Hatua za haraka
zichukuliwe kwenye miundombinu - KIKWETE
25/01/2010

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ametaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka kutengeneza upya
miundombinu nchini, hasa reli na barabara, iliyoharibiwa kutokana na
mvua na mafuriko ya wiki za karibuni katika baadhi ya mikoa nchini.
Mheshimiwa Rais pia amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za
kiraia na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kukabiliana na
kazi ya kukarabati miundombinu hiyo.
“Uchumi huu utaishiwa sana nguvu kama hatukushughulikia haraka suala la
kukarabati miundombuni na hasa reli,” Rais Kikwete amekiambia kikao cha
dharura alichokiitisha mchana wa leo, Jumatatu, Januari 25, 2010, Ikulu,
Dar es Salaam, kujadili kiwango cha uharibifu na jinsi ya kunusuru
miundombinu ya reli na barabara.
Rais Kikwete aliagiza kufanyika kwa kikao hicho Ijumaa iliyopita,
Januari 22, 2010, wakati alipoendesha kikao cha Baraza la Mawaziri.
Waziri wa Miundombinu, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa amewaongoza
maofisa waandamizi kutoka wizara yake na kutoka baadhi ya makampuni na
mashirika yaliyoko chini ya wizara yake, ikiwamo Kampuni ya Reli
Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara (Tanroads) katika kikao cha leo.
Katika kikao hicho, maofisa hao walimweleza Rais Kikwete uharibifu
uliofanyika katika Reli ya Kati na hasa kati ya Stesheni za Gulwe na
Kilosa, katika mikoa ya Dodoma na Morogoro, kutokana na mvua
zilizonyesha katika wilaya za Mpwapwa na Kilosa kati ya Desemba 24,
mwaka jana, 2009 na Januari 10, mwaka huu, 2010.
Katika maeneo ya Kilosa, mvua hizo na mafuriko yaliyoandamana na mvua
hizo, yameng’oa kabisa sehemu ya Reli ya Kati na kusimamisha huduma za
reli hiyo kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Sababu kubwa za uharibifu huo ni kufurika na kwa mito ya Mkondoa na
Kinyasungwi, hali iliyosababisha kuhama kwa mito hiyo kutoka katika njia
za asili na kuelekea kwenye tuta la reli.
Maofisa hao wamemweleza Rais Kikwete kuwa zipo sehemu 28 zilizoharibika
kati ya stesheni hizo mbili lakini ni sehemu 26 zilizoaharibika zaidi.
Pia wamemweleza kuwa madaraja tisa yamesombwa na maji na mengine matatu
yako katika hatari ya kusombwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mhandisi Omar Chambo pia
amemweleza Rais Kikwete mipango ya ukarabati wa sehemu hiyo ya reli na
kuahidi kuwa kazi hiyo inaweza kuwa imekamilika kati ya miezi miwili na
miezi mitatu.
Kuhusu uharibifu kwenye barabara, Mhandisi Chambo amesema kuwa uharibufu
kwenye barabara umefanyika katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
Mikoa hiyo ni Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Kilimanjaro, Kigoma, Lindi,
Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga,
Singida, Tabora na Tanga.
Mhandisi Chambo amesema kuwa kiasi cha sh bilioni 13.286 zinahitajika
kuweza kukarabati barabara hizo ambazo zimeharibika kwa viwango tofauti
huku uharibifu mkubwa ukiwa umetokea katika Mkoa wa Dodoma ambako
barabara zake tatu hazipitiki.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Januari, 2010
|