Waliohitimu (SUZA)
wapewa shahada
13/12/2009

Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, akimtunuku
Raha Ahmada Ali, Shahada ya kwanza ya Elimu ya Sanaa ya Chuo kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika mahafali ya tano ya Chuo hicho
yaliyofanyika huko viwanja vya Victoria Garden Mjini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, akimtunuku
Rashid Mohammed, Shahada ya kwanza ya Elimu ya Sayansi ya Chuo kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika mahafali ya tano ya Chuo hicho
yaliyofanyika huko viwanja vya Victoria Garden Mjini Zanzibar.

Rais wa zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, akimkabidhi
zawadi ya mfanyakazi bora Hassan Simba, katika mahafali ya 5 ya chuo
kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyofanyika huko viwanja vya
Victoria Garden Mjini Zanzibar.
HOTUBA YA RAIS KARUME KATIKA MAHAFALI
YA TANO YA CHUO CHA (SUZA):-
Mheshimiwa Waziri Kiongozi,
Mheshimiwa Naibu Waziri Kiongozi,
Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge,
Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,
Ndugu Kaimu Manaibu Makamu Wakuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,
Ndugu Wageni,
Ndugu Wanachuo,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Aleykum
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Hekima na Mjuzi wa Yote,
kwa kutujaalia afya njema, uzima na kuweza kukutana tena hapa leo hii
katika mahafali iliyojaa furaha na kheri.
Mimi binafsi na wananchi wa Zanzibar kwa jumla tuna wingi wa furaha leo
kuadhimisha kuhitimu kwa vijana wetu katika fani mbali mbali. Furaha
yangu zaidi ni kuona katika muda mfupi wa kuanzishwa chuo chetu hiki cha
SUZA tumeweza kutoa wahitimu wa kwanza wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta.
Pamoja na wao, kama tulivyokwishaelezwa, wapo wahitimu wengine wa daraja
mbali mbali katika Sayansi ya Kompyuta. Hili ni jambo la sote kujivunia.
Kama tunavyofahamu, dunia ya leo ni ya Sayansi na Teknolojia. Mambo hayo
mawili hayafanikiwi au kupatikana bila ya ujuzi wa fani ya Sayansi ya
Kompyuta. Nchi zilizoendelea kama Marekani, Japani, Ujerumani, Ufaransa
na Uingereza, miongoni mwa nchi nyingi, zimefika zilizopo kwa kutilia
mkazo elimu ya Sayansi na Teknologia ikiwemo hii ya Sayansi ya Kompyuta
kwa vijana wao tokea umri mdogo.
Kwa kufahamu hayo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeitia elimu hiyo
katika mitaala yake tokea skuli za msingi. Kwa jitihada zetu na
ushirikiano wa wadau mbali mbali, somo la kompyuta sasa linaeleweka na
watoto wetu kiasi kikubwa. Huo ni mwanzo mzuri ambao lazima tuuendeleze
kuueneza na kuukuza.
Nachukua nafasi hii kukipongeza Chuo chetu cha SUZA kwa jitihada yao
hata leo tukaweza kushuhudia kuhitimu wanafunzi kumi na moja ambao
wametunukiwa shahada zao. Aidha, nawapongeza wahitimu hao na kuwashauri
kutumia ujuzi na maarifa waliyopata katika shughuli za maendeleo ya nchi
yetu, ambazo zinahitaji sana maarifa yao .
Pia ni jambo la faraja na la kuzidi kutafakari nalo kuwa hivi sasa chuo
chetu kinaendelea kutoa wahitimu wa elimu ya sanaa na sayansi. Hao ndio
askari miamvuli wa maendeleo ya elimu katika skuli na taasisi zetu mbali
mbali. Nawapongeza wahitimu wote hao na walimu wao, pia nakipongeza chuo
na uongozi wake pamoja na Baraza la Chuo lililomaliza muda wake kwa
kufanikisha hatua hiyo ya maendeleo ya chuo.
Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti mpya wa Baraza la
Chuo, Mzee Hassan Nassor Moyo na wajumbe wake. Nawatakia kheri na
mafanikio katika dhamana zao nzito za kutoa uongozi kwa chuo ili
kiendelee kupata mafanikio zaidi. Wakati huo huo, nashauri kuwepo
ushirikiano mkubwa baina ya Baraza na uongozi wa chuo. Ushirikiano wao
ndio utakaofanikisha ustawi na maendeleo ya chuo chetu.
Nampongeza na kumshukuru pia Waziri wetu wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman kwa juhudi zake binafsi katika maendeleo
ya chuo hiki na elimu nchini kwa jumla. Nawapongeza pia watendaji wa
wizara yake kwa juhudi zao.
Ushirikiano wa viongozi na watendaji ni muhimu sana katika kufanikisha
maendeleo. Haya tunayashuhudia hapa chuoni na wizarani. Napenda
kusisitiza jambo hili ili liwe ndio msingi wa utaratibu wetu wa
maendeleo. Tukifanikiwa hivyo, itakuwa wepesi kuwashirikisha wananchi
wenyewe katika kupeleka mbele maendeleo yao .
Tuelewe kwamba mipango yetu yote ya maendeleo tunayojipangia, haiwezi
kufanikiwa bila ya ushirikiano kamili wa wananchi wetu. Hili ndilo lengo
la juhudi ya serikali yenu na ni wajibu wa viongozi, watendaji na
wananchi kwa pamoja kulitilia mkazo na kulishughulikia ipasavyo.
Ndugu Makamo Mkuu wa Chuo,
Katika kuendeleza mipango yetu ya maendeleo, kama Mpango wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umasikini, ni lazima chuo kishiriki katika kutoa
maarifa na mbinu kwa wananchi. Haya yatawezekana tukitilia mkazo mambo
ya utafiti katika fani zote tunazotumilia. Utafiti hauna kiwango au
maeneo fulani bali unawezekana kufanyika katika sekta zote ambazo tuna
watu wenye maarifa kama wahitimu na wahadhiri wa chuo. Napenda kushauri
chuo chetu, pamoja na mipango yake ya kujiimarisha na kujiendeleza, ipo
haja zaidi ya kutilia maanani suala la utafiti. Tukiangalia nchi
zilizoendelea, utafiti na matumizi ya matokeo yake ndio umekuwa chachu
za maendeleo. Tusikubali kuwekwa nyuma au kuwa na dhana kwamba hatuwezi.
Natoa wito kwa wahitimu wote waliotunukiwa shahada zao hivi leo kuitumia
vyema elimu waliyoipata kwa manufaa ya nchi, wananchi na hata familia
zao kwa jumla.
Kwa kumalizia, natoa shukurani zangu kwa wale wote wanaojitokeza
kukisaidia chuo chetu kwa njia moja au nyengine. Tunathamini sana
michango yao na nawaomba waendelee kutuunga mkono.
Nachukua fursa hii pia kuwapongeza wanafunzi wa chuo chetu kwa kuwa na
nidhamu wakati wote na ushirikiano na wakuu wao, wakiwemo wakufunzi,
wahadhiri, watendaji na wafanyakazi wengine wa chuo. Naamini huku
kunatokana na upendo wao wa chuo chao na kupenda kujinasibisha na
maendeleo yake. Ni mfano mzuri wa kuigwa na taasisi zetu nyenginezo za
elimu .
Sitawasahau wazazi, jamaa, marafiki na wahisani wa wanafunzi wetu kwa
kujitolea kwao kwa hali na mali kuwasaidia vijana wetu kufaulu. Ni
wajibu wa wanaorehemewa nao kurejesha rehema kwa waliowapa, yaani wazee
na ndugu zao pamoja na nchi yao .
Nimalizie kwa kuwakumbusha maneno ya Shakespeare:
“The quality of mercy is not strained. It drops like rain from heaven.
It is twice blessed. It blesses him that gives and him that receiveth”
Kwa kifupi ni kwamba sifa ya rehema ni kwamba inateremka kama mvua
kutoka mbinguni. Inabarikiwa mara mbili. Inambariki yule anayetoa na
inambariki yule anaepokea.
Basi wahitimu na wafadhili wa maendeleo tutafute baraka hizo.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
|