Uraia wa Nchi Mbili
(Tanzania Diaspora)
20/01/2010

Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe akifungua mkutano wa majadiliano
baina ya wataalamu wa Tanzania na wa nje ya nchi kuhusu uwezekano wa
kuwashirikisha kikamilifu Watanzania walio nje ya nchi. Mkutano huo
unaratibiwa na Wizara ya Nje ambayo tayari wameshaunda Idara ya
DIASPORA.

WAZIRI wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe amesema kuna haja ya kubadili
sheria ya uraia ya Tanzania ambayo haimruhusu Mtanzania kuwa na
uraia wa nchi mbili kwani sheria hiyo, imepitwa na wakati na haimpi
hamasa mtanzania mwenye uraia wan je kuisaidia nchi yake kwa kuwa
anakuwa amepoteza uraia wake.
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam jana alisema serikali hivi sasa
inalifanyia kazi suala la maombi ya uraia wa nchi mbili na wadau
husika wameshaombwa kutoa ushauri.
Alisema kuna haja ya
watanzania wanaoishi nje ya nchi kupatiwa uraia wa nchi mbili ili
waweze kuchangia na kuwekeza katika rasilimali zilizopo nchini kwa
lengo la kuleta maendeleo.
"Tunatumaini kulimaliza
suala hili hivi karibuni kwa faida ya wadau wote na taifa letu kwa
ujumla," alisema.
Alisema kwa serikali
kuruhusu uraia wa nchi mbili kutatoa fursa zaidi kwa wadau kufaidika
na haki muhimu ambazo wanatakiwa kupata.
"Kwa kuongeza kipato
wakiwa katika mataifa hayo, Watanzania wataweza kuwasaidia wenzao
wanaobaki nchini na hivyo kupunguza hali ya umasikini nchini,"
alisema Waziri Membe.
Membe alisema katika
kipindi chote cha uhuru hawakuangalia hilo ila sasa kuna haja
kuwashirikisha watanzania wanaoishi nje ili kuleta Tanzania
maendeleo.
Alisema wizara ya mambo
ya nje imeanzisha idara maalumu ili kujua takwimu za watanzania
wanaoishi nje ya nchi kwa kuwatambua kwa vipaji na utaalamu walio
nao.
Alisisitiza kuwa
watanzania tunaoishi hapa nchini tuwaone wanaoishi nje kama wenzetu
na sio kuwatenga pindi watakapopata nafasi ya kupata urai.
Baadhi ya watanzania
wanaoishi nje walipata nafasi ya kuchangia katika mkutano huo na
kusema kuwa kuna sababu nyingi zinapzowafanya kushindwa kuchangia
maendeleo ya nchi yao.
Akizungumza na waandishi
wa habari Mkurugenzi na Mtaalamu wa nyumba mpya na upangishaji
Daniel Mwasandunge ambaye ni mtanzania anayeishi Uingereza alisema
kuwa kutokana na nchi kutokuwa na takwimu za wanaoishi nje na
taaluma walizonazo imeshindwa kutafuta wataalamu kuanzia wafanyakazi.
"Serikali haina takwimu
za watanzania tunaoishi nje na wala haijui taaluma tulizo nazo,
hivyo inashindwa kupata wataalamu kuanzia wafanyakazi.
"Tunataka nafasi za ajira
zitangazwe kule kama zinavyotangazwa huku kama zipo, kwani
tunapofanya kazi tunategemea maisha fulani," alisema Mwasandunge.
|