Rais aamrisha mitambo
mipya ya umeme (IPTL) kuwashwa haraka
24/10/2009

WAFANYABIASHARA na wawekezaji nchini
katika kongamano la kujadili fursa za utalii nchini, mjini Dar es
Salaam, jana, Jumanne, Oktoba 20, 2009 walimwomba Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuingilia kati
matatizo ya sasa ya mgawo wa umeme kwa kuruhusu kuwashwa kwa mitambo ya
kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa tayari
Mhe. Rais ameingilia kati kumaliza mgawo wa sasa wa umeme nchini.
Tokea majuzi, Mhe. Rais alikwishakutoa maagizo kwa Wizara ya Nishati na
Madini, pamoja na Kampuni ya TANESCO, kuchukua hatua za kuhakikisha
mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL inawashwa, haraka iwezekanavyo, na
umeme unaanza kupatikana.
Kutokana na kuharibika kwa mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas, Ubungo,
mjini Dar es Salaam, na Kihansi, Mkoani Iringa, Gridi ya Taifa ina
upungufu wa megawati 80, ikiwa ni megawati 20 ambazo kwa kawaida
huzalishwa na Songas, na megawati 60 ambazo huzalishwa Kihansi.
IPTL kwa sasa haizalishi umeme. Lakini ina uwezo wa kuzalisha megawati
90 hadi 100. Hizi zinatosha kuziba pengo la sasa la megawati 80 katika
Gridi ya Taifa, na kumaliza mgawo wa sasa wa umeme.
Ni kweli kwamba IPTL iko kwenye mchakato wa ufilisi ambao unaendelea
sasa mahakamani, lakini Mhe. Rais Kikwete ameelekeza kuwa mchakato wa
ufilisi mahakamani hauzii mitambo ya kampuni hiyo kuwashwa na kuzalisha
umeme wakati malumbano ya kisheria yakiendelea kortini.
Katika kuhakikisha kuwa umeme unapatikana haraka iwezekanavyo, Mhe. Rais
Kikwete ametoa maagizo mbalimbali kwa Wizara za Serikali kama ifuatavyo:
(a) Wizara ya Nishati na Umeme, kwa kushirikiana na TANESCO, imeagizwa
kusimamisha masuala yote ya kiufundi ikiwa ni pamoja na upatikanaji
haraka wa mafuta, ili umeme huo wa IPTL uanze kuzalishwa mara moja.
(b) Wizara ya Fedha na Uchumi imeagizwa kuhakikisha kuwa inatafuta fedha
za kuwezesha ununuzi wa mafuta na mahitaji mengine muhimu, ili umeme
uweze kuzalishwa.
(c) Wizara ya Katiba na Sheria imeagizwa kuhakikisha kuwa inasimamia
masuala yote ya kisheria yanayohusu suala hilo.
Katika kutekeleza maagizo hayo ya Mhe. Rais, jana, Jumanne, Oktoba 20,
2009, Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, tayari aliitisha kikao maalum cha
Mawaziri wa Nishati na Madini, Fedha na Uchumi, Katiba na Sheria,
TANESCO na vyombo vingine husika katika suala hilo kujadili jinsi ya
kuhakikisha kuwa umeme wa IPTL unawashwa haraka.
Kupatikana kwa umeme wa IPTL utawawezesha mafundi ambao kwa sasa
wanahangaika kutengeneza mitambo ya Songas na Kihansi kuifanya kazi hiyo
kwa utulivu zaidi.
Mhe. Rais Kikwete anaelewa fika matatizo yanayowapata wananchi kwa
sababu ya mgawo wa sasa wa umeme, na madhara yake kwenye uchumi wa nchi.
Lakini anapenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa mgawo wa sasa wa umeme
utakwisha katika siku chache zijazo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
|