UK Border Agency yataka
wanafunzi wafuate sheria
21/02/2010

Sheria kali zilizoanzishwa nchini
Uingereza kuhusu wanafunzi kutoka nje ya ulaya wanaokuja nchini humo kwa
masomo zitawafanya wanafunzi wengi kutoka barani Afrika kutoweza kusomea
Uingereza.
Idara ya uhamiaji Uingereza - UK Border Agency, imesema watu wengi
wametumia vibaya na kukiuka sheria za uombaji wa viza hasa za wanafunzi.
Serikali ya Uingereza imeongezea vikwazo
kupiga vita ukiukaji wa sheria hizi. Ukiukaji wa sheria umekuwa
ukifanyika kufuatia kukomeshwa kwa uchunguzi uliokuwa ukifanywa
kuhakikisha kwamba wanafunzi wanarudi nchini mwao baada ya kumaliza
masomo yao na mda waliopewa na idara ya uhamiaji Uingereza kumalizika.
Ingawaje wanafunzi wanachunguzwa kabla ya kupewa viza, hawajakuwa
wakichunguza hivi karibuni kuhakikisha kwamba wamerudi nchini
mwao.Imekuwa vigumu kujua idadi ya wale wanaorudi na wale wanaoishi
Uingerza kinyume cha sheria. Idara ya uhamiaji inasema kwamba itakuwa
vigumu sana kuvunja sheria za uhamiaji siku zijazo. Mnamo mwaka 2011,
Idara hiyo itakuwa na teknolojia ya kipekee duniani kuwachunguza watu
wakiingia na kutoka Uingereza.
Idara hii imeanzisha vikwazo mbalimbali
ambavyo wanafunzi wengi kutoka nchi za kigeni wanasema ni vikali mno.
Mwaka uliopita mwezi Machi, Idara ya uhamiaji ilibadilisha taratibu
ambazo wanafunzi kutoka nchi zingine hutumia kuomba viza za kuja
Uingereza na kuanzisha mfumo ujulikanao kama Tier 4 Points based system.
Katika mfumo huu, vyuo vyote vya elimu ya juu ni lazima vijiandikishe
katika idara ya uhamiaji. Vikitimiza mahitaji yote, vitapewa leseni ya
kuwaleta wanafunzi kutoka nchi mbalimbali hapa Uingereza. Wanafunzi nao
wanahitajiwa kuwa na pointi arubaini ndio watapewa viza. Wanafunzi
watashinda pointi thelathini wakipewa barua ya kuomba viza kutoka chuo
ambacho kimesajiliwa. Watashinda pointi kumi kama watakuwa na karo yote
na pesa za matumizi za mwaka mmoja.
Wakitaka kuongezea mda wa viza zao wakiwa
Uingereza, watahitajiwa kuonyesha kwamba wamekuwa na kiasi cha pauni 800
kila mwezi, kama chuo chao kiko mjini London na pauni 600 kila mwezi
kama chuo chao kiko nje ya mji wa London.
Kabla ya kuongezewa mda wao kama wanafunzi, wale wanaoishi mjini London
watahitajika kuonyesha kwamba kiasi cha £ 1600 kimekuwepo kwenye akaunti
yao ya benki kwa mda wa siku 28. Wale wanaoishi nje ya mji wa London,
watatakiwa kuonyesha wamekuwa na kiasi cha £ 1200 kwenye akaunti yao ya
benki kwa mda wa siku 28.
Wanafunzi watakaopewa fursa kufanya kozi
za muda mfupi wataruhusiwa kufanya kazi kwa masaa kumi kila wiki lakini
kama wanasomea shahada, wataruhusiwa kufanya kazi masaa 20.
Wanaopinga hatua hii wanasema vikwazo hivi havijafanikiwa. Dr. Zakir
Hussein, mkuu wa chuo cha London Trinity , anasema hivi vikwazo
vimefanya wanafunzi wengi kuja Uingereza wakiwa hawawezi kuzungumza
Kiingereza, wengi wao wakitoka bara la Asia.
Idara ya uhamiaji Uingereza imesimamisha
kwa muda uombaji wa viza kutoka kaskazini mwa India, Nepal na
Bangladeshi. Walichukua hatua hii kufuatia kuongezeka kwa idadi ya
wanafunzi walioomba viza eneo hilo kutoka 2,000 mwaka 2008 hadi 13,500
mwaka uliopita. Mabadiliko haya yatawaathiri vibaya wenye vyuo ambavyo
havitoi shahada.
Jeremy Oppenheim ambaye ni mkuu wa mfumo wa Tier 4 Point based amesema
kwamba kuanzia mwezi Machi mwaka huu, idara ya uhamiaji itawapa viza
wanafunzi watakaopata nafasi kwenye vyuo ambavyo vitatoa shahada na
zaidi . Mfumo huu utamaliza mafunzo yote ambayo wanafunzi hawatapewa
shahada.
David Game, mkuu wa muungano wa vyuo wa
David Game group of colleges, amesema kama serikali ya Uingereza
itafuata sera hii kwa makini, basi utakuwa mwisho wa vyuo kama vyake.
Kama idara ya uhamiaji itachukua hatua hiyo, David anasema yeye ataacha
nchi yake na kuanzisha vyuo vya elimu ya juu nchi zingine.
|