Habiba Kawawa afariki
dunia
08/02/2010

Marehemu Habiba Kawawa amezikwa jana jioni
huko Moshi katika maziko ambayo mwanasheria wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya,NHIF, Christina alipata shida ya kumalizia wasifu wa Marehemu.
Habiba aliyezaliwa Desemba 21,1975 jijini Dar es Salaam na kupata elimu
yake ya msingi mwaka 1982 hadi 1988 katika shule za msingi za Karume na
Kiluvya zote za Dar es Salaam alisomea Sekondri za Weruweru na Kibosho
mkoani Kilimanjaro ni mtaalamu wa sheria.
Habiba alipata elimu yake ya sheria IDM - Mzumbe kuanzia mwaka 1995 hadi
mwaka 1997 alipofanikiwa kupata diploma ya Sheria.Alijiunga na chuo
kikuu cha Dar es salaam 1998 na kutunukiwa shahada ya sheria mwaka 2001.
Juni 15,2006 alifaulu mtihani wa uawakili na kutunukiwa cheti cha
uwakili. Wakati anakufa alikuwa anaandika 'thesis' ya digrii yake ya
pili ambayo alikuwa akiipata kutoka Chuo Kikuu cha Capetown. Habiba
ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha Sheria na kile cha wansheria
wanawake alishawahi kuwa mwandishi wa habari kwa muda mfupi katika miaka
ya 1995 na 1996 katika magazeti ya Habari Corporation chini ya usimamizi
wa Jenerali Ulimwengu na John Bwire.
Mwaka 1997 aliingia Halmashauri ya Jiji la dar es salaam kama Afisa wa
Sheria Msaidizi na kupanda ngazi kufikia Afisa Sheria mwaka 2001. Mwaka
2006 alijiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya kama Afisa Sheria
Daraja la Pili, akapanda cheo kuwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Sheria na
mwaka huu aliteuliwa kuwa Meneja Mradi wa Huduma za kinamama wajawazito
wasio na uwezo na wanaoishi na virusi vya ukimwi, nafasi aliyoshika hadi
umauti unamkuta.
Akiwa kama mtaalamu wa sheria na wakili, Habiba aliwasaidia watu wasio
na uwezo wa kifedha mahakamani na kuwatetea. Marehemu Habiba ambaye
alikuwa mjamzito usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu ya tarehe Mosi mwezi
huu wa Februari alifika hospitalini kuona daktari wake na alimshauri
kupumzika hospitalini hapo kuangaliwa mwenendo wa presha yake.
Alhamisi ya tarehe 4 marehemu aliwapa matumaini watu wote waliokwenda
kumjulia hali na kuonge anao na hata kusaini baadhi ya nyaraka za ofisi
yake ili kuwezesha mchakato wa mradi wa huduma za kminana wajawazito
wasio na uwezo na wanaoishi na virusi vya ukimwi uweze kuendelea. Saa
kumi jioni hali ilibadilika na saa 11.30 jioni Habiba alifariki dunia.
Habiba alifunga ndoa na Johnson Maleko Aprili 29,2000 na katika ndoa yao
walibahatika kuwa na mtoto Anna Asia Maleko ambaye sasa ana miaka 7.
Mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake na
amlaze pahala pema peponi, Amen.
|