Magari ya wizi yakamatwa
Tanzania
02/12/2009

JESHI la
polisi nchini kwa kushirikiana na ofisi za Interpol Kanda ya Kusini mwa
Afrika (SARPCCO) wameendesha operesheni maalum ya siku mbili
inayojulikana kama “NAMUTUNI” nchi nzima na kukamata watuhumiwa 110, na
vielelezo mbalimbali yakiwemo magari 54 yaliyoibwa nchi tofauti.
Polisi pia wamekamata pikipiki sita, nne kati ya hizo ziliibwa nchini
Kenya.
Magari 48 kati ya waliyokamatwa yaliibwa nchi mbalimbali ikiwemo matatu
Afrika Kusini, 38 Japan, magari manne England, na moja moja katika nchi
za Jamuhuri ya Dominic, Australia na Kenya.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba,
ameyasema hayo katika taarifa iliyosomwa na Kamishna wa polisi, Dominic
Hayuma wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Amesema, operesheni hiyo ilifanyika Novemba 23 hadi 25 na ilifanikisha
kukamata dawa za kulevya zikiwemo kete 28 za Heroine, kilo 608 za
mirungi, ekari 6 na kilogramu 801,335 za bangi, na misokoto 40 ya bangi.
“Pia tulikamata silaha mbalimbali zikiwemo bastola mbili, gobore moja,
mabomu mawili ya kutupa kwa mkono, magazine 11, SMG nne na risasi zake
607 pamoja na wahamiaji haramu (wa kinyume na sheria) 25 kutoka nchi za
Ethiopia, Burundi, Marekani, Jamaica na DRC” amesema Manumba katika
taarifa hiyo.
|