Hati ya Muungano
Tanganyika-Zanzibar kuwekwa hadharani
31/10/2009

SERIKALI imesema mkutano
ujao wa bunge itagawa kwa wabunge pamoja na kuweka katika maktaba
mbalimbali pamoja na makumbusho Hati ya Muungano kwa kuwa ni haki ya
kila mtu kuufahamu mkataba huo.
Aidha pamoja na kuweka katika maeneo
hayo, bado hati hiyo itawekwa katika mtandao maalumu kumuwezesha kila
Mtanzania kuiona na kuisoma kwa urahisi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano), Mohamed Seif Khatibu aliwaambia wabunge kwamba hati ya
Muungano ni nyaraka ya umma na kila raia ana uhuru na haki ya kuipata na
kuitumia.
Khatibu alisema hati hiyo ni sehemu ya
sheria za Muungano (The Act of Union) ya sheria nambari 22 ya mwaka 1964
na kwamba haki hiyo iliridhiwa na kupatikana na katika maktaba ya bunge
pamoja na sheria namba 22 ya mwaka 1964.
Awali Mbunge wa Tumbe, Salim Abdallah
Khalfan, alitaka kujua hati ya mkataba wa Muungano (Article of Union) ni
waraka muhimu wa historia ya nchi na akahoji ni kwa nini waraka huo
hauonekani wazi.
Mbunge huyo pia alitaka kujua vipi
nafasi ya kawaida kuweza kuupata na kuutumia waraka huo na kama serikali
itakuwa tayari kuusambaza waraka huo kwa baraza la wawakilishi, wabunge
pamoja na maeneo ya maktaba za vyuo na makumbusho ya Taifa.
Hata hivyo, Waziri aliwataka wabunge
kutumia nafasi hiyo kusoma vitu mbalimbali katika maktaba ya bunge kwa
kuwa waraka huo upo tangu Februari 11, 2002 hivyo aliwataka wabunge
wanaohitaji kujua waende katika maktaba yao kwa ajili ya kuusoma.
|