Pangani yapewa hadhi ya
Kihistoria na Kiutamaduni duniani
17/10/2009

SHIRIKA la Makumbusho Duniani la World
Monuments Fund (WMF) limeutambua na kuupa heshima mji wa Pangani kuwa
mmoja wa miji mikongwe ya kihistoria na urithi wa Utamaduni duniani.
Mkurugenzi wa shirika la Uzima kwa Sanaa (UZIKWASA) la mjini Pangani,
Dkt. Vera Pieroth alisema mjini huo wa kihistoria umetajwa kuwa ni
miongoni mwa miji 93 ya urithi wa Utamaduni iliyopo katika nchi 47
duniani zinazotambuliwa na shirika hilo.
Vera alisema kuwa uamuzi wa kutunuku mji huo heshima hiyo umetangazwa
hivi karibuni na Rais wa WMF, Bonnie Burnham, jijini New York, Marekani
ambapo mji wa Pangani umekuwa kati ya maeneo manne katika bara la Afrika
ambayo imepewa hadhi na WMF.
“Kuteuliwa kwa mji wa Pangani ni faraja kubwa kwa watu wa hapa na
shirika letu la UZIKWASA. Tangu mwaka 2007 shirika letu kwa kushirikia
na Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Kamati za kijamii tumekuwa
kutangaza vivutio vya kihistoria vya mji hapa na tunafurahi sasa juhudi
za pamoja ambazo zimeleta matunda mazuri,” alisema.
Miaka miwili iliyopita UZIKWASA kwa kushirikiana na Idara ya mambo ya
Kale iliendesha kongamano la kujadili jinsi ya kuhifadhi na kutanga Mali
kale na urithi wa Utamaduni wa Pangani, lililofadhiliwa na Ubalozi wa
Ujerumani na Wizara ya Maliasili na Utalii, na baadaye kufanyika utafiti
wa kubainisha maeneo ya urithi wa utamaduni na historia yaliyopo katika
Wilaya ya Pangani.
“Utafiti ulitusaibia kubainisha mambo mbalimbali, wananchi wengi
walishiriki katika kutaja maeneo muhimu, kuibua vitu vya kizamani, kutoa
picha na michoro, vyombo na mambo mengine mbalimbali ya kihitoria ambayo
tuliyaweka kumbukumbu ambazo baada ya kupata baraka za Wilaya tulituma
WMF na hatimaye tumepata heshima hii,” anasema.
Kwa kutambuliwa na shirika la WMF lililoanzishwa mwaka 1965 kwa lengo la
kuhifadhi, kutunza na kuendeleza maeneo ya makumbusho ya urithi wa
Utamaduni na mali kale, mji wa Pangani sasa unatangazwa na kutambuliwa
rasmi kuwa ni sehemu ya Utalii wa kihistoria na kiutamaduni Duniani.

Ramani ya Pangani, Tanzania.
|