Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuchapisha noti mpya

16/10/2009

SERIKALI imeanza mchakato wa kuchapisha upya fedha zake za noti zitakazokuwa na sura na muundo mpya, ambazo zitaanza kutumika baada ya miezi minane ijayo ambapo fedha zilizopo zitaendelea kutumika kama kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu alisema tayari mchakato wa kuzipata kampuni zitakazochapisha fedha hizo umekamilika.

"Tayari tumekwishapata kampuni mbili za kutoka nchi mbili tofauti kwa ajili ya kuchapisha fedha zetu mpya za noti yaani Sh 500, 1000, 2000, 5000 na 10000," alisema Profesa Ndullu.

Profesa Ndullu alifafanua kuwa serikali imeamua kuchapisha fedha hizo ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupambana na uingizwaji wa fedha bandia na haramu katika matumizi, pamoja na kuziboresha kulingana na matumizi.

Gavana huyo alisema awali kampuni 10 ziliomba tenda ya kuzichapa noti hizo, lakini ni kampuni tisa ndizo zilizobainika kuwa na uwezo wa kuchapa fedha hizo katika kiwango kinachohitajika.

"Tulizichuja hizo kampuni tisa na tukapata kampuni mbili ambazo ni Cren Currency ya nchini Sweden itakayochapisha noti za Sh 500, 2000, 5000 na 10,000, wakati noti za Sh 1000 zitachapwa na kampuni ya De-rarue ya nchini Uingereza," alisema gavana huyo.

Profesa Ndullu ambaye hivi karibuni alitunukiwa nishani ya gavana bora alisema kutokana na kampuni nyingi kujitokeza kuomba tenda hiyo zimesaidia kupunguza gharama za uchapishaji wa fedha hizo.

Katika hatua nyingne, Profesa Ndullu alisema kimsingi hakuna sababu ya kuundwa kwa chombo maalumu kitakachosimamia Benki Kuu katika utendaji wake.

Alisema kinachohitajika kwa sasa ndani ya BoT ni ufanyaji kazi kwa uwazi na uwajibikaji.

Pia Profesa Ndullu alisema BoT wanatakiwa kuwa wawazi katika ripoti zao ambazo zitasaidia ukaguzi kuwa mzuri.

"Kinachohitaji kwa sasa ndani ya BoT ni wafanye shughuli zao kwa uwazi na uwajibikaji na pia wawe wazi katika ripoti zao, ili kufanya ukaguzi kuwa mzuri," alisema Profesa Ndullu.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano unaohusu usimamizi na uratibu wa sekta ya kibenki nchini, ulioitishwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu nchini (CAG), Eva Lindstr÷m ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Sweden, alishauri kiundwe chombo kitakachosimamia Benki Kuu (BoT) katika utendaji wake.

Lindstr÷m alisema Serikali ya Sweden imeunda chombo hicho ambacho ni huru na kuwa siyo sehemu ya Benki Kuu.

Alisema chombo hicho ni taasisi huru ya serikali ambayo siyo sehemu ya Benki Kuu ya Sweden, inasimamia mfumo mzima wa kifedha nchini humo ikiwemo mabenki, mashirika ya umma na ya mashirika ya pensheni.

Kauli hiyo ya Lindstr÷m, iliungwa mkono na CAG, Ludovick Utouh, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Mzee pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Dk Willibrod Slaa, ambao walisema kuundwa kwa taasisi hiyo huru kutasaidia kupunguza upotevu wa fedha katika benki hiyo.

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©