Serikali ya mseto
kufanyika Zanzibar
31/01/2010

HATIMAE
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeidhiria hoja ya kuundwa kwa serikali
ya kitaifa kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.
Hoja
hiyo iliyowasilishwa na kiongozi wa kambi ya upinzani Abubakar Khamis
Bakari, inayotaka kuundwa kwa serikali hiyo ili kujenga umoja na
maridhiano kwa Wazanzibari ambayo wamekuwa katika migogoro ya kisiasa
kwa muda mrefu.
Wajumbe wa baraza hilo wote kwa sauti moja walikubaliana na suala hilo
kwa kuridhia baaada ya Baraza la Wawakilishi kuwasilisha mapendekezo ya
hoja binafsi ya chama cha wananchi, CUF, na kujadiliwa na Mwakilishi
huyo wa Jimbo la Mgogoni, Pemba.
Hata hivyo kabla ya kufanyika kwa mabadiliko hayo CUF walikubali kufanya
mabadiliko katika hoja zake kadhaa baada ya wajumbe wa CCM kutaka
kufanyiwa mabadiliko hayo ya hoja yake.
"Marekebisho ya sheria ya uchaguzi, hatua ya kutaka ridhaa ya wananchi
kwa njia ya kura ya maoni, na marekebisho ya katiba endapo wananchi
wataridhia uanzishwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa, yote hayo
yafanywe kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010," kilisema kipengele hicho
ambacho kimekubaliwa na wote.
Katibu wa baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee akisoma vipengele
vilivyoridhiwa na baraza hilo alisema, pamoja na kukubaliwa kuundwa kwa
kamati ya wajumbe sita ambao watasimamia suala hilo watatu wataotoka
upinzani na serikalini.
Aidha Baraza hilo alisema limekubali suala la wakuu wa mikoa waendelee
kuwa wanasiasa, lakini bado wateuliwe na rais kwa kufuata uwiano wa kura
za rais za vyama viliomo kwenye Baraza kwa vyama vya siasa vilivyomo
humo ama waondolewe kabisa katika vyama vya siasa ili wasiwe wateuliwa
wa Rais.
Nafasi ya makamu wa rais ambayo ilikuwa na utata kidogo baada baadhi ya
wajumbe kuwa na wasi wasi nayo juu ya mfumo utakaotumika kuunda nafasi
hiyo bila ya kuingilia vipengele vya katiba vya muungano.
Hoja hizo zilizuka baada ya wajumbe hao kuuliza iwapo nafasi hiyo
ikaleta utata wa kisheria katika katiba ya muungano kwa kuwa tayari
nafasi hiyo imetajwa katika nafasi ya muungano na haitawezekana kuwa
makamu wa pili kutoka Zanzibar.
Hoja nyingine kuhusu suala hilo kuwepo utata pindi rais aliteteuliwa
pamoja na wateuliwa wengine wakiwewa pingamizi kwa mujibu wa tume ya
uchaguzi je nafasi hiyo itaweza kupatikana hivi ambapo upande wa
upinzani wanapendekeza suala hilo lipelekwe kwa wajumbe wa baraza la
wawakilishi kwa ajili ya kuteuliwa kwa mujbu wa kura.
Akijibu hoja hizo Bakari amesema haoni haja ya kuwa na wasi wasi huo kwa
kuwa suala hilo litaingizwa katika mapendekezo ya marekebisho ya katiba
na baadae kuwasilishwa katika kikao cha baraza la wawakilishi jambo
ambalo litawapa nafasi ya kutoa maoni yao juu ya uendeshaji wa suala
hilo.
Hata hivyo suala la hoja ya makamu wa raias wa muungano Bakari alisema
hakuna utata wowote kwa kuwa huyo atakuwa ni makamu wa rais wa Zanzibar
kama vilivyo nafasi nyengine za mawaziri wa Zanzibar.
Awali jana wawakilishi hao walionekana kuzungumza lugha laini tofauti ya
siku ya kwanza katika kuchangia hoja binafsi iliyowasilishwa na kiongozi
wa kambi ya upinzani Abubakar Khamis Bakari.
Wakichangia hoja hiyo wajumbe mbali mbali kutoka CCM na CUF walionekana
kutumia busara zaidi kuliko katika michango yao tofauti kabisa na siku
ya mwanzo waipokuwa wakichangia hoja hiyo kwa kuwa zaidi upande wa CCM
walionekana kusimamia hoja ya Butiama zaidi kuliko kukubaliana na hoja
hiyo.
Ingawa baadhi ya wajumbe wao tokea kuanza mjadala huo walionekana
kulainika mapema na kuwataka wenzao watumie hekima na busara zaidi
katika michango kama walivyoelekezwa na Spika wa baraza hilo, Pandu
Ameir Kificho, kuwataka kuwa makini zaidi na michago yao ili kujenga na
kuepukana na jazba ambazo zimezoeleka katika vikao vya baraza hilo.
Mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM) Ramadhani Nyonje Pandu aliwahimiza
wajumbe wenzake kuona umuhimu wa hoja hiyo na kuwataka waiunge mkono na
kuacha kuvutana kwani hoja hiyo ikiwachwa itaweza kusababisha matatizo
makubwa nchini.
"Napenda kwa mara ya kwanza nimsifu na kumpongeza maalim Seif kwa
kukomaa kwake kisiasa na ukomavu wake wa kutaka mazungumzo ya kujenga
umoja, mashirikiano na utulivu katika nchi yetu," alisema Pandu.
Mwenyekiti wa baraza la wawakilishi Ali Mzee Ali (CCM) naye aliunga
mkono hoja na kuwataka wajumbe wenzake waungane kwani ni kitu kizuri
kilichoanzishwa na ni muhimu sana kwa kuwaunganisha Wazanzibari ambao
wamekuwa katika mazungumzo na hakuna haja yoyote ya kuikata hoja hiyo
ambayo lengo lake ni kuwaunganisha Wazanzibari.
"Nakuombeni sana hoja hii tuipitishe kwa furaha na tusiwe na pingamizi
hapana pahala mazuri kama hapa serikali ya shirikisho, umoja wa kitaifa
ni mhimili mkuu katika nchi na Rais Karume yeye ndio kisiwa cha amani na
utulivu jina lake Amani na anapenda amani na amani ndio hii tayari,"
alisema.
Mwakilishi wa jimbo la Mkanyageni (CUF), Haji Faki Shaali alisema suala
la kura ya maoni linatia hofu kutokana na historia kuwepo na shaka juu
ya suala hilo kwa kuwa mara nyingi kura hizo huwa hazipigwi kwa haki na
inavyotakiwa na ndio maana baadhi ya watu wengine huwa hawalitaki maana
linaweza kusababisha mivutano kama ile ya uchaguzi ambayo mara huwagawa
wananchi.
Mwakilishi aliyeteuliwa na rais, Juma Duni Haji (CUF) alisema
haiwezekani kwa Wazanzibari kila baada ya miaka mitano kwanza wapigane
na wauane ndio wapate rais kwanza jambo ambalo alisema wananchi
wanapaswa kulikataa suala hilo kwani linaleta hasara kubwa katika jamii.
Alisema ni vizuri kutayarishwa kwa mazingira mazuri ili kuelekea
uchaguzi mkuu na bila ya hivyo ni hatari kuingia katika uchaguzi kauli
ambayo iliungwa mkono na waziri wa maji, ujenzi, nishati na ardhi,
Mansoor Yussuf Himid ambaye kwa upande wake alisema hakuna haja ya
kukimbilia uchaguzi wakati mazingira ni mabaya.
Mwakilishi wa Gando (CUF), Said Ali Mbarouk akichangia hoja hiyo alisema
mawaziri wapatikane kwa kura na ukifanywa utaratibu wa wingi wa viti
huenda vyama vidogo vikateketea na kupotea kabisa kwani chama kupata
asilimia 10 ya kura za rais halafu kukiwacha nje haitakuwa vyema
tutakuwa na vitakavyopata asilimia 5 na 10 na kupendekeza kwamba vile
viti viwili vya upinzani wapewe wao maana wakiwekwa nje watakuwa ni
waangalizi katika suala la demokrasia jambo ambalo sio zuri.
Salma Said, Zanzibar.
|