumuiya
ya Madola saa nne asubuhi.Baadae jioni yake alishiriki kwenye hafla
ya chakula cha jioni alichowaandalia wabunge.
Rais aliondoka saa sita usiku kwenda kulala.Hatuna hakika alilala
saa ngapi kwani najua akiwa na kazi huchelewa sana kulala. Tarehe 3
Oktoba, 2009 alikuwa na mikutano mfululizo na viongozi na wananchi
pale Arusha kabla ya kuondoka majira ya alasiri kwenda
Mwanza.Alipofika Mwanza alikuwa na mazungumzo na wenyeji wake usiku
ule mpaka saa nne ya usiku. Tulipofuatilia tuligundua kuwa hata siku
hiyo nayo alichelewa sana kulala kwani walipondoka wageni wake yeye
aliendelea kushughulikia hotuba yake mpaka karibu na alfajiri.
Katika mazingira hayo kupata matatizo ya mwili kuchoka sana, na hata
kukataa kuendelea kutumika,na kutaka kupumzika kama ilivyotokea si
jambo la ajabu. Mwisho kabisa napenda kuwahakikishia kuwa Rais yuko
salama. Afya yake ni nzuri na haina shaka yoyote. Uchovu uliokithiri
ndicho chanzo cha yaliyotokea Mwanza siku ile ya tarehe 4 Oktoba,
2009. Mimi na wenzangu katika Ofisi Binafsi ya Rais (OBR)
tumejifunza na tumeazimia kuwa waangalifu zaidi katika kupanga
ratiba ya kazi ya Rais.
Ikulu, Dar es Salaam
Daktari wa Rais
|