Balozi wa Afrika Kusini
asifia hatua ya Zanzibar
12/11/2009

AFRIKA Kusini imeeleza kuridhishwa na
mazungumzo kati ya rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Amani Abeid Karume na Seif Sharrif Hamad ambaye ni katibu mkuu wa CUF na
kueleza kuwa hatua hiyo ni changamoto kwa bara la Afrika.
Afrika Kusini pia imeeleza kuwa hatua
ya viongozi hao wawili wa vyama vyenye upinzani mkubwa kwenye visiwa
hivyo, imeonyesha kukua kwa demokrasia.
Balozi wa Afrika Kusini, Sindiso
Mfenyana, ambaye anamaliza muda wake nchini, alisema hayo jana wakati
alipokuwa na mazungumzo na Rais Karume Ikulu mjini Zanzibar.
Balozi Mfenyana alimueleza Rais Karume
kuwa hatua hiyo ni somo kubwa kwa nchi za barani Afrika, ikiwemo nchi
yake ya Afrika Kusini kwani kilichozingatiwa zaidi ni maslahi ya
wananchi na nchi yao.
Mfenyana alieleza kuwa Afrika Kusini
itaendelea kuimarisha uhusiano na udugu wake na Zanzibar na kusisitiza
kuwa hatua hiyo ina matarajio makubwa ya kusonga mbele kisiasa, kiuchumi
na kijamii.
Alieleza kuwa mazungumo hayo yanatoa
faraja kubwa na ni imani yake kwamba Zanzibar itaendelea kupiga hatua
kubwa katika maendeleo yake, ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo
sanjari na kuimarisha amani na utulivu uliopo.
Alisema kuwa hatua ya kukaa kwa pamoja
kati ya viongozi hao imeudhihirishia ulimwengu kuwa Wazanzibari wote ni
wamoja na tofauti zao za kisiasa haziwezi zikawatenganisha.
Habari na Salma Said, Zanzibar.
|