KOMBE la Dunia laingia
Tanzania
19/11/2009

KOMBE la Dunia la FIFA limezuru Tanzania
kabla ya kuelekea Afrika ya Kusini ambapo kutakapochezewa mashindano ya
kugombea kombe hilo mwakani 2010. Rais Kikwete alipewa fursa ya
kulinyanyua kombe hilo huku mwakilishi wa FIFA bwana Hadi Amal (kushoto)
akiangalia.
Hotuba ya Rais Kikwete katika hafla ya uzinduzi wa Kombe la Dunia:
Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni na
Michezo,Mheshimiwa Joel Bendera (Mb;)
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe.Chiku Garawa;
Waheshimiwa Wabunge;
Wawakilishi wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA;
Viongozi wa Kampuni ya Coca-Cola;
Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF;
Wageni Waalikwa;Mabibi na Mabwana;
Najisikia mwenye furaha kubwa
kupata fursa hii ya kujumuika nanyi katika tukio hili la kihistoria
kuhusu ziara ya Kombe la FIFA la Dunia hapa Tanzania.Nchi yetu
imebahatika, kwa mara nyingine tena, kupata ugeni huu mkubwa wa Kombe la
FIFA la Dunia ambayo ndiyo tuzo ya juu inayotolewa kwa nchi bora kuliko
zote katika soka duniani.
Hii ni mara ya pili sasa kwa FIFA
kutupa heshima hii. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2006.Napenda
kuwashukuru FIFA na Coca- Cola kwa upendeleo huo kwa nchi yetu.Kabla ya
FIFA na Coca-Cola kuanzisha ziara ya Kombe la FIFA la Dunia, wapenda
soka wengi duniani walikuwa wanaliona kombe hili kupitia kwenye picha za
magazeti na luninga.
Leo hii kupata bahati ya kuliona kombe
lenyewe “live” ni jambo la kihistoria litakalodumu katika kumbukumbu
yetu kwa miaka mingi. Naipongeza FIFA kwa kuanzisha utaratibu huu wa
kuwezesha maelfu ya wapenda soka duniani kuliona kombe hilo kwa karibu
na wengine hata kupata nafasi ya kulishika na kupiga nalo picha.
Hii ni fursa ya pekee na ya kujivunia.
Kwa Watanzania wenzangu tuichukulie ziara ya Kombe la Dunia nchini mwetu
kama ni changamoto kubwa kwetu inayotutaka tufanye vizuri zaidi katika
soka ili tulingane nayo heshima hii tuliyopewa.
Hasa ni changamoto kwa viongozi wa soka
wa ngazi zote pamoja na wachezaji na wapenzi wa mpira wa miguu nchini.
Kuja kwa kombe hili ni deni kwetu na kulilipa kwetu sisi ni kuzinduka,
tuendeleze kiwango chetu cha soka nchini ili na sie siku moja tushiriki
fainali za kombe hili.
Hili ni jambo linalowezekana. Wapo
wenzetu Afrika wameweza, kwa nini sisi tusiweze. Wao ni watu kama sisi,
maadamu wameweza na sisi tutaweza. Lakini, ili tuweze hatuna budi kuiga
mfano wao hususan waliyofanya na wanayoendelea kufanya kuendeleza mpira
wa miguu. Twende tukajifunze kutoka kwao.
Lakini hata kabla ya kwenda huko, yapo mambo ambayo hatuna budi
kuyafanya. Naomba nitaje baadhi yake:-
1. Tuimarishe uongozi, utendaji na
uendeshaji wa vilabu vya mpira. Mchezaji hufundishwa kucheza mpira
katika klabu yake. Hapo ndipo hufundishwa maarifa ya kucheza mpira na
vipaji kuendelezwa. Hebu tujiulize hali ya vilabu vyetu vya soka nchini
ikoje.
Je vinaongozwa vizuri? Vinaendeshwa vizuri? Jibu tunalijua sote kwamba
ni hapana. Lazima suala hili tulitafakari kwa yakini na kulipatia jawabu.
Tukishindwa kupata jawabu muafaka na mambo yakaachwa kuendelea yalivyo,
mpaka mwisho wa dunia hatutakuwa tumesogea popote.
2. Tupate walimu wenye ujuzi na uzoefu kufundisha timu zetu. Hii ndiyo
njia ya uhakika ya kukuza na kuendeleza vipaji na hivyo kupata wachezaji
walio bora.
3. Tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka umri
mdogo. Vilabu viwe na timu za watoto na vijana. TFF isaidie kuanzishwa
kwa shule za mchezo wa mpira wa miguu kwa watoto na vijana. Mashuleni
wapatikane walimu wa michezo walio wazuri kufundisha.
4. TFF ionekane zaidi ya ilivyo sasa katika mipango ya kuendeleza soka
mashuleni, vijijini, mitaani na hata vilabuni. TFF ikiwa na mipango na
ikasimamia na kuwabana wadau kuitekeleza itasaidia. Vinginevyo TFF
itabakia kusimama ligi kuu, kutoa adhabu kwa wachezaji, na timu ya taifa.
Hiyo haitoshi.Napenda kutumia nafasi
hii kutoa pongezi kwa kampuni ya Coca-Cola kwa mchango wake muhimu
inaotoa kuendelea mchezo wa soka nchini na hasa soka la vijana.
Mashindano ya Kombe la Copa Coca-Cola kwa vijana wa chini ya miaka 17 ni
ushahidi tosha wa mchango huo adhimu.
Mashindano hayo yamegusa vijana wengi
kote nchini.Naambiwa zaidi ya timu 1500 zilijitokeza kwa mwaka huu na
maelfu ya vijana walijitokeza kuonyesha vipaji vyao. Naomba utaratibu
huu uendelee kwani utakuwa na manufaa makubwa siku za usoni.
Maombi yangu kwa TFF ni kujipanga vizuri kutambua vijana wenye vipaji
vizuri na kupanga mipango ya kuiendeleza.Ujio kwa Kombe la FIFA la Dunia
hapa nchini mbali na kuhamasisha vijana wetu pia ni fursa nzuri ya
kutangaza nchi yetu pamoja na fursa zake za utalii na uwekezaji.
Watu wengi zaidi wataifahamu nchi yetu
vizuri zaidi kupitia ziara hii ya Kombe la Dunia. Hivi sasa tuna uwanja
mpya wa kisasa ambao utaonekena vizuri wakati wa ziara hii na pengine
kuvutia timu kubwa duniani kuja kufanya mazoezi hapa wakati wa fainali
za Kombe la Dunia zitakazofanyika Afrika Kusini 2010.
Changamkieni fursa hii kwa maslahi ya
taifa letu ili tunufaike na sisi. Baada ya kusema maneno haya machache,
sasa niko tayari kufanya kazi iliyotuleta hapa sote. Nawashukuruni kwa
kunisikiliza.
|