UMEME wa IPTL kuwashwa
05/11/2009

HATIMAYE kampuni ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL), imesema sasa inaweza kuwasha mitambo yake ya
kuzalisha umeme baada ya serikali kuilipa kiwango walichokubaliana na
kukamilika kwa matengenezo.
Serikali ilitangaza kuwa mitambo hiyo, inayoendeshwa kwa dizeli na yenye
uwezo wa kuzalisha megawati 100, ingewashwa Novemba mosi baada ya Rais
Jakaya Kikwete kuagiza “iwashwe mara moja, lakini baadhi ya mafundi wa
kampuni hiyo waliiambia Mwananchi kuwa uwezekano wa kuiwasha tarehe hiyo
ulikuwa ni mdogo na mitambo hiyo haijawashwa hadi sasa.
Jana, meneja utawala na uendeshaji wa IPTL, Venerabilis Jigge aliwaambia
waandishi wa habari ofisini kwake Tegeta jijini Dar es salaam kuwa
mitambo hiyo itawashwa wakati wowote wiki hii baada ya kukamilika kwa
ukarabati na malipo hayo kwa ajili ya uendeshaji.
Meneja huyo hakutaja kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali, lakini
alisisitiza kuwa malipo hayo ni muhimu kwa uendeshaji wa mitambo hiyo.
Alieleza kuwa kuchelewa kwa malipo hayo kulisababisha ukarabati wa
mitambo hiyo kuchelewa na hivyo kuchelewa kuiwasha.
Juzi serikali ilitulipa fedha tulizokuwa tumekubaliana. Tunategemea
kuwasha mitambo wiki hii kwa kuwa fundi mkuu ametuthibitishia na
tumeshakamilisha kila kitu ambacho kilikuwa kinaonyesha kuwa kinaweza
kuwa kikwazo kwa kampuni katika uendeshaji mitambo hiyo, alisema Jigge.
Kwa mujibu wa meneja huyo, tayari IPTL imekabidhi fedha hiyo kwa kampuni
ya Wartsila ambao wameingia mkataba wa miaka miwili na serikali
kuendesha mitambo yake ya umeme.
Hivi sasa kazi ni kwa waendeshaji (Wartsila), kwani fedha tumeshawalipa
jana(juzi) na mafuta yataanza kuingia leo (jana) jioni, alisema Jigge.
Jigge alisema ili kufanikisha kazi hiyo, tayari IPTL imeagiza tani 7,500
za mafuta kwa gharama ya Sh 7.5 bilioni.
Fundi mkuu wa kampuni ya Wartsila, Jaakko Kaihua alisema ukarabati wa
mitambo hiyo unaendelea vizuri na kwamba, wakati wowote wiki hii
itawashwa na kuzalisha umeme.
kama unavyosikia sasa mitambo inanguruma... tunaichemsha kwa sababu
imekaa siku nyingi hivyo lazima tuichemshe,alisema Kaihua.
Alisema mafundi wa kuendesha mitambo hiyo walianza kuingia jana kutoka
sehemu mbalimbali duniani na wataendelea kuja kadiri watakavyohitajika.
Siwezi kuahidi siku maalum ya kuanza kuwasha mitambo hii kwani bado
tunaendelea na ukarabati lakini, hali si mbaya na ni matengenezo madogo
tu yanayoendelea,alisema Kaihua.
Mitambo hiyo, ambayo inahusisha sehemu kumi ambazo kila moja ina uwezo
wa kuzalisha megawati 10 kwa kila mmoja, ilifungwa nchini mwaka 1998.
Rais Kikwete aliagiza mitambo hiyo iwashwe mara moja baada ya wananchi
na wafanyabiashara kumlilia kutaka aingilie kati kutatua tatizo kubwa la
mgawo wa umeme unaondelea nchi nzima.
Kupungua kwa uzalishaji umeme kulikosababisha mgawo huo kumetokana na
kuharibika kwa mitambo ya Songas inayotumia gesi asilia, na mingine
kwenye mabwawa ya Kihansi na Hale na kupungua kwa kiwango cha maji
katika mabwawa ya Kihansi na Pangani. |