Maafa wilayani Same -
Kilimanjaro
18/11/2009

SIMANZI na vilio vilitawala kwenye mazishi
ya watu 2O waliofariki dunia kwa kufunikwa na kifusi kilichoporomoka
mlimani na kufukia nyumba zao usiku wa manane katika Kata ya Mamba
Miamba, wilayani Same, Kilimajaro. Waandishi wa habari walishuhudia watu
zaidi ya 1,000 waliokusanyika katika msiba huo mkubwa wakiwa wamefunikwa
na simazi, huku wakilia kwa uchungu kutokana na kupoteza ndugu zao ama
jamaa zao ama marafiki katika msiba huo. Asilimia kubwa ya watu
walionyesha masikitiko yao, hasa kwa familia ambayo imepoteza watu 15 na
kati ya hao wanne hawajapatikana mpaka sasa.

Wananchi hao waliiomba serikali iwasaidie
kutafuta miili ya watu hao na ikiwezekana watumie kikosi cha mbwa ili
kubaini mahali ilipo. Elineema Shambi, mmoja wa ndugu wa wanafamilia 15
waliofariki dunia na ambaye alinusurika kwa vile alikuwa amekwenda mjini
Moshi kwa shughuli za kibiashara, alisema kwa majonzi kwamba amepoteza
mke na watoto wake wanne ambao walifukiwa na kifusi hicho.

Alisema alikwenda mjini Moshi kununua
bidhaa za kuuza, na kesho yake asubuhi alipigiwa simu na kuondoka mara
moja. Alieleza kuwa alipofika alikuta nyumba yake imefunikwa kabisa
kiasi cha kutoonyesha kama kulikuwa na nyumba na mwili wa mkewe ulikuwa
haujapatikana hivyo akasaidia kuutafuta na kuupata pamoja na miili ya
watoto wake. Alifahamisha kuwa yeye ni mmoja kati ya ndugu wa watu 15
waliofariki katika tukio hilo.

Akisimulia juu ya maporomoko hayo, alisema,
dalili za mlima huo kuporomoka zilianza kuonekana mwaka jana kwa kuwa
kulikuwa na ufa, hata hivyo hakueleza kwamba ni kwa nini hawakuhama
katika eneo. Akiunga mkono maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Monica Mbega alibainisha kuwa wananchi wa Kata ya Mamba Miamba
walishaona dalili za kuporomoka kwa mlima ulioua watu 20, tangu mwaka
jana, lakini hawakuchukua tahadhari.
|