Mzee Rashid Mfaume Kawawa
afariki dunia
01/01/2010

Mzee Rashid Mfaume Kawawa amefariki dunia
jana siku ya Alhamisi ya tarehe 31/12/2009 katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili alikolazwa tokea jana baada ya kupata matatizo ya kiafya. Mzee
Rashid Mfaume Kawawa alijulikana kwa jina lingine kama "simba wa vita"
alizaliwa Liwale, Dar es Salaam, mwaka 1926 ambapo baada ya kushika
nyadhifa mbalimbali alikuwa Waziri Mkuu kuanzia Januari 22, 1962 hadi
Februari 13, 1977 akifuatiwa na hayati Edward Moringe Sokoine, baadaye
aikuwa Katibu Mkuu wa CCM kabla ya kustaafu kwake.

Picha zifuatazo ni picha zake mbalimbali
ambazo zilichukuliwa katika uhai wake. Juu pichani akiwa na na Rais
Jakaya Kikwete akiongea jambo na Mzee Rashid Kawawa katika mojawapo ya
picha za mwisho za kutumikia taifa wakati wa uhai wake.

Mzee Kawawa akiwa na mkewe bungeni Dodoma,
pamoja na utu uzima wake daima alikuwa mstari wa mbele kulitumikia taifa
katika uhai wake.

Mzee Kawawa akitunukiwa tuzo ya Amani ya
Martin Luther King na aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Tanzania.

Mzee Kawawa alikuwa hakosekani kwenye
vikao muhimu vya chama chake pale alipoalikwa katika kutumikia taifa
wakati wa uhai wake.

Mzee Kawawa akiwa mgeni rasmi kwenye
onesho la Miss Tanzania ambapo mshindi alikuwa Richa Adhia, katikati
pichani.

Mzee Kawawa aliyesimama pili kutoka
kushoto, akiwa katika baraza la kwanza la Mawaziri Tanganyika mara baada
ya uhuru mwaka 1961. Katika baraza hilo, Mzee Kawawa ndiye aliyekuwa
peke yake amebaki hai kati ya waasisi hao mpak kufa kwake jana tarehe
31/12/2009; Mungu atulindie taifa letu. Amen.

Mzee Kawawa (watatu kulia) na Mwalimu
Nyerere (wanne kulia) wakiwa pamoja na Wakuu waliopigania uhuru akiwa
katika tafrija ya kusheherekea uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Mzee Kawawa akiwa na Mwalimu Nyerere na
aliyekuwa Rais wa Zanzibar enzi hizo Mzee Aboud Jumbe huku Rais wa
Msumbiji, Samora Machel akiangalia.

Mzee Kawawa akiwa na Mwalimu pamoja na
kiongozi wa dini wa dhehebu la Ismailia duniani, H.H. Aga Khan.

Akiwa kama kiongozi wa vitendo, Mzee
Kawawa alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujiunga na jeshi la kujenga
taifa kwa mujibu wa sheria mara tu lilipoanza rasmi.

Mzee Kawawa akiwa na timu ya taifa, Taifa
Stars.

Mzee kawawa alikuwa mpenzi mkubwa wa
michezo ya mpira wa miguu na hapa akiwa kama refa katika mchezo wa
Wabunge na Mawaziri wakati wa uhai wake.

Tarehe 31/12/2009 Mzee Kawawa afariki
dunia; rasmi Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete alitangaza kifo
hicho kwa waandishi wa habari waliokusanyika ikulu, Dar es Salaam. Rais
ametangaza pia siku saba za maombolezo kitaifa ambapo bendera zitapepea
nusu mlingoti nchi nzima.

Rais Jakaya Kikwete akiongea na mwanasiasa
mkongwe, Mzee Kingunge Ngombare Mwiru baada ya kutangaza rasmi kifo cha
Mzee Rashid Mfaume Kawawa Ikulu Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam, William Lukuvi akimpa pole Mh. Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo,
Songea, ambaye mtoto wa Marehemu Rashid Kawawa nyumbani kwa marehemu,
Madale, jijini Dar es Salaam jana jioni.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam, William Lukuvi akimfariji mke wa Marehemu Rashidi Mfaume Kawawa,
Asina Kawawa, wakati alipoitembelea familia ya marehemu nyumbani kwa
marehemu, Madale, jana jioni.

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf
Makamba (kushoto) akimlilia Mzee Rashid Kawawa wakati alipokwenda
nyumbani kwa marehemu, Madale, jijini Dar es Salaam jana jioni.

Mzee Yusuf Makamba
akimfariji Zainab Kawawa mtoto wa marehemu Rashidi Kawawa, Madale, jana
jioni.

Leo tarehe 01/01/2010,
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete walikwenda kutoa
heshima za mwisho kwa marehemeu Mzee Rashid Mfaume Kawawa katika ukumbi
wa Karimjee jijini Dar es Salaam jioni hii. Mamia ya wananchi wamefurika
ukumbini hapo kumuaga Mzee Kawawa anayetarajiwa kuzikwa nyumbani kwake
Madale kesho Jumamosi.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete
na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiifariji familia ya Marehemu Mzee Rashid
Mfaume Kawawa muda mfupi baada ya kutoa heshima za mwisho.
|