Stendi ya Ubungo
yakabidhiwa serikali
02/11/2009

KAMPUNI ya Smart Holdings, iliyokuwa
ikisimamia uendeshaji wa Kituo Kikuu cha Mabasi ya kwenda mikoani cha
Ubungo, Dar es Salaam, imekabidhi rasmi kituo hicho kwa serikali.
Makabidhiano hayo yalifanyika juzi usiku kwa mujibu wa Mkurugenzi
mtendaji wa kampuni hiyo Hassan Khan, inafuatia kumalizika kwa mkataba
wa miaka mitano ya kuendesha kituo hicho.
"Makabidhiana hayo yalifanyika usiku wa saa sita kwa sababu ya mkataba
wetu ulikuwa unaishia siku ya 'wikiendi," alisema Khan.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, shughuli hizo zilishuhudiwa na Mkurugenzi
wa Jiji la Dar es Salaam Alhaji Kingobi na viongozi wengine wa jiji.
Kampuni hiyo iliyoendesha kituo cha mabasi Ubungo tangu mwaka 2004,
imekuwa ikihusishwa na mwanasiasa mkongwe hapa nchini Kingunge Ngombale
Mwiru, lakini juzi Khan alikanusha kuwa mzee huyo na familia yake
hawahusiani na kampuni hiyo.
Alisema kampuni hiyo inamilikiwa na yeye, Victor Mwiru na Peres Mwiru
ambao hata hivyo, wakuwepo kwenye tukio la kukabidhiana kituo.
Khan alikuwa akijibu swali kuhusu wamiliki wa kampuni hiyo ambapo
alisisitiza kuwa inamilikiwa kwa ubia.
Kampuni hii si ya kiongozi huyo
anayetajwa tajwa wa watu, kampuni hii ni ushirikiano wa Hassan Khan,
Victor Mwiru na Peres Mwiru, ambao wameungana na kuianzisha," alisema
Khan.
Wakati wa ziara yake mwanzoni mwa mwaka
huu katika kituo hicho Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliagiza kufanyika
kwa uchunguzi wa hesabu za uendeshaji wa kituo hicho.
Hatua hiyo ilikuja baada ya baadhi ya wafanyabiashara kulalamikia
ubadhirifu waliodai kuwa umekuwa ukinafanywa na viongozi wa kituo hicho
chini ya Kampuni ya Smart Holdings.
Matokeo ya ukaguzi huo uliofanywa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa
Hesabu za Serikali (CAG) yalionyesha kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha
katika uendeshaji wa kituo hicho.
|